Siha, Rombo zashika mkia matumizi ya nishati safi Kilimanjaro
Muktasari:
- Licha ya jitihada za Serikali na taasisi binafsi, wananchi wengi bado hawajapata mwamko wa kutumia nishati safi.
Moshi. Halmashauri za Siha na Rombo mkoani Kilimanjaro zimetajwa kuwa na kiwango cha chini zaidi cha matumizi ya nishati safi ya kupikia katika taasisi za umma na binafsi, kulinganisha na halmashauri nyingine za mkoa huo.
Hali hii inatajwa kuchangia madhara kiafya na uharibifu wa mazingira kutokana na utegemezi wa kuni na mkaa.
Katika Halmashauri ya Rombo, kati ya taasisi 211 ni tatu pekee zinazotumia gesi. Taasisi hizo ni Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Mamtukuna (FDC), Gereza la Rombo na Shule ya Sekondari Kiraeni.
Hali ni kama hiyo katika Halmashauri ya Siha, ambako kati ya taasisi 85 ni nne pekee zinazotumia nishati safi. Taasisi hizo ni Shule ya Sekondari Visitation, Shule ya Sekondari Magnicat, Shule ya Sekondari ya Wasichana Kilimanjaro na Hospitali ya Charlote.
Kwa mujibu wa taarifa ya utekelezaji iliyotolewa na ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, hadi kufikia Mei 2025, kulikuwa na taasisi 25 kati ya 1,316 za umma na binafsi mkoani humo zinazotumia nishati safi ya kupikia, ikiwamo gesi na umeme.
Mbali ya hizo, Halmashauri ya Hai ina taasisi 13 kati ya 267 zinazotumia nishati safi, Moshi Mjini na Moshi Vijijini zina taasisi 23 kati ya 54, Same ina taasisi tatu kati ya 211, huku Mwanga ikiwa na taasisi sita kati ya 127.
Nini kinafanyika
Licha ya changamoto zilizopo, baadhi ya taasisi zimeonesha mfano kwa kuwekeza kwenye gesi na umeme. Mkuu wa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Rombo, Herry Kinyamagoha, anasema wamekuwa wakitumia gesi ya LPG tangu mwaka 2021 kwa wanafunzi 460.
Anasema awali walikuwa wakitumia kuni, hali iliyokuwa ikisababisha changamoto za kiafya kwa wahudumu jikoni na gharama kubwa za usafirishaji wa kuni.
“Mtungi wa gesi unaogharimu Sh3.1 milioni unadumu siku 45, wakati lori la kuni la Sh300,000 lilikuwa likidumu miezi miwili. Ingawa gharama za awali za gesi ni kubwa, tuliona faida kiafya na kimazingira, ndiyo maana tukaamua kuwekeza,” anasema.
Mkuu wa Wilaya ya Siha, Christopher Timbuka, anasema juhudi za kuhamasisha matumizi ya nishati safi zimeanza kuzaa matunda, ikiwamo kugawa mitungi zaidi ya 6,000 kwa wananchi kupitia ruzuku.
“Kwa kushirikiana na kampuni kama Lake Oil, tulinunua mitungi na kuwagawia wananchi ili waone faida ya kutumia gesi badala ya kuni. Pia, tumeshirikiana na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kugawa miche ya miti na kuanzisha vitalu shuleni ili kuimarisha utunzaji wa mazingira sambamba na matumizi ya nishati safi,” anasema.
Timbuka anasema shule za sekondari za Kilimanjaro na Namwai zimeweka mifumo ya kutumia gesi na mpango ni kuzifikia shule nyingine wilayani humo.
Mkuu wa Wilaya ya Rombo, Raymond Mwangwala, anasema Serikali inashirikiana na vyama vya akiba na mikopo (Amcos) kusambaza majiko rafiki yanayotumia umeme mdogo kwa gharama nafuu.
“Serikali imekuwa ikitoa ruzuku na hata kugawa bure majiko rafiki, hasa kwa mama lishe. Tunataka kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa ambao umekuwa ukiharibu misitu na kuathiri afya ya watumiaji,” anasema.
Mwamko wa wananchi
Licha ya jitihada za Serikali na taasisi binafsi, wananchi wengi bado hawajapata mwamko wa kutumia nishati safi.
Esteri Mushi, mkazi wa Kijiji cha Ngareni wilayani Siha, anasema anategemea kuni kwa sababu hana uwezo wa kununua gesi.
“Jiko la gesi na mtungi ni gharama kubwa. Hata mkaa nao bei imepanda, lakini angalau kuni tunazipata msituni. Sasa hivi ni vigumu kwa familia kama yangu kumudu gharama za gesi kila mwezi,” anasema.
James Kimaro, mkazi wa Tarakea, wilayani Rombo, anasema elimu ya nishati safi imekuwa ikitolewa mara kwa mara lakini bado haijawafikia moja kwa moja wananchi vijijini.
“Mitaa ya mjini ndiyo wananufaika na gesi, lakini huku vijijini bado tunategemea kuni na mkaa. Watu wanashindwa kubadilika kwa sababu hakuna mifumo ya usambazaji inayofika vijijini,” anasema.
Mchango wa Veta
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Chuo cha Ufundi Stadi Moshi (Veta), Msajili wa chuo hicho, Mhandisi Frank Kabipe, anasema kina wanafunzi 847, kati yao wasichana 227 na wavulana 620.
Anaeleza kati ya hao, 574 ni wa bweni, huku chuo kikihudumiwa na watumishi 70 wakiwamo walimu 48.
Kabipe anasema chuo kimeanza kutumia kuni rafiki aina ya briquette kama nishati safi na kipo mbioni kuhamia kwenye matumizi ya gesi.
Anasema majiko ya gesi yanayotumika yamebuniwa na kutengenezwa na walimu kwa kushirikiana na wanafunzi wa fani husika chuoni hapo.
Mwalimu wa Uungaji Vyuma chuoni hapo, Buriani Rashid, anasema tangu mwaka jana wameuza takribani majiko 10 kwa taasisi za Serikali.
Anasema gharama za jiko moja la lita 50 ni Sh2.5 milioni, la lita 100 ni Sh2.1 milioni na la lita 200 ni Sh3.3 milioni.
Kwa sasa, Veta Moshi inatumia majiko sita ya kuni rafiki, ikitumia tani tano kwa mwezi zinazogharimu Sh3 milioni, sawa na Sh600,000 kwa tani moja.
Mkakati wa Tanesco
Meneja wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) Mkoa wa Kilimanjaro, Mhandisi Doto Chacha anasema juhudi zinaendelea kuhakikisha wananchi na taasisi wanaacha kuni na mkaa na kuelekea matumizi ya nishati safi.
“Tuna wateja 341,000 sasa, lakini lengo letu ni kufikia wateja 500,000 ifikapo Desemba 2025. Ili kufanikisha hilo, mwaka huu pekee tunalenga kuongeza wateja wapya 89,614. Tukiwafikia, tunaamini tutakuwa tumepiga hatua kubwa ya kuimarisha matumizi ya nishati safi ya umeme kwa wananchi,” anasema.
Anasema Tanesco imekuwa na kampeni ya kupita wilaya zote mkoani humo kuhamasisha matumizi ya nishati safi, akieleza mwitikio wa wananchi ni mkubwa.
“Tumeshuhudia baadhi ya familia zikibadili majiko ya kuni na kutumia ya umeme, jambo linaloonyesha mwamko unaanza kuongezeka,” anasema.
Matarajio ya baadaye
Ili kupiga hatua, wadau wanashauri Serikali kuweka mazingira rafiki kwa wawekezaji na sekta binafsi kushiriki kikamilifu katika usambazaji wa bidhaa na huduma za nishati safi.
Pia, taasisi za kifedha zinahimizwa kuandaa mikopo nafuu kwa wananchi na wafanyabiashara wa bidhaa za nishati safi.
Vilevile, vyuo vya elimu na utafiti vinatarajiwa kushiriki kwa kufanya tafiti na kutengeneza teknolojia mpya zitakazopunguza gharama na kuongeza upatikanaji wa nishati safi kwa wananchi.
Kwa mujibu wa mikakati ya kitaifa, ifikapo mwaka 2034, zaidi ya asilimia 80 ya Watanzania wanatarajiwa kutumia nishati safi ya kupikia.
Hata hivyo, wataalamu wanasema mafanikio hayo yatategemea kasi ya uwekezaji, uhamasishaji na ushirikiano kati ya Serikali, sekta binafsi na wananchi.
Imeandikwa kwa udhamini wa Taasisi ya Gates Foundation
Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765 864 917