Suluhu ya kudumu ya wakimbizi yatafutwa Ulyankulu

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Innocent Bashungwa akijibu maswali ya wabunge leo Mei 2,2025 bungeni jijini Dodoma. Picha na Hamis Mniha
Muktasari:
- Serikali imesema inaendelea na jitihada za kutafuta suluhisho la kudumu kuhusu hadhi ya uraia kwa baadhi ya wananchi wa Jimbo la Ulyankulu, ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakiishi katika hali ya sintofahamu ya kisheria.
Dodoma. Mbunge wa Ulyankulu, Rehema Migila, ameitaka Serikali kueleza ni lini wananchi wa Kata za Milambo, Kanindo na Igombemkulu wataanza kutambuliwa chini ya Sheria Na. 7 ya Tawala za Mikoa (Tamisemi), badala ya Sheria Na. 9 ya Wakimbizi.
Katika swali la nyongeza bungeni leo, Ijumaa Mei 2, 2025, mbunge huyo amesema kuwa maisha ya wananchi wa kata hizo yamekuwa katika hali ya sintofahamu, hasa wanapohitaji huduma muhimu kutoka kwa taasisi za umma.
Akijibu swali hilo, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Innocent Bashungwa, amesema maeneo hayo yana makundi matatu ya wakazi wenye hadhi tofauti wazawa, raia tajnisi na wakimbizi kutoka nchini Burundi.
"Ikumbukwe kuwa eneo la Ulyankulu lilitengwa na kuanzishwa mahsusi kwa ajili ya kuhifadhi wakimbizi, na kwa sasa sehemu kubwa ya wakazi wake ni raia tajnisi waliotokana na kundi la wakimbizi kutoka nchini Burundi," amesema Waziri Bashungwa.
Ameeleza kuwa watu hao waliingia Tanzania mwaka 1972 na baadaye walipatiwa uraia wa Tanzania kama sehemu ya suluhisho la kudumu la kuwapatia makazi na hadhi ya kisheria.
Bashungwa amesema Serikali inaendelea na mchakato wa kutafuta suluhisho la kudumu kwa wakazi wa eneo hilo, ikiwemo kubaini hatima ya wakimbizi waliobaki na mustakabali wa eneo la Ulyankulu kwa ujumla.
Bashungwa amewaomba wakazi wa eneo hilo kuendelea kuwa na subira na uvumilivu, wakati Serikali ikiendelea kukamilisha mchakato wa kuwatafutia suluhisho la kudumu wakimbizi waliobaki, pamoja na kuamua hatima ya kudumu ya eneo la Ulyankulu.