Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Simulizi za machungu kwa wakazi, mafuriko Rufiji

Dar es Salaam. Ukiwa umepita mwezi mmoja tangu maji yalipoanza kufurika wilayani Rufiji, Mkoa wa Pwani na kufunika makazi na mashamba ya wananchi, hali ya wananchi inazidi kuwa mbaya.

Mafuriko hayo yalianza kujidhihirisha katika vijiji baada ya Bwawa la Mradi wa Umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) kujaa Machi 5, na inaelezwa maji hayo yatapungua ifikapo Mei 25, mwaka huu.

Hata hivyo, Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) limekanusha kusababisha mafuriko hayo, likisema bwawa hilo ndilo limepunguza kasi ya mafuriko.

Licha ya mafuriko hayo kuathiri kata 12 kati ya 13, kata iliyoathirika zaidi ni ya Mohoro yenye vijiji sita, vikiwamo vinne vilivyofunikwa kabisa na maji.

Kutokana na maji hayo, mamia ya wananchi hawana makazi na wanakabiliwa na njaa, kwa kuwa chakula walichokuwanacho kimesombwa na mazao yaliyokuwa shambani nayo yamefunikwa na maji, huku kukiwa na hatari ya kupata magonjwa ya milipuko kwa sababu maji yaliyojaa yamechanganyika na vinyesi kutoka vyooni.

Mwananchi, lililotembelea eneo hilo, hasa katika Kata ya Mohoro limeshuhudia nyumba zikiwa zimezama na baadhi ya wakazi wamekimbilia kwenye shule za msingi za Mohoro na wengine katika Shule ya Msingi Nyampaku.

Kutokana na mafuriko hayo, usafiri umebadilika kutoka kwenye pikipiki zilizokuwa zimezoeleka na unaotegemewa ni wa mitumbwi (boti).

Wahenga walisema kufa kufaana, ndicho unachoweza kusema kwa kile kinachoelezwa na Hanafi Simba, ambaye ni nahodha wa mtumbwi, kuwa huu ni wakati wa neema, kwani alisema abiria wameongezeka.

“Kwa siku navusha watu 80, kwa sababu chombo changu kinachukua abiria 20 na kila mtu analipa Sh200. Ni kusaidiana tu maana wengi wameathirika,” alisema.
Kuhusu waathirika kuhamia shuleni kinabaki kuwa kitendawili, kwani zinafunguliwa kesho na wanafunzi wanatakiwa kuanza masomo, lakini bado wananchi wameonekana wakimiminika kwenye shule hizo.

Mwalimu wa Shule ya Msingi Mohoro, Yusuf Mbawala ni miongoni mwa waliohamia shuleni, akisema hakuwa na suluhisho.

Mwalimu Mbawala alisema hiyo ni mara ya pili kushuhudia mafuriko kama hayo na kwamba walijihifadhi shuleni hapohapo. “Mwaka 2020 mafuriko yalifika hadi hapa shule, lakini angalau maji hayakuwa mengi, tulijihifadhi hapahapa,” alisema.

Naye Bahati Msura alisema alihamia kijiji hicho mwaka 2023 akitoa Mkoa wa Mara, kwa ajili ya kazi za kilimo, lakini ameambulia uharibifu.

Alisema siku mafuriko yalipoanza walijaribu kuondoa mizigo kwenye nyumba waliyokuwa wakiishi, lakini hawakumaliza. “Tulianza kuondoa saa 12 jioni, hadi saa 4 usiku, tukapumzika. Ilipofika saa 9 usiku maji yalikuwa yamefika kifuani, tukashindwa kuondoa vitu.

“Japo tumekuja hapa, hatujui tutakapopata chakula, maana mashamba yote yamezama kwenye maji,” alisema.

Zainab Bakari alisema: “Sisi tunakaa katika bonde la maji la Nyampaku, ilipofika usiku maji yalijaa, tukaondoka na hatukuweza kuokoa chochote na kuna mwanafunzi anasoma darasa la kwanza, sijui atakwendaje shule kwa hali hii.”

Naye Pili Yusuf alisema, “Tumekuja jengo hili la Serikali mimi na familia yangu yote, mashamba yameathirika na maji na kuku tuliokuwa nao wameondoka, kwa hiyo hatuna kitu chochote, tunaishi hapa tupate angalau msaada,” alisema.

Shule hiyo yenye madarasa 14, huenda ikazidi kufurika kutokana na ongezeko la watu waliokuwa wakiendelea kuhamia, huku kila familia ikichukua darasa zima.

“Nimekuja hapa na makochi, vitanda na vyombo vyote kwa kuwa nimefanikiwa kuviokoa. Tutaishi hapa hadi tutakapopata mahali pengine pa kuishi,” alisema Juma Selemani, aliyekuwa akihamishia vifaa vyake darasani.

Katika shule ya Msingi Nyampaku nako maandalizi ya kupokea watu yanaendelea.Mmoja wa walimu aliyekuwepo eneo hilo na ambaye hakutaka kutajwa jina lake, alisema wazazi wameendelea kufika kuomba hifadhi.

“Kwa sasa kuna familia moja, ila kuna wazazi wengine wamekuja kuomba hifadhi na wameshasafisha madarasa,” alisema.

Mbali na wanaoishi shuleni, Mariam Mtulia, ambaye nyumba yake imezama, alisema amehamishia makazi kwa jirani yake. “Maji haya yametujia ghafla ndio tunapata adha hii hivyo tunaomba msaada. “Kwa biashara zangu hizi za chakula, napata taabu kwa sababu ya maji. Nyumba yangu imezama hivyo nimejihifadhi kwa ndugu,” alisema.
Mwantumu Omar, aliyewahifadhi waathiriwa hao, alisema adha imekuwa kubwa.

“Tumewahifadhi watu, hadi vyombo vimekaa darini, hakuna njia ya kupita, wengi wamepoteza nyumba.

“Mimi nimechukua familia tatu zote tunaishi hivyo hivyo hadi hapo mafuriko yatakapoisha,” alisema.

 

Msaada utakuja lini?

Wakati wananchi wakiendelea kuteseka, Mkuu wa Wilaya ya Rufiji, Edward Gowele alisema bado tathmini inaendelea kufanywa bila kubainisha itakamilika lini.
Kauli hiyo inatia shaka kuwepo kwa uharaka wa kuwasaidia wananchi hao.
 

Tanesco wafafanua chanzo cha mafuriko

Akizungumza na Mwananchi jana, Mkurugenzi wa Tanesco Kanda ya Mashariki, Kenneth Boymanda alisema mradi wa Bwawa la Umeme la Julius Nyerere (JNHPP) kuwa chanzo cha mafuriko hayo si kweli, ni mvua zinazoendelea kunyesha kwenye mikoa yote ya Nyanda za Juu Kusini Magharibi zinazoingiza maji kwenye mto Rufiji.