Shughuli za kibinadamu zaharibu misitu

Aliyesimama ni Diwani viti maalum Tarafa ya idodi akizungumza na wananchi wa Makifu kuacha mara moja tabia ya ukataji wa miti hovyo
Muktasari:
- Wakati dunia ikiadhimisha siku ya misitu shughuli za binadamu zikiwamo za ujenzi, kilimo na nishati zimetajwa kuharibu rasilimali hiyo.
Dar es Salaam. Ikiwa leo ni siku ya misitu duniani ambayo inaadhimishwa Machi 21 kila mwaka, Wakala wa Uhifadhi Misitu Tanzania (TFS) wamebainisha shughuli za kibinadamu kuwa changamoto kubwa za uhifadhi na utunzaji wa misitu.
Siku hiyo ilianza kuadhimishwa Tanzania mwaka jana ambapo ilihusisha shughuli za upandaji wa miti na kitaifa ilifanyika wilaya ya Magu mkoani Mwanza.
Akizungumza na Mwananchi leo Machi 21, Kamishna wa Uhifadhi Misitu (TFS) Profesa Dos Santos Silayo amesema bado kuna changamoto ambazo zinachangia sana kupotea au kuharibiwa kwa misitu nchini katika kipindi hiki cha mabadiliko ya tabia nchi.
“Ukosefu wa ajira kwa vijana wengi unafanya wanageukia rasilimali iliyo karibu na rahisi kuigeuza kuwa bidhaa na kupata fedha kwa bahati mbaya misitu imekuwa kimbilio la wengi,” amesema Silayo.
Amesema kuna utegemezi mkubwa wa nishati ya mimea (kuni na mkaa), kilimo cha kuhamahama au ufunguzi wa maeneo makubwa ya kilimo ambapo huchangia upotevu kwa wastani wa asilimia 73.
Ameongeza kuwa uvamizi kwa ajili ya makazi, uchimbaji madini holela na matumizi ya teknolojia duni za uchimbaji madini, kulisha mifugo na matukio ya moto pori ni miongoni mwa sababu za uharibifu wa misitu.
Kwa nyakati tofauti Serikali imekuwa ikiwataka wananchi waliovamia hifadhi za misitu kwa ajili ya makazi, kilimo na utafutraji wa nishati waondoke.