Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Lugha chafu serikalini zamchefua Rais Samia

Rais Samia Suluhu Hassan akipokea Mwenge wa Uhuru kutoka kwa kiongozi wa Mbio hizo, Abdallah Shaibu Kaimu wakati wa Maadhimisho ya Kilele cha mbio hizo katika uwanja wa Tanzanite Kwaraa, Babati mkoani Manyara leo Oktoba 14, 2023.

Muktasari:

  • Matumizi ya lugha chafu, kuchelewesha huduma imetajwa ni changamoto kwa watumishi wa umma ambapo Rais Samia ametoa maagizo kwa wakuu wa mikoa kulifanyia kazi.

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan, amesisitiza nidhamu na uadilifu kwa watumishi umma wanapotoa huduma, akisema eneo hilo bado lina changamoto inayosababisha malalamiko kwa wananchi wanaohudumiwa.

 Rais Samia amesema kumekuwa na malalamiko matumizi ya lugha chafu, kuchelewesha huduma au kudaiwa rushwa kwa watumishi wa Serikali.

Mkuu huyo wa nchi, ameyasema leo Jumamosi Oktoba 14, 2023; katika kilele cha maadhimisho ya mbio Mwenge wa Uhuru yaliyofanyika uwanja wa Tanzanite Kwaraa mjini Babati mkoani Manyara.

Maadhimisho ya yalikwenda sambamba na kumbukizi ya kifo cha Hayati Julius Nyerere kilichotokea Oktoba 14 mwaka 1999 pamoja kilele cha siku ya vijana kitaifa.

Maadhimisho hayo yalihudhuriwa pia na Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango, Naibu Waziri Mkuu, Dk Doto Biteko, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla na viongozi wengine waandamizi wa Serikali, wakiwemo mawaziri.

Mbio za Mwenge za mwaka huu, zilizozinduliwa Aprili Mosi mkoani Mtwara zilibeba kauli mbiu ya ‘Tunza mazingira, okoa vyanzo vya maji kwa ustawi wa viumbe hai na uchumi wa Taifa’, ukilenga kuhamasisha utunzaji wa mazingira na vyanzo vya maji.

“Kumekuwa na malalamiko ya wananchi kuhusu matumizi ya lugha chafu, kuchelewesha huduma au kudaiwa rushwa na watumishi wa Serikali. Hili nataka wakuu wa mikoa na wilaya kulibeba ipasavyo, maana huko chini ndiko kwenye shida,” amesema Rais Samia.

Rais Samia amewataka Watanzania kutekeleza maelekezo ya watalaamu kuhusu lishe, akisema licha jitihada kubwa za kukabiliana na changamoto hiyo bado hali hairidhishi huku akiwasisitizia wakuu wa mikoa kuendelea na utekelezaji wa mikataba ya lishe walioisaini.

Kwa mujibu wa Rais Samia takwimu za udumavu zinaonyesha kwamba asilimia 28 ya wanawake waliopo katika hatua ya kujifungua wana upungufu wa damu huku asilimia 32 wana uzito uliozidi.

Amesema tatizo la udumavu kwa watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano ni asilimia 30 na uzito pungufu ni asilimia 12, ukondefu asilimia tatu na uzito uliopitiliza asilimia nne, kazi imefanyika lakini bado jitihada zinahitajika.

“Kiwango cha udumavu cha asilimia 30 ni kiashiria cha hali mbaya ya lishe kwa mujibu wa viwango vya WHO (Shirika la Afya Duniani). Mikoa inayoongoza kwa kuwa kiwango kikubwa cha udumavu na udumavu zaidi ya wastani wa kataifa ni Iringa asilimia 56.9.

“Ikifuatiwa na Njombe (50.4), Rukwa (49.8), Geita (38.6) Ruvuma (35.6), Kagera (34.3), Simiyu (33.2), Tabora (33.1), Katavi (32.2), Manyara (32), Songwe (31.9) na Mbeya (31.5),” amesema Rais Samia.


Amani na mshikamano

Katika maadhimisho hayo, Rais Samia pia amehimiza Watanzania kulinda, kudumisha kuimarisha amani umoja na mshikamano, kwa kufanya kazi kwa bidii kila mmoja kwa nafasi yake ili kuchangia katika ujenzi wa Taifa kueleekea katika kujitegemea.

“Leo tunapohitimisha kilele cha Mwenge wa Uhuru kitaifa, hatuna budi kujitafakari kama Taifa namna tunavyotekeleza kwa vitendo msingi wa falsafa ya Mwenge kwa kujiuliza maswali yafuatayo.

“Swali la kwanza je tumeendelea kulinda amani, umoja na mshikamano wa kitaifa, je tunadumisha uzalendo, uadilifu na nidhamu. Mwisho tujiulize kila mmoja kwa nafasi yake tunafanya kazi kwa bidi ili kushiriki kikamilifu katika kujenga Taifa.”

Rais amesema maswali hayo ni ya msingi na hakuna budi kuendelea kujiuliza endapo Taifa linataka kujengwa imara na kujitegemea. Alisema ndio maana maadhimisho hayo kila mwaka yanafanyika yakiambatana na kumbukizi ya Hayati Nyerere ambaye ni mwasisi wa Taifa hili.

Rais Samia amesema ili Uhuru uwe na maana hakuna budi kudumisha umoja na kuwajibika na kufanya kazi kwa bidi ili kujitegemea. Amesema vijana ndio nguvu kazi ya katika Taifa lolote linalojitegemea.

Akizungumzia kauli mbiu ya Mwenge wa Uhuru kwa mwaka huu, Rais Samia amesema ni ujumbe mwafaka kwa nchi na dunia kwa ujumla hasa kutokana na changamoto iliyopo ya mabadiliko ya tabia nchi yanayotokana shughuli za kibinadamu zinazoharibu ikolojia, bionuwai na kuleta athari za mafuriko na kutotabirika kwa mvua, ukame, kuongezeka kwa viwango vya joto.

 “Sisi sote ni mashahidi wa baadhi ya matokeo ya athari hizi, kuna nchi kutokana na athari hizi zimekumbwa na baa la njaa, hivyo kwa upande wetu hatuna budi kumshukuru Mungu kwa kutunusuru, tunaendelea kumuomba Mungu atuhifadhi na athari za mabadiliko ya tabia

“Tuchukue hatua za kuhifadhi mazingira yetu na kutunza vyanzo vya maji na kupanda miti.Kwa mujibu wa mkakati wetu kila wilaya ipande miti milioni moja kila mwaka, idadi hii ingesaidia kuziba pengo la miti milioni mbili inayopotea kila mwaka katika hekta 400,000 zinazovunwa,” amesema.

Kutokana na hilo, Rais Samia ameagiza kurejeshwa kwa tuzo ya upandaji miti kwa wale waliopanda na ikastawi ili kwa mikoa kutekeleza wajibu huo kwa kupanda miti kwa wingi.

Katika hotuba yake, Rais Samia amewakumbushia Watanzania umuhimu wa kuchukua tahadhari dhidi ya uwezekano wa kunyesha mvua za Elnino, kama ambavyo Mamlaka ya Utabiri wa Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ilivyotabiri hivi karibuni.

Amesema licha ya matangazo ya mara kwa mara kutolewa, lakini katika miji hakuna tahadhari inayochukuliwa dhidi ya mvua hizo ikiwemo wahusika kusafisha mitaro iliyojaa maji ili kuzuia madhara yatokanayo na mvua hizo. Aliwataka viongozi wa majiji kuchukua hatua hizo.


Mapambano ya ukimwi

Pia amewataka wananchi kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa ukimwi, akisema kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2021 wastani wa Watanzania 54000 wanapata maambukizi mapya ya virusi ya ukimwi kwa mwaka huku Idadi ya vifo vinavyotokana ugonjwa huo ni 29000 kwa mwaka.

“Hii sio idadi ndogo, naomba kila mmoja awe mlinzi yeye mwenyewe na janga hili. Kwa wastani maambukizi ya watu wenye umri wa miaka15 hadi 49 ni asilimia 5. Hata hivyo, tumejitahidi kukabiliana na ugonjwa huu, ukilinganisha tulikotoka,” amesema.


Waziri Ndalkichako

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Profesa Joyce Ndalichako amesema wakimbiza Mwenge wakiongozwa na Abdallah Shaibu Kaimu wametembea kilomita 27,437.82 katika mikoa 31 halmashauri 195 ndani ya siku 196.

Amesema miongoni mwa mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na ukaguzi na ufuatiliaji wa miradi 1,424 yenye thamani ya Sh 5.3 trilioni iliyozinduliwa na kuwekewa jiwe la msingi.

“Miradi hii iliyopitiwa na Mwenge ni sehemu tu ya miradi mingi na mikubwa iliyotekelezwa na Serikali.Miradi iliyokaguliwa ilihusu sekta za afya, elimu, maji na barabara na uwezeshaji wananchi kiuchumi.

“Miradi saba yenye thamani ya Sh 1.8 bilioni ilikataliwa na nyaraka zake zimekabidhiwa kwa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), kwa hatua zaidi,” amesema Profesa Ndalichako.

Akizungumzia suala hilo, Rais Samia kukutwa miradi saba yenye dosari katika 1,424 ni maendeleo makubwa huku akiwaonya watumishi wanaodhani kutumikia wananchi ni kazi ya kawaida na kuwataka kujirekebisha.

“Sasa mwakani nataka mamlaka zinazohusika ziwasilishe taarifa (kuhusu miradi yenye changamoto) ya hatua zilizochukuliwa kwa Waziri Mkuu na kwangu kabla ya kilele cha Mwenge hakijaadhimishwa. Mwaka 2024 Mwenge utawashwa iliamanjaro na kuzimwa Mwanza,” amesema.

Kiongozi wa mbio za Mwenge, Kaimu amesema kwa siku 196 kuanzia Aprili Mosi hadi jana walioupokea ujumbe wa Mwenge kitaifa kama ilivyokusudiwa kwa ushirikiano walifanikiwa walipanda miti, kusafisha mazingira kutunza vyanzo vya maji kwa ustawi wa viumbe hai.

“Pamoja na kazi nzuri ya upandaji wa miti na utunzaji wa mazingira iliyofanywa na Mwenge kwa ushirikiano na wananchi pamoja halmashauri bado uharibifu wa mazingira nchi ni mkubwa,” amesema.