Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Songwe wapuliza dawa magari, treni kudhibiti magonjwa

Muktasari:

  • Mkoa wa Songwe, umeanza kupuliza dawa za kuzuia magonjwa ya mlipuko katika vyombo vya usafiri yakiwemo mabasi ya abiria na treni.

Songwe. Kutokana na ripoti za nchi ya Zambia kukumbwa na ugonjwa wa kipindupindu na kusababisha vifo, Mkoa wa Songwe umeamua kupuliza dawa ya kuzuia magonjwa ya mlipuko kwenye vyombo vya usafiri huku ikiwatahadharisha wanaokwenda Dar es Salaam kujihadhari na ugonjwa wa macho (Red eyes).

Upulizaji huo umeanza Januari 17, 2024 kwa kushirikisha Wizara ya Afya kwa kuingia katika vyombo vyote vya usafiri na kupulizia dawa na mpango huo utasitishwa hali itakapokuwa salama.

Akizungumza na Mwananchi Digital, leo Alhamisi Januari 18, 2024 Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Dk Francis Michael amesema pia wanahakikisha watu wanatumia vyoo na kunawa mikono yao kila wakati.

"Tunashirikiana na Wizara ya Afya kutoa elimu na kupuliza dawa zinazozuia maambukizi katika maeneo yote ya mkusanyiko wa watu katika vyombo vya usafiri ikiwepo kwenye treni," amesema.

Amesema wanapofika kwenye vyombo vya usafiri huwataka abiria wote kushuka kwa ajili ya kupuliza dawa katika mabehewa na baada ya muda huwaruhusu waendelee na huku wakiwapa elimu kuhusu ugonjwa wa macho ulioripotiwa kuwepo jijini Dar es Salaam.

"Tunapuliza dawa hii ina maana kama mtu atakuwa amekanyaga au kushika mdudu wa kipindupindu akifika Tunduma asiweze kuambukiza watu wengine,"amesema.

Baadhi ya abiria wamepongeza hatua hiyo wakisema inawapa tahadhari ya magonjwa ya mlipuko.

Emmanuel Hantumbu, raia wa Zambia na mfanyabiashara amepongezaa hatua hiyo akisema inalenga kulinda wananchi.

"Sisi na Tanzania ni majirani kupata huu ugonjwa wa kipindupindu ni rahisi, kushushwa abiria na kupuliza dawa ni jambo zuri linasaidia kwa wageni kutoleta maambukizi kwa wenyeji," amesema Hantumbu.

Kwa upande wake Jacob Mwakipesile amesema Serikali inatakiwa kuzuia watu kuuza vyakula ovyo ili kuzuia magonjwa ya tumbo kwa wasafiri ambao wanakula njiani bila kujua maandalizi ya vyakula hivyo.

"Ukisafiri tena kwa njia ya treni unajikuta kula ni lazima sasa huruma inakuja kwa wale wenye watoto wananunua vyakula ovyo njiani hawajui mazingira ya vyakula vilivyoandaliwa,"amesema.

Naye Cosmas Njeru dereva wa lori amesema kupulizwa kwa dawa katika magari inawasaidia kujilinda na ugonjwa huo ulioripotiwa nchini Zambia.

"Tunaoishi barabarani inatusaidia naenda nchi karibu tatu naweza jikuta naambukiza nchi zote hizi bila mimi kujua, unaweza kuua au kuwasababishia maradhi watu wasiokuwa na hatia," amesema Njeru.