Sungusia, Heche wawapa somo mawakili vijana

Muktasari:
- Wanafunzi wa sheria kutoka vyuo vikuu mbalimbali nchini wameshiriki shindano ya uendeshaji kesi mahakamani, huku viongozi wa vyao vya taaluma hiyo wakiwapa somo kukabili changamoto za matumizi ya tekonolojia.
Dar es Salaam. Mawakili nchini watakiwa kutafuta maarifa mapya yatakayo wawezesha kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya teknolojia.
Hayo yamesemwa kwa nyakati tofauti na Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Harold Sungusia, pamoja na Mwenyekiti wa Chama cha Mawakili Vijana (TYL), Edward Heche wakati wa ufunguzi wa fainali za shindano la uendeshaji kesi (mahakama ya mfano – Moot Court).
Shindano hilo ambalo imefanyika leo Jumamosi, Oktoba 14, 2023, katika ukumbi wa jengo la TLS (Wakili House) jijini Dar es Salaam, liliandaliwa na Victors Hub Limited (VICON), kwa kushirikiana na Victory Attoneys & Consultant, likiwa na lengo la kuwajengea uwezo na kuwapa uzoefu wa uendeshaji kesi wanafunzi hao wa sheria.
Katika tukio hilo, pia kuliwasilishwa mada zilizohusu teknolojia katika masuala ya kifedha na uchumi wa kidigitali (Fintech and digital economy), ambapo wanafunzi wa sheria 20, kutoka vyuo vikuu mbalimbali nchini, walishiriki.
Katika hotuba yake wakati wa ufunguzi wa shindano hilo, Wakili Heche amesema kuwa kwa sasa wanashuhudia mabadiliko ya haraka katika ulimwengu wa teknolojia ya kifedha na kwamba hivyo suala la udhibiti ni muhimu sana kwa Wanasheria na Wanafunzi wa sheria.
“Tunapochunguza masuala haya, nawaasa kuwa na ujasiri wa kufuata maarifa na ujuzi mpya, kwani ndivyo tutakavyoweza kuelewa na kushughulikia changamoto za kisheria zinazoendana na maendeleo haya, ili kuleta mabadiliko chanya katika jamii yetu,” amesema Heche.
Amesema kuwa shindano hilo ni fursa nzuri ya kuonyesha ujuzi wao wa kisheria na jinsi wanavyoweza kutumia sheria kama chombo cha kutatua changamoto za kisasa na kwamba kila changamoto ni fursa mpya ya kujifunza na kukua.
Wakili Heche amesema kuwa ushindi sio tu kuhusu kupata tuzo bali ni juu ya safari yenyewe na ukuaji wanaoupata kupitia njia hiyo.
“Hivyo basi, nawasihi muwe wabunifu, weledi, na wabebaji wa maadili wakati wote wa mashindano haya. Fanyeni kazi kwa bidii. Kumbukeni, kila hatua mnayochukua leo inachangia kujenga mustakabali wenu.
Kwa upande wake Sungusia amewataka Wanasheria kutojifungia katika wigo wa tasnia hiyo pekee bali watazame fursa nyingine zinazotokana na maendeleo na mabadiliko ya kiteknolojia pamoja na kukabiliana na changamoto zake.
Amesema kuwa Mwanasheria hawezi kuwa mjuvi wa sheria mbalimbali bila kujipanua zaidi nje ya eneo lake na kwamba teknolojia inawalekeza hivyo kwa kuwa inazidi kupanuka na kuja na changamoto nyingi.
Amesema mambo mengine ya kisasa yanayotokea katika utaratibu huo wa kiteknolojia ambayo yanaweza kusaidia sekta na tasnia yao ya sheria.
“Wengi tumekua tukijifungia ndani tunashindwa kuangalia fursa kubwa ambazo zinajitokeza baada ya teknolojia kukua. Kuna mambo mengi yanatokea sasa ambayo tunapaswa kuyazingatia yakiwemo matumizi ya akili bandia. Hivyo hata sisi Wanasheria tunapaswa kutumia fursa zinazopatikana katika maendeleo ya kiteknolojia,” amesema Sungusia.
Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Victors Hub, Wakili Rayson Luke, amesema kuwa lengo la shindano hilo ni kuwajengea vijana uwezo wa namna ya kuendesha mashauri mahakamani na kuwawezesha kuona fursa nyingine.
“Unajua kule vyuoni wanasoma sheria za kawaida tu kama vile jinai, madai, mikataba na nyinginezo lakini sasa inapokuja vitu kama hivi fintech (mifumo ya kiteknolojia ya kifedha), uchumi wa kidigitali na akili bandia wanaona kuna maeneo mapya ambayo wanaweza kuyafanyia kazi,” amesema Luke na kuongeza:
“Hii inawafanya wajue kwamba dunia inabadilika, sheria pia zinabadilika na kuna maeneo mapya ya sheria ambayo yana upungufu wa wataalamu na baada ya kumaliza vyuo wanaweza wakajikita kwenye maeneo hayo.”
Luke amesema kuwa washindi katika shindano hilo watapewa zawadi mbalimbali kama tuzo, zawadi, ufadhili wa masomo ya katika Shule ya Sheria kwa Vitendo (Law School of Tanzania – LST), nafasi ya kufanya mazoezi katika kampuni za kisheria hasa baada ya kumaliza vyuo.
Ametoa wito kwa vyuo vikuu nchini kuwa na mfumo wa mahakama hizo za mfano kama ilivyo katika nchini nyingine kwa kuwa sheria ni vitendo badala ya nadharia pekee.