Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Shule yatishia usalama wa wanafunzi

Muonekano wa moja ya vyumba vya madarasa Shule ya Msingi Izumbwe Wilaya ya Mbeya ikiwa na nyufa na matundu na kukosa madirisha kwa ajili ya kuzuia baridi kwa wanafunzi. Picha na Hawa Mathias.

Muktasari:

  • Shule hiyo ilijengwa miaka 50 iliyopita  ikiwa  ni miongoni mwa shule kongwe katika  Halmashauri ya  Mbeya Vijijini,  huku wanafunzi wakisomea kwenye vyumba vilivyo na nyufa na mashimo kwa nje.

Mbeya. Uongozi wa Shule ya Msingi Izumbwe II Halmashauri  ya Wilaya ya Mbeya, umesema baadhi ya wanafunzi wanasoma katika mazingira magumu kufuatia uchakavu wa miundombinu ya vyumba vya madarasa kuwa na nyufa na mashimo.

Shule hiyo imetajwa kuwa ni miongoni mwa shule kongwe katika Mkoa wa Mbeya ikiwa  imejengwa miaka 50 iliyopita huku  miundombinu yake ikiwa  sio rafiki na kuhatarisha usalama wa wanafunzi na usikivu mzuri kwenye masomo

Akizungumza leo Jumamosi Julai 13 ,2024   Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Ipyana Ndumba amesema shule  ina miundombinu  chakavu sana iliyosababisha kuta kuwa na nyufa na matundu, hali inayosababisha tatizo la utoro kwa wanafunzi na kutosoma kwa weledi.

"Watoto wanasoma katika mazingira magumu sana miundombinu ni chakavu tunaomba Serikali kuitazama kwa jicho la kipekee ili wanafunzi wasome kwenye mazingira mazuri na  kufanya vyema kwenye masomo kwa  kuongeza ufaulu,"amesema.

Amesema mbali na uchakavu wa vyumba vya madarasa pia kuna tatizo la huduma hali ambayo inasababisha watoto kutembea umbali mrefu kusaka huduma kutokana na mahitaji muhimu katika huduma za vyoo.

"Tunaishukuru Serikali kwa kuboresha sekta ya elimu kwa kutoa elimu bure kikubwa tunaomba shule za vijijini kukumbukwa kuboreshwa kwani mazingira ya kusomea na kujifunzia ni changamoto."amesema.

Eneo la ndani ya chumba cha darasa ambapo chini ya ubao kukiwa na nyuma.

Akizungumza kwa niaba ya  wazazi, Joseph Mwaigaga amesema shule hiyo ni miongoni mwa zilizojengwa kwa nguvu za wananchi kwa lengo la kuwapa maarifa watoto na imezalisha wataalamu wengi ambao wamelitumikia Taifa.

"Ni vyema sasa wadau hata  waliosoma katika shule ya Izumbwe  kuunga mkono juhudi za Serikali kuchangia ili iweze kufanyiwa ukarabati kwa kutambua ina mchango mkubwa katika maisha yao kwa kuwajengea maarifa"amesema.

Naye Mbunge wa Mbeya vijijini, Oran Njeza amesema atawasilisha changamoto hizo  maeneo husika na kuitaka jamii kushirikiana na Serikali kuchangia sekta ya elimu hususan miti kwa ajili ya kuchonga madawati huku yeye akichangia mafuta kwa ajili ya kupasua.

"Nitazungumza na watu wa halmashauri kuona namna bora ya  upatikanaji wa rasilimali fedha ili kunusuru madhara kutokea kwa wanafunzi kutokana  na changamoto ya  miundombinu chakavu "amesema Njeza.

Akitolea ufafanuzi wa changamoto hiyo Kaimu Ofisa elimu msingi, Daniel Mwala amesema tayari Serikali imetenga Sh50 milioni  kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu chakavu katika shule hiyo ambayo ni miongoni mwa shule kongwe nane ambazo ziko kwenye mpango.

"Hiyo ni miongoni kwa Shule kongwe lakini kuna nyingine ya  Irambo iliyojengwa mwaka 1950 sambamba na  Igale iliyojengwa mwaka 1930  ambazo zimekarabatiwa kwa gharama ya Sh 90 milioni kwa kila moja,  lengo ni kuboresha mazingira wezeshi ya elimu bora kwa watoto "amesema.