Silaa atoa maagizo manne NHC

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Jerry Silaa (watatu kutoka kulia) akimsikiliza Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Hamad Abdallah (wapili kushoto) alipokuwa katika ziara ya kuangalia maendeleo ya miradi mipya ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) jijini Dar es Salaam. Wapili kulia ni Mkurugenzi wa Ujenzi wa Shirika ilo, Mhandisi Haikamen Mlekio. Picha na Michael Matemanga
Muktasari:
- Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Jerry Silaa ametoa maagizo manne kwa Shirika la Nyuma (NHC) ikiwemo kuhakikisha ifikapo mwezi Oktoba mwaka huu mradi wa 711 uliopo kawe ujenzi wake unaendelezwa.
Dar es Salaam. Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Jerry Silaa ametoa maagizo manne kwa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) ikiwemo kuhakikisha mradi wa 711 uliokwama tangu mwaka 2017 kufikia Oktoba mwaka huu ujenzi wake uendelezwe.
Mradi huo uliosimama kwa muda mrefu sasa kama ungekamilika mwaka 2017 ungegharimu Sh107 bilioni lakini kutokana na ucheleweshaji huo gharama ya ujenzi wake zinatarajiwa kupaa zaidi kutokana na vifaa vya ujenzi kupanda bei.
Akizungumza Dar es Salaam baada ya kufanya ziara ya kutembelea miradi mitatu ikiwemo wa 711, leo Septemba 11, Silaa ameutaka uongozi wa taasisi hiyo kuharakisha mazungumzo yanayofanyika kati yake na mkandarasi katika kuangalia bei ili jitihada za ujenzi zianze.
“Kuna madai ya ucheleweshaji na kuna gharama zilizoongezeka, sasa kufikia mwezi Oktoba jambo lifikie mwisho na tuanze kuona mitambo inazunguka.
“Mradi huu ni lazima ujengwa kwa sababu kunafedha ya mkopo imelala, mkopo unaongezeka na kuna wananchi wengi wanauhitaji wa nyumba na ni eneo nzuri kwa makazi,” amesema.
Ameagiza mradi wa Samia unaojengwa Kawe unakamilika kwa wakati na kuhakikisha unapelekwa mikoa mingine hasa kwenye majiji yenye mahitaji makubwa.
“Natamani kuona Mwanza, Mbeya, Dodoma ni maeneo yenye uhitaji mkubwa wa nyumba na yana watu wengi kutokana na mwingiliano uliopo ili kutengeneza sura mradi huo siyo wa Dar es Salaam pekee,”amesema.
Maagizo mengine shirika hilo kuangalia mpango wa ubia kwa kuendelea miradi yake kwa kuwavutia watu wenye msuli wa kifedha, Mradi wa Morocco Square ukamilike kwa wakati.
Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Hamad Abdallah amesema mradi wa Morocco Square utakamilika mwishoni mwa mwaka huu na ukikamilika taasisi hiyo kila mwezi itakuwa inaingiza Sh850 milioni.
Mradi huo uliogharimu Sh137 bilioni hadi sasa umefikia asilimia 98, sehemu iliyobakia ni maeneo ya ofisi kubwa na maduka makubwa hadi mwezi Desemba mwaka huu kutakuwa tayari kwa matumizi.