Hiki ndicho kilichomuua Profesa Sarungi, mdogo wake naye afariki dunia

Profesa Phelemon Sarungi enzi za uhai wake. Picha na Mtandao
Muktasari:
- Mdogo wake marehemu Profesa Sarungi aitwaye Emmanuel Sarungi amefariki dunia hii leo Alhamisi Machi 6, 2025.
Dar es Salaam. Familia ya Profesa Philemon Sarungi (89) imetaja sababu ya kifo cha bingwa huyo wa upasuaji na tiba ya mifupa ni moyo.
Profesa Sarungi alifariki dunia jioni ya jana Jumatano, Machi 5, 2025 nyumbani kwake Oysterbay jijini Dar es Salaam.
Akizungumza leo Alhamisi, Machi 6, 2025 nyumbani kwa marehemu na waandishi wa habari, mtoto wa mdogo wake marehemu, Sabasaba Sarungi amesema baba yake mkubwa (Profesa Sarungi) alikuwa na tatizo la moyo alikuwa nalo kwa muda mrefu ingawa halikuwa inampa shida kutekeleza majukumu yake.
“Kwa sasa wanaosubiriwa ni watoto wa marehemu walioko nje ya nchi na baadhi ya ndugu wafike kisha tutatoa taarifa rasmi ya maziko ya mzee wetu,” amesema Sabasaba.
“Alikuwa na changamoto ya moyo ila hadi jana alikuwa mzima na alipata wageni, ameshinda nao wakala wote na daktari wake wa mazoezi alikuja wakafanya mazoezi. Ilipofika saa kumi jioni akajisikia vibaya kumbe ndio tatizo la moyo lilitokea ghafla basi saa 11:10 jioni akafariki,” amesema.
Amesema mwaka 2021, Profesa Sarungi aliyewahi kuwa waziri wa zamani na mbunge wa Rorya alipata ajali ya kuteleza na kuanguka akavunjika mguu ambapo akawa anatumia kiti mwendo kwa kuwa hakuwa anaweza kutembea.
Msiba mwingine umetokea leo
Katika hali ya masikitiko familia imesema mdogo wake na Profesa Sarungi anayeitwa Emmanuel Sarungi pia amefariki dunia hii leo Alhamisi ya Machi 6, 2025 nyumbani kwake jijini Mwanza.
Kwa mujibu wa Sabasaba, Mzee Emmanuel mwenye umri wa miaka 80 amefariki baada ya kupata taarifa ya kifo cha kaka yake, Profesa Sarungi.
“Akitoka kuzaliwa Profesa Sarungi anafuatia yeye Emmanuel tunadhani baada ya kupata taarifa ya kifo cha kaka yake basi tatizo hilohilo la moyo likamkumba na tunaweza kusema ni tatizo tunalo kwenye familia,” amesema.
Waombolezaji mbalimbali wanaendelea kufika nyumbani hapo kutoa pole. Jirani wa marehemu, Samwel Agunda amesema Mzee Sarungi alikuwa ni mtu mwema na ameishi naye vizuri bila tatizo lolote.
"Alikuwa mpole kwa kweli. Kwenye familia hii muda wote nilikuwa naingia napewa chai sijaona ubaya wowote. Namchukulia kama baba yangu," amesema Agunda.
Historia ya Profesa Sarungi
Mzee Sarungi ambaye alikuwa Waziri wa zamani na mbunge wa Rorya, ambaye kitaaluma ni daktari bingwa wa mifupa aliwahi kushika nafasi mbalimbali za uongozi serikalini, baadaye aliingia kwenye siasa na kuwa mbunge wa jimbo la Rorya mkoani Mara.
Safari yake ya kisiasa, Profesa Sarungi amewahi kuwa Waziri wa Elimu, Waziri wa Afya, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Waziri wa Mawasiliano na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro.
Profesa Sarungi alikuwa mwalimu, daktari wa upasuaji na mtaalamu wa mifupa, waziri, mbunge na mwanamichezo.
Akizungumza Sabasaba amesema familia inamkumbuka marehemu kwa upendo wake mkubwa kwa familia na kwa kuwatumikia Watanzania.
“Ametusomesha na hadi leo hii tumekuwa wakubwa tunajitegemea yote tumepitia kwake na alikuwa mzalendo kwelikweli,” amesema Sabasaba.
Profesa Sarungi alizaliwa Machi 23, 1936 huko Tarime, mkoani Mara, wazazi wake ni Sarungi Igogo Yusufu na Amimo (Maria) Sarungi.
Mwaka 1966, Sarungi alipata shahada ya udaktari wa Tiba kutoka Chuo Kikuu cha Tiba, Szeged, Hungary.
Mwaka 1970, alihitimu shahada uzamivu ya upasuaji kutoka Chuo Kikuu cha Tiba, Szeged, Hungary. Sarungi alihitimu Diploma katika Orthopedics/trauma kutoka Chuo Kikuu cha Tiba, Vienna, mwaka 1973.
Pia, mwaka 1975 alihitimu Diploma katika upasuaji wa upandikizaji viungo kutoka Chuo Kikuu cha Shanghai.
Kuanzia mwaka 1971 hadi 1973, Sarungi alifanya kazi kama Mhadhiri wa upasuaji katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Aliwahi kushika nafasi ya Mhadhiri Mkuu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, mwaka 1973-1976.
Pia, Sarungi alifanya kazi kama Profesa Mshiriki katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, mwaka 1977-1979 na kuwa Profesa mwaka 1979, mkuu wa idara mwaka 1977-1984 katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Kuanzia mwaka 1984-1990, Sarungi alifanya kazi kama Mkurugenzi Mkuu katika Kituo cha Tiba cha Muhimbili na katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Alikuwa pia Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu, mwaka 1989-1991.
Pia, kuanzia mwaka 1990-1992, Sarungi alifanya kazi kama Waziri wa Afya, Waziri wa Mawasiliano na Usafirishaji mwaka 1992-1993 na tangu mwaka 1993 amekuwa Waziri wa Elimu na Utamaduni na pia Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.
Pia, Sarungi mwanachama wa CCM tangu mwaka 1971. Pia, ni Mjumbe wa Chama cha Madaktari Tanzania na Chama cha Madaktari wa Upasuaji wa Afrika Mashariki.