Spika ‘aapa’ kutowakingia kifua wabunge wenye madeni

Muktasari:
- Wakati Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) wakidai madeni yake, Spika wa Bunge Tulia Ackson amesema wabunge wengi wanadaiwa na kuwataka walipe kodi za nyumba.
Dar es Salaam. Spika wa Bunge Tulia Ackson amewaonya wabunge wanaodaiwa na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), kutomfuata wakati wanaopotakiwa kuondolewa kwenye nyumba za wakala huyo.
Spika ameyasema hayo leo Alhamis, Mei 4, 2023 wakati wa kipindi cha maswali na majibu baada ya Mbunge wa Viti Maalum, Asha Abdullah Juma (Mshua) kuuliza swali la nyongeza.
Katika swali lake, Asha amesema nyumba kadhaa zilizochini ya TBA zikiwemo za Dodoma ni chakavu na kwamba miundombinu ya majitaka imechoka na hivyo kufanya maji ya karo na vyoo kufurika ovyo na kuwa tishio kwa afya.
“Ni nini mkakati wa Serikali kuhakikisha inawasimamia TBA kuhakisha nyumba hizi zinakuwa katika usalama na hasa kwasababu wapangaji wake wanalipa kodi na hawakai bure,”amesema.
Hata hivyo, kabla ya kumruhusu Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Atupile Mwakibete kujibu swali hilo, Dk Tulia amesema wabunge wengi wanadaiwa kodi na TBA na kuwataka kulipa ili waweze kutimiza majukumu yao.
“Wabunge wengi mnadaiwa kodi TBA. Wabunge mnaodaiwa kodi na TBA muilipe ili kusudi iweze kufanya majukumu yake. Nasema hivyo kwasababu nina barua zenu itakapofika muda wa kufukuzwa msinifuate mimi, nendeni ili TBA ifanye kazi zake,”amesema Dk Tulia.
Akijibu swali hilo, Mwakibete amekiri kuwa baadhi ya nyumba ni chakavu na kwamba TBA inategemea fedha za ruzuku ya Serikali na kodi za nyumba katika kutekeleza majukumu yake.
Amesema zinapokusanywa na ndipo wanakarabati nyumba hizo na kuwataka watumishi wanaodaiwa kulipa.