Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Shule zilizojengwa kwenye miinuko zakabiliwa na makorongo Dar

Muktasari:

  • Makorongo yanayoongezeka, mmomonyoko wa ardhi na nyufa kwenye majengo sasa ni sehemu ya mazingira ya baadhi ya shule, hali inayoweka rehani usalama wa watoto wanaopata elimu katika maeneo hayo.



Dar es Salaam. Baadhi ya maeneo ya mijini, hasa Dar es Salaam, ujenzi wa shule katika maeneo ya miinuko umeibua hali ya wasiwasi miongoni mwa wazazi, wanafunzi na walimu kutokana na athari zinazoendelea kujitokeza katika kila msimu wa mvua.

Makorongo yanayoongezeka, mmomonyoko wa ardhi na nyufa kwenye majengo sasa ni sehemu ya mazingira ya baadhi ya shule, hali inayoweka rehani usalama wa watoto wanaopata elimu katika maeneo hayo.

Katika kata ya Msigani iliyopo Wilaya ya Ubungo, jijini Dar es Salaam yenye shule tano hali si nzuri , shule zake mbili zinazofuatana zipo kwenye muinuko huku moja ikiwa kando ya mto.

Shule ambazo zipo katika kata hiyo zina wanafunzi wengi kwa mujibu wa takwimu za Best zinazotolewa na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) za mwaka 2025 ni  Bwawani wanafunzi 2,075 walimu 46, Malamba Mawili  wanafunzi 2,510 na walimu 47, Msigani wananfunzi 2,230 na walimu 48.

Shule ya Malamba Mawili imejengwa mwaka 1998/1999, Bwawani imejengwa mwaka 2018 huku Bangulo Mpya ikijengwa mwaka 2022/23.

Makorongo yaliyopo Shule ya Msingi Bwawani iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Ubungo ambayo yametokana na mvua.

Hali hiyo si katika wilaya hiyo hata Wilaya ya Ilala inakabiliwa na jambo hilo kwa kuwepo kwa shule ya Msingi Bangulo yenye wanafunzi 2,687 walimu 53 inakumbana na hali hiyo na nyingine ni Bangulo Mpya iliyopo Hali ya Hewa.  


Kauli za wazazi

Mzazi ambaye mwanaye anasoma Shule ya Msingi Bwawani, Maulid Mohamed anasema kila mvua inaponyesha, maji hutiririka kwa kasi kutoka juu ya mlima na kupita katikati ya viwanja vya shule, yakibeba udongo na kuchimba mashimo makubwa yanayoongezeka kila mwaka.

“Kwa kweli tuna hofu mtoto akicheza karibu na eneo hilo anaweza kudondoka wakati wowote kwa sasa tumekuwa tukibaki na watoto nyumbani kwa kuhofia usalama wao kutokana na mazingira ya shule,”anasema Mohamed.

Wanafunzi wakipita jirani na darasa ambalo kingo moja ya ukuta imeanguka kutokana na mvua katika shule ya Msingi Malamba Mawili iliyopo Wilaya ya Ubungo, jijini Dar es Salaam

Anasema mazingira ya shule kipindi cha mvua na baada ya mvua ni hatari zaidi kwa sasa wanatueleza kuwa, marafiki zao wa shule ya jirani ya Malamba Mawili wanaogopa kucheza jirani na darasa la nne kwa sababu ukuta umeanguka.

Mohamed anasema watoto wamekuwa waoga kupita baadhi ya maeneo kwa sababu ya kuwa na mashimo na wakati mwingine wamejikuta wakizunguka ili kufika shuleni kwao.

Mkazi na jirani na shule hiyo, Alphonce Kiwage anasema maji yanayotoka kwenye eneo la shule kuingia barabara ya mtaa imekuwa ni sehemu ya watoto kucheza na inapotokea mvua kuwa kubwa wanawakataza.

“Hizi shule mbili ni shida na sio shule pekee, jirani kuna hospitali pia mvua ikinyesha ni shida watoto wanajikuta kwenye mazingira magumu, Serikali inahitajika kufanya kitu kwa sasa maana inahatarisha maisha ya watoto,”anasema Kiwage.

Wananfunzi wakifanya usafi kwenye moja ya korongo lililopo katika shule ya msingi Malamba Mawili iliyopo wilaya ya ubungo jijini Dar es Salaam.

Anasema kutokana na hali hiyo, watoto wanakosa eneo la kuchezea kwani itakapotokea mmoja amedondoka, ataumia vibaya na baadhi ya wazazi ambao sio walewa hulalamika walimu hawapo makini.

Wanafunzi nao wanaeleza changamoto wanazokutana nazo katika mazingira ya shule hizo.

“Mara mvua ikinyesha, hatuwezi hata kutoka darasani kwa sababu maji yanakuwa mengi na barabara zinakuwa zenye matope na mashimo,” anasema mwanafunzi mmoja tumehifadhi jina lake.

Anasema njia wanazotumia zinakuwa na tope, hata vyoo vyao wanavyotumia vipo mbali na madarasa, wanatakiwa kupita kwenye makorongo ili kufika huko.

Mbali na huduma hizo hata mazingira ya ulaji wa vyakula kipindi cha mvua imekuwa ni changamoto, eneo lao kubwa linakuwa limetawaliwa na tope la mfinyanzi pamoja na mashimo.

Aidha, kuna hofu ya muda mrefu kuhusu uimara wa majengo yenyewe kutokana na nyufa zinazoanza kujitokeza kwenye kuta na sakafu.

Sehemu ya kipande cha ardhi kilichoondolewa na mvua katika Shule ya Msingi Msigani ambayo ipo jirani na mto.

Katika shule nyingine ya msingi ya Msigani iliyopo pembezoni mwa mto imejikuta kwenye changamoto ya eneo lake kuchimbwa na maji hali inayoendelea kuweka hatari zaidi kwa wanafunzi na walimu.

“Hapa zamani kulikuwa sawa, lakini sasa mvua zinaponyesha tunaona udongo unateremka kidogo kidogo. Tunaogopa siku moja darasa linaweza kuathirika,” anasema mzazi mmoja wa mwanafunzi wa darasa la saba.

Anasema katika eneo hilo mvua zikiendelea kunyesha watu wanaogopa, zikiwa kubwa wazazi wanaendelea kuogopa kwa kuhofia hatari kwa watoto wao.

Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo anasema anamuagiza mhandisi kwa ajili ya kufanya tathimini ya shule za msingi za Banguluo na sekondari ili waweze kujadili hatua za kuchukua.

“Nikiri sina taarifa ya muhimu kwa sasa, namuagiza mhandisi kwa ajili ya kufanya tathimini ya shule hizo maelezo yake yatatupa njia ya kufanya na kinachohitaji kwa kipindi hiki,”anasema Mpogolo.


Tathimini ya mazingira

Ofisa Miradi wa GreenFaith Africa, Baraka Machumu, ameitaka Serikali kuimarisha usimamizi wa tathmini za athari za mazingira ili kuepusha majanga yanayoendelea kuathiri wananchi, hususan watoto.


Akizungumza kuhusu hali hiyo, Machumu anasema kumekuwa na ongezeko la matukio ya watoto kuanguka na kujeruhiwa kutokana na mazingira hatarishi yanayotokana na ujenzi usiozingatia ushauri wa kitaalamu, ikiwamo maeneo yenye utelezi na maporomoko ya udongo.

“Miradi mingi ya maendeleo inatekelezwa bila kuzingatia kikamilifu tathmini za mazingira. Matokeo yake tunaona athari kama utelezi, maporomoko na hata uharibifu wa mifumo ya asili ambayo ingeweza kuzuia majanga haya,” anasema Machumu.

Anasema moja ya changamoto kubwa ni ukataji wa miti wakati wa ujenzi wa miundombinu kama barabara bila juhudi za kurejesha uoto wa asili baada ya ujenzi kukamilika.

Katika sekta ya elimu, Machumu anasema hali hiyo pia imejitokeza, miradi ya ujenzi wa madarasa imekuwa ikiharibu juhudi za awali za uhifadhi wa mazingira, ikiwamo upandaji miti mashuleni.

“Tumewahi kufanya miradi ya upandaji miti mashuleni, lakini baadaye madarasa yanajengwa katika maeneo hayo hayo, hii inaonesha ukosefu wa mipango endelevu na uratibu,” anasema.

Anasema ni muhimu kwa Serikali kuhakikisha tathmini za athari za mazingira zinafanyika kabla ya kuanza kwa mradi wowote, iwe mkubwa au mdogo, na kwamba mapendekezo yake yazingatiwe kikamilifu.

Baadhi ya viroba vyenye mchanga vikiwa vimepangwa ili kuzuia mmomonyoko wa ardhi katika shule ya Msingi Msigani ambayo ipo jirani ma mto

Hata hivyo, anahoji utekelezaji wa tathmini hizo, akisisitiza kuwa baadhi yake huonekana kufanyika kwa ajili ya kukidhi taratibu tu bila kufuatwa ipasavyo.

“Ni muhimu kujiuliza kama hizi tathmini zinafanyiwa kazi au zinabaki kwenye makaratasi, Serikali inapaswa kuongeza ufuatiliaji na kuwawajibisha wale wote wanaokiuka,” anasema.


Utafiti wa wadau wa elimu

Utafiti uliofanywa unaonesha katika baadhi ya maeneo, shule zinajengwa bila kuzingatia mahitaji halisi ya wanafunzi wala miongozi ya kitaalamu ya upangaji wa miundombinu ya elimu.

Hali hii imeelezwa kuchangiwa kwa kiasi kikubwa na utaratibu wa sasa, maeneo ya kujenga shule hutolewa na vijiji au mamlaka za mitaa bila tathmini ya kina ya kitaalamu.

Mtafiti binafsi wa masuala ya elimu Dk Muhanyi Nkoronko anasema mara nyingi maeneo yanayotengwa kwa ajili ya shule hayakidhi vigezo vinavyotakiwa, hali inayosababisha upangaji mbovu wa madarasa na miundombinu mingine muhimu.

“Unakuta eneo limetolewa lakini haliruhusu upangaji mzuri wa madarasa, maeneo ya michezo, au hata huduma za msingi. Hii inaathiri moja kwa moja ujifunzaji wa mtoto,” alieleza.

Mbali na hilo, anasema ufuatiliaji wa miongozo ya ujenzi kunasababisha baadhi ya shule kujengwa katika mazingira hatarishi. Mfano uliotolewa ni shule ambazo zinakatizwa na barabara katikati, hali inayohatarisha usalama wa wanafunzi na kuvuruga utulivu wa masomo.

“Fikiria mtoto anasoma huku magari yanapita katikati ya shule, kelele na hatari ya ajali vinakuwa sehemu ya maisha ya kila siku ya mwanafunzi. Hii siyo mazingira rafiki kwa ujifunzaji,” anasema.

Mtaalamu huyo anasema ili kuboresha hali hiyo kuna haja ya kuweka utaratibu madhubuti wa kuhakikisha kabla ya shule kujengwa, inapata idhini rasmi inayozingatia tathmini ya mazingira pamoja na vigezo vya upangaji bora.

Anashauri pia kuwepo kwa mwongozo (checklist) maalumu utakaotumika kuthibitisha ubora wa eneo kabla ya ujenzi kuanza, ikiwa ni pamoja na kuangalia usalama wa eneo, upatikanaji wa huduma muhimu, na urahisi wa kufikika kwa wanafunzi na walimu.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa ushirikishwaji wa mamlaka zinazohusika na mazingira katika mchakato wa kupanga na kujenga shule, ili kuhakikisha kuwa majengo yote yanazingatia viwango vinavyotakiwa.

“Serikali kwa kushirikiana na wadau wa elimu inapaswa kuhakikisha hakuna ujenzi holela wa shule. Lazima kuwe na idhini ya mazingira kabla ya kuanza ujenzi wowote,” alisisitiza.


Hatari ya kimuundo

Mhandisi wa ujenzi, Hamis Mshana anasema kuongezeka kwa makorongo katika maeneo ya shule ni ishara ya moja kwa moja ya udhaifu katika upangaji na utekelezaji wa miundombinu ya kudhibiti maji.

Viroba vikiwa vimewekwa pembezoni mwa darasa ili kuzuia mmomonyoko wa udongo utakaoathiri msingi.

“Unapoona makorongo yanaanza kujitokeza ndani au pembezoni mwa shule, ujue maji hayakudhibitiwa ipasavyo tangu mwanzo. Haya maji yanapopita kwa kasi, yanaondoa udongo hatua kwa hatua na kuacha mashimo makubwa yanayoendelea kupanuka kila mvua inaponyesha,” anasema Mshana.

Anasema hali hiyo ndiyo inayosababisha baadhi ya madarasa kuanza kupata nyufa au hata msingi kudhoofika.

“Makorongo haya yanapokaribia majengo, huanza kuathiri msingi wa darasa, udongo unaoshikilia jengo unapungua na matokeo yake unaona nyufa kwenye kuta, sakafu kupasuka, au hata jengo kuanza kuinama kidogo.”

Kwa mujibu wa mhandisi huyo, kama hatua za haraka hazitachukuliwa, baadhi ya madarasa yako kwenye hatari ya kuendelea kuharibika au kutokuwa salama kabisa kwa matumizi.

“Ni muhimu sana kuchukua hatua mapema kwa kujenga mifereji ya maji, kurekebisha maeneo yaliyochimbika na kuimarisha msingi wa majengo yaliyoathirika. Vinginevyo, uharibifu utaongezeka na gharama ya marekebisho itakuwa kubwa zaidi,” anasema.


Itaendelea kesho