Prime
Sura tofauti za Profesa Sarungi

Muktasari:
- Wanataaluma na wanasiasa wakongwe wamemzungumzia Profesa Sarungi, kuwa alikuwa mtu aliyependa kazi yake, aliyejitoa katika kutoa huduma kwa wagonjwa na kutoa mawazo yaliyosaidia kuboresha sekta ya afya nchini.
Dar es Salaam. Profesa Philemon Sarungi, gwiji wa tiba ya mifupa nchini Tanzania, ameaga dunia akiwa na umri wa miaka 89, huku historia yake ikibaki kuwa mwanga kwa vizazi vijavyo.
Akiwa daktari bingwa wa kwanza wa upasuaji wa mifupa nchini, mchango wake hauishii tu katika taaluma ya tiba bali unagusa maisha ya maelfu, likiwemo tukio la kihistoria la kumuokoa majeruhi wa ajali ya treni kwa kuukata mguu ulionasa kwenye behewa.
Katika kumbukumbu zao, wanasiasa, wanataaluma, na binti yake Maria Sarungi Tsehai, wamesifu ujasiri, weledi, na uzalendo wake usio na kifani.
Mbali na kuwa mbunge, waziri na kwenye nafasi alizokuwa nazo, Profesa Sarungi bado aliweza kutumia taaluma yake ya udaktari kuokoa maisha ya watu.
Zito Kabwe, mmoja wa wanasiasa aliyekutana naye bungeni, amemwelezea Profesa Sarungi kwamba alikuwa mmoja wa wazee waliomlea, alipoingia bungeni kwa mara ya kwanza.
Pia, binti yake Maria amesema baba yake aliwalea kwa kuwafundisha umuhimu wa nidhamu, upendo wa dhati kwa watu wote na kupenda usawa na haki kwa kila mtu, bila ubaguzi.
Akizungumza na Mwananchi kutoka Nairobi nchini Kenya, Maria amesema baba yao aliwafundisha nidhamu na kupenda usawa na haki kwa wote.
Maria ambaye ni mwanaharakati wa kutetea haki za binadamu, amesema baba yake ni kizazi cha vijana walioshiriki kujenga msingi ya Taifa changa la Tanganyika baada ya uhuru wa mwaka 1961.
“Kwa hiyo alituimarisha sana katika kulitumikia Taifa kwa uaminifu, lakini pia alipenda mijadala na kusikiliza maoni ya kila mtu, hadi mwisho wa maisha yake alikuwa mtu wa kujitoa kumsaidia yeyote kwa njia yoyote, hakuwa mbinafsi.
“Ametuachia jambo muhimu kuliko vyote, misingi imara ya kuwa binadamu mwenye utu na mpenda haki,” amesema Maria.
Wanataaluma wamzungumzia
Aliyewahi kuwa mkurugenzi mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Profesa Lawrence Mseru amesema yeye ni mmoja wa waliopita mikononi mwa Profesa Sarungi katika hospitali hiyo.
“Mwaka 1970 alirudi (Profesa Sarungi) kutoka masomoni, akaenda Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) na kuanzisha kitengo cha tiba ya mifupa na majeruhi ambapo alikuwa peke yake, akapambana kuanzisha idara na ilipofika mwaka 1976 kitengo kikawa idara kamili.
“Mwaka 1976 ilipoanza idara akaanza kuajiri wataalamu wa kumsaidia, miongoni mwa watu wa mwanzo alikuwepo Profesa Kessy (marehemu), aliyekuwa mkuu wa chuo cha KCMC,” amesema.
Wengine ambao aliwataja kwa jina moja moja ni Dk Chaga (marehemu), Dk Mhina, Dk Sharif pamoja na yeye akisema wao ndiyo walikuwa watalaamu wa mwanzoni kuajiriwa chini ya Profesa Sarungi.
Profesa Mseru amesema mchakato wa kuajiriwa watalaamu hao ulikwenda sambamba na kuwasaidia watu kwenda nje ya nchi katika mataifa ya Uholanzi na Ujerumani Magharibi kuongeza elimu zao.
Amesema wakati huo idara ya tiba ya mifupa na majeruhi ilikuwa inasifika kwa uchapakazi na kutoa huduma bora ndani ya MNH kutokana na uhodari wa Profesa Sarungi.
MOI ilivyozaliwa
Profesa Mseru ameongeza: “Profesa Sarungi alikuwa na mawazo ya kwamba ni muhimu kuboresha miundombinu ya kutolea huduma na vifaa ili watalaamu waweze kufanya kazi vizuri.
“Hili wazo liliendelea hivi hadi miaka ya 80 mwishoni, alipotokea daktari mmoja kutoka Uswisi, Dk Uma Gro, aliyetafsiri pamoja na Sarungi aliyekuwa waziri wa afya wakati huo, kwamba kuna haja ya kuboresha miundombinu. Ndipo wazo hili lilipozaa Moi iliyojengwa miaka ya 90.
“Ninachoweza kusema sisi tuliopita chini ya Profesa Sarungi, alitujenga kuheshimu kazi, kujali mgonjwa. Lakini kikubwa ni kuangalia mbele, ukiangalia historia ya Moi ni wao (Profesa Sarungi na Dk Grob) walionyesha njia ya kutaka itoe huduma za kibobezi ndani ya taasisi ya umma,” amesema Profesa Mseru.
Akutana na Dk Maua Daftari
Dk Maua Daftari ambaye amekuwa naibu waziri kwenye wizara kadhaa amesema alionana na Profesa Sarungi wakati akifanya mafunzo kwa vitendo katika Hospitali ya Taiafa Muhimbili katika wodi ya watu waliovunjika miguu na viuno.
“Katika mafunzo yetu tulikuwa kama tisa, wote walikuwa wanamwogopa Profesa Sarungi kwa sababu alikuwa mkali. Mimi nilikwenda naye vizuri kwa sababu nilifuata anavyotaka, ikiwemo kuwandaa wagonjwa vizuri kabla ya kwenda katika chumba cha upasuaji,” amesema Dk Daftari.
Kwa mujibu wa Dk Daftari, Profesa Sarungi akiingia chumba cha upasuaji saa mbili asubuhi anatoka saa 12 jioni, kama kuna wagonjwa wanane wa upasuaji, kubwa anahakikisha anawamaliza wote.
“Alikuwa hataki upambavu katika kazi zake, lakini kubwa zaidi alikuwa anakumbuka kila mgonjwa na anachoumwa katika wodi waliyolazwa yenye watu kati ya 20 hadi 30,”amesema Dk Daftari.
Dk Daftari amesema kwenye operesheni zilizofanywa na Profesa Sarungi nyingi wagonjwa walikuwa wanatoka salama bila vidonda, hivyo kuwarahisishia kazi wauguzi na madaktari.
“Alikuwa halali yule baba (Profesa Sarungi), Serikali iangalie namna ya kumpa nishani kutokana na juhudi zake. Kipaumbele cha Profesa Sarungi ilikuwa ni wagonjwa wake kwanza,” amesema Dk Daftari.
Sambamba na hilo, Dk Daftari amesema Profesa Sarungi alikuwa mtalaamu aliyejitolea katika kutoa huduma katika ajali mbalimbali zilizotokea, ikiwemo wa treni.
“Nikiwa naibu waziri wa mawasiliano na uchukuzi, ilitokea ajali ya treni (Msagali na Igandu, Dodoma) tukamuomba Rais madaktari na Profesa Sarungi (akiwa waziri) alisaidia sana na alikuwa mwepesi kwa kila tukio, iwe mchana au usiku, iwe mvua au jua anashiriki,” amesema Dk Daftari.
Simulizi hiyo, imeungwa mkono na Mudhihir Mudhihir, mbunge wa zamani wa Mchinga, mkoani Lindi kuhusu anavyokumbuka Profesa Sarungi (akiwa Waziri wa Ulinzi) katika ajali hiyo ya treni alivyoshirikiana na Dk Daftari kutoka huduma.
“Profesa Sarungi na madaktari wenzake, kina Profesa David Mwakyusa na Dk Maua Daftari waliongoza uokoaji kuanzia asubuhi hadi jioni.
“Nakumbuka mtu mmoja mguu wake ulinasa, lakini alikuwa hai, basi Profesa Sarungi aliukata palepale ule mguu ili kuokoa maisha yake. Unaweza kuona namna alivyokuwa na msaada kwa watu wengine,”amesema Mudhihir ambaye aliwahi kuwa Naibu Waziri wa Michezo.
Alichoeleza Zitto
Mbunge wa zamani wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe amesema alipochaguliwa mbunge mara ya kwanza mwaka 2005, alipata wazee watatu kama walezi wake bungeni kwa kujitolea kwao.
“Mzee William Shelukindo alinifundisha namna nzuri ya kuandika maswali ya bungeni. Mzee Jackson Makwetta na Profesa Sarungi walikuwa wakinichukua kwenda kunywa chai au kahawa mara kwa mara kuchambua nilichozungumza bungeni na kunionyesha maeneo ninayopaswa kuboresha.
“Kupitia malezi hayo ya Mzee Sarungi ndipo nilikutana na binti yake Maria Sarungi Tsehai kwa mara ya kwanza katika viunga vya Bunge mwaka 2006.
“Mzee Sarungi aliendelea kuwa Mzee wangu kwa muda mrefu akinipa nasaha katika vipindi mbalimbali vya maisha yangu ya siasa,” amesema Zitto.
Kwa upande wake, Profesa Amandina Lihamba ambaye aliwahi kufanya kazi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), ameelezea masikitiko yake kwa kifo cha Profesa Sarungi.
“Ingawa hatukuwa karibu sana, lakini Profesa Sarungi alikuwa ni mtu anawajibika katika kazi, aliichukulia kazi yake kwa uzito mkubwa na aliwavutia wengine kufanya hivyo.
“Hii itakuwa mojawapo ya alama zake aliyoaicha kwa wengi waliomfahamu,” amesema Profesa Lihamba.
Historia yake
Profesa Sarungi alikuwa mwalimu, daktari wa upasuaji na mtaalamu wa mifupa, waziri, mbunge na mwanamichezo.
Alizaliwa Machi 23, 1936 huko Tarime, mkoani Mara, wazazi wake ni Sarungi Igogo Yusufu na Amimo (Maria) Sarungi.
Mwaka 1966, Sarungi alipata Shahada ya Tdaktari wa Tiba kutoka Chuo Kikuu cha Tiba, Szeged, Hungary.
Mwaka 1970, alihitimu Shahada Uzamivu ya Upasuaji kutoka Chuo Kikuu cha Tiba, Szeged, Hungary. Alihitimu diploma katika tiba ya upasuaji wa mifupa na madhara ya ajali kutoka Chuo Kikuu cha Tiba, Vienna, mwaka 1973.
Pia, mwaka 1975 alihitimu diploma katika upasuaji wa upandikizaji viungo kutoka Chuo Kikuu cha Shanghai, China.
Kuanzia mwaka 1971 hadi 1973, Sarungi alifanya kazi kama mhadhiri wa upasuaji katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na mhadhiri mkuu mwaka 1973-1976.
Pia, Sarungi alifanya kazi kama Profesa mshiriki katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, mwaka 1977-1979 na kuwa Profesa mwaka 1979 na mkuu wa idara mwaka 1977-1984 katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Kuanzia mwaka 1984-1990, Sarungi alifanya kazi kama Mkurugenzi Mkuu katika Kitivo cha Tiba cha Muhimbili cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Alikuwa pia Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu mwaka 1989-1991.
Pia, kuanzia mwaka 1990-1992, Sarungi alikuwa Waziri wa Afya, Waziri wa Mawasiliano na Usafirishaji 1992-1993 na tangu mwaka 1993 amekuwa Waziri wa Elimu na Utamaduni na pia Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.
Pia, Sarungi mwanachama wa CCM tangu mwaka 1971. Pia, ni Mjumbe wa Chama cha Madaktari Tanzania na Chama cha Madaktari wa Upasuaji wa Afrika Mashariki.