Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Simulizi mwanamke anayefanya kazi mochwari

Precious Landa, mhudumu wa chumba cha kuhifadhia maiti katika kituo cha afya Likombe. Picha na mpigapicha wetu

Dar es Salaam. Uhudumu wa mochwari, licha ya kuwa ni fani ambayo watu huingia darasani kusoma, mtazamo wa jamii bado ni hasi, hivyo wahusika kujikuta wakinyanyapaliwa.

Precious Landa, mhudumu wa mochwari katika kituo cha afya Likombe, kilichopo Halmashauri ya Mtwara-Mikindani ni mwathirika wa unyanyapaa huo.

Katika mahojiano na Mwananchi, anasema amelazimika kufanya kazi ya kuelimisha jamii ili kubadili mitazamo hasi juu ya fani hiyo.

Anasema baadhi ya wanajamii humuona kuwa mtu katili, wengine wakiamini huwa anatumia pombe au dawa za kulevya kutokana na dhana kuwa mochwari ni chumba chenye mauzauza, hivyo mtu mwenye akili timamu hawezi kuhudumu.

“Jamii isichojua ni kwamba, watu wanaingia darasani na kujifunza kazi hii. Wanasoma kama fani nyingine kama vile udaktari, uuguzi au ualimu," anasema Precious.

Anasema aliipenda kazi hiyo tangu akiwa mdogo, baada ya kuingia mochwari na kushuhudia namna mwili unavyoandaliwa.

Precious anasema alimuuliza mmoja wa wahudumu kama ni kweli chumba hicho kina mauzauza au wao wanatumia pombe na bangi.

“Hakunijibu pale, nilifanya utafiti na kubaini ni kitu kinachosomewa. Awali, nilisoma uuguzi usaidizi katika chuo cha St David Comprehesive College kilichopo Iringa, kabla ya kujiendeleza kwa kusoma uhudumu wa mochwari katika Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas) kwa miezi miwili kati ya Aprili na Juni, 2022,” anasema.

Alipomaliza masomo, anasema Agosti mwaka huohuo alipata kazi katika kituo anakofanya kazi hadi sasa, ikiwa ni kitu alichofurahia kwa kuwa anafanya kile anachokipenda.

Akiwa na majokofu sita katika eneo lake la kazi yaliyopewa majina ya majiji makubwa duniani, New York, Paris, Moscow, Tokyo, Dubai na London, anasema anajihisi fahari kuhudumu katika eneo hilo.

Kituo hicho kilipandishwa hadhi kutoka zahanati baada ya kuwekwa vifaa vya zaidi ya Sh361.5 milioni, hivyo kuboresha huduma mbalimbali, zikiwamo za mama na mtoto, upasuaji na usimikaji wa mitambo ya kufanya vipimo kama X-ray.

“Nafurahi kwa sababu ni kama nalipa fadhila kwa waliomhudumia mama yangu alipofariki, sikuwa na uwezo wa kushiriki, lakini kwa sasa naweza kuwasaidia wale wasiokuwa na uwezo kwa namna wanavyohitaji,” anasema Precious.


Siku ya kwanza mochwari

Kila kitu kinapofanyika kwa mara ya kwanza, lazima kunakuwa na changamoto, hata yeye anaeleza alipata woga alipohudumia mwili wa kwanza.

“Ilikuwa ni mama aliyepata ajali, nilitakiwa nimuandae akae vizuri, niliogopa ila nilijipa moyo na kuona kama namhudumia mama yangu,” anasema.

Kuhusu changamoto anazopitia mbali ya kuonekana mtu wa ajabu, anaelezwa namna alivyoachwa na mchumba wake, kwa kile alichoona huenda mwanamke anayetarajia kumuoa ni mtu katili.

“Ilifika wakati ambao natakiwa kuchagua kati yake na masomo, nilichagua kusoma kwa sababu familia inalipa fedha. Pia niligundua natakiwa kuolewa na mtu anayeunga mkono ndoto zangu na si kuniwekea kikwazo,” anasema.


Anavyozungumzwa

Wakizungumzia kazi yake, baadhi ya watu waliokuwa hospitalini hapo walimtaja kama mtu jasiri, anayejua anachofanya bila kujali wanaomzunguka wanasema nini.

“Siku ya kwanza nilishangaa na kumuogopa kiasi, ila ukikaa naye utajua ni mtu mwema, anayesali, anafanya kitu hicho kwa moyo na anakipenda anachokifanya,” alisema Grace Mapunda, mkazi wa Mtwara.

Abdul Tengeneza, anasema mitazamo ya jamii juu ya watu wanaohudumu mochwari ndiyo kitu kinachopaswa kufanyiwa kazi, ili kuhakikisha watu hao wanakuwa huru katika majukumu yao.

“Tuwatafutie uhuru, kama ilivyo kwa walimu, madaktari, jamii ielimishwe, kwa sababu hizi zote ni huduma ambazo watu wanapaswa kupatiwa,” anasema Tengeneza.

Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Likombe, Dk Victor Andrea, alisema Precious ni mtu mwenye nidhamu, anayezingatia maelekezo ya kazi anayopewa.

Anamsifu kwa kumuelezea: ‘‘Kama eneo lake la kazi halina watu wa kuhudumia, yuko tayari kuhudumu katika maeneo mengine pia.’’

“Ni mtu mwepesi kubadilika kulingana na mazingira ya kazi husika, kama kuna eneo linahitaji usaidizi ukumuomba aende atakwenda, yuko tayari kufanya kazi yoyote anayoimudu pia ni mtu anayependa kujifunza,” anasema.