Serikali yatoa tahadhari ugonjwa wa macho

Muktasari:
- Kufuatia kusambaa kwa kasi kwa ugonjwa wa macho mekundu (Red Eyes) nchini, Serikali imewataka wananchi kuchukua tahadhari na kuzingatia usafi kwani ndiyo njia pekee ya kuepuka maambukizi.
Dar es Salaam. Kufuatia kuwapo kwa ongezeko la wagonjwa wanaofika hospitalini kuhitaji huduma dhidi ya ugonjwa wa macho mekundu, Wizara ya Afya, imewaasa wananchi kuchukua tahadhari.
Ugonjwa huo huenea kupitia maambukizi ya kirusi kwenye ngozi ya juu ya gololi ya jicho yajulikanayo kitaalamu “Viral Keratoconjunctivitis.”
Angalizo hili pia linatolewa na Serikali ikiwa tayari kuna malalamiko kutoka kwa baadhi ya Watanzania kupitia mitandao ya kijamii juu ya kusumbuliwa na ugonjwa wa macho.
Hayo yamesemwa leo Jumatatu Januari 15, 2023 na Mkurugenzi wa Huduma za Tiba Wizara ya Afya, Profesa Pascal Ruggajo kwa niaba ya Mganga Mkuu wa Serikali, Profesa Tumaini Nagu wakati akitoa taarifa ya uchunguzi wa awali ya ugonjwa huo ambao umeripotiwa kuathiri watu wengi nchini.
Profesa Ruggajo amesema taarifa za uchunguzi zinaonesha maambukizi ya kirusi hicho kwenye ngozi ya juu ya gololi ya jicho yajulikanayo kitaalamu ni maambukizi yanayosambaa kwa kasi kubwa.
Profesa Ruggajo amesema mwenendo wa ugonjwa huo unaonyesha kuna ongezeko kubwa la wagonjwa wanaofika katika vituo vya kutolea huduma za afya wakiwa wanasumbuliwa na ugonjwa huo.
“Katika kipindi cha Desemba 22, 2023 hadi Januari 11, 2024 kumeshuhudiwa ongezeko la wagonjwa hawa. Mfano mkoa wa Dar es Salaam pekee kuna wagonjwa wapya 869 huku hali ya kawaida katika kipindi cha mwezi Desemba 2023 kulikuwa na wagonjwa 17 pekee” amesema Profesa Ruggajo.
Miongoni mwa dalili za ugonjwa huo ni macho kuwasha, kuchomachoma, kuuma, macho kutoa machozi na kutoa tongo tongo za njano.
"Hakuna tiba maalumu kwa ugonjwa huu na hata bila tiba dalili huisha zenyewe ndani ya wiki mbili," amesema Profesa Ruggajo.
“Ugonjwa huu huweza kudhibitiwa ikiwa usafi utazingatiwa kutokana na tabia ya ugonjwa huo kusambaa kwa kasi, maambukizi hayo huleta mlipuko ambao husambaa kupitia kirusi kwa asilimia zaidi ya 80,” amesema.
Hata hivyo, Profesa Ruggajo amewashauri wananchi kutotumia dawa zisizo rasmi, ambazo hawajaandikwa na daktari.
“Pia wananchi wasitumie dawa za macho anazotumia mgonjwa mwingine ili kuepuka madhara kwa kuwa dawa za macho ni tofauti na ni kwa matumizi tofauti,” amesema.