Mwanafunzi matatani kwa kujifungua mtoto na kumtupa chooni

Kamanda Masija wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu tukio la mwanafunzi aliyejifungua na kisha kumtupia mtoto kwenye shimo la choo.
Muktasari:
- Polisi wachunguza mwanafunzi aliyejifungua, kumtupa mtoto kisha kwenda darasani kusoma
Rukwa. Jeshi la Polisi mkoani Rukwa linaendelea kufanya uchunguzi wa kina kuhusu tukio linalomhusisha mwanafunzi wa kidato cha nne, Julitha Saimon (18) siyo jina lake sahihi, kutoka Shule ya Sekondari Nkasi, ambaye alijifungua na kisha kumtupa mtoto chooni.
Akizungumzia tukio hilo leo Jumatano Aprili 16, 2025, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Rukwa, Shadrack Masija amesema inadaiwa wiki iliyopita, mwanafunzi huyo alijifungua mtoto kisha kumtumbukiza kwenye shimo la choo cha nyumbani kwao na baadaye akaelekea shuleni kuendelea na masomo.
“Lakini asubuhi hiyo, baadhi ya watu waliopita karibu na choo hicho, walisikia sauti ya mtoto huyo ikitoka ndani ya choo wakachukua hatua ya kuja kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi, tuliwatuma askari eneo hilo na wakamuokoa mtoto huyo ambaye mpaka sasa yuko hai na anaendelea vizuri,” amesema kamanda huyo.
Amesema baada ya ukoaji huo, mtoto aliwahishwa hospitali kwa ajili ya matibabu.
Hata hivyo, amesema baada ya binti huyo kuhojiwa, alikiri kufanya tukio hilo na hajui ni nini kilimsukuma amtupe mwanawe chooni baada ya kujifungua.
"Alijifungua mtoto akiwa katika choo cha nyumbani kwao bila hata familia yake kujua chochote, akaamua kumtumbukiza chooni na yeye akaelekea shuleni,” amesema Kamanda Masija.
Kamanda huyo amesema kwa sasa mwanafunzi huyo amekabidhiwa mtoto wake kwa ajili ya kumnyonyesha.
Aidha kamanda huyo amesema uchunguzi wa awali unaonyesha huenda mwanafunzi huyo alipata changamoto ya afya ya akili wakati wa kujifungua.
“Wataalamu wanasema wajawazito hukumbwa na changamoto mbalimbali za kiafya, zikiwamo matatizo ya afya ya akili. Hii ndiyo sababu Jeshi la Polisi linaendelea kufanya uchunguzi wa kina kuhusu tukio hili. Endapo itabainika kuwa mwanafunzi huyo alichukua hatua hizo kwa makusudi, hatua kali za kisheria dhidi yake zitachukuliwa,” amesema kamanda huyo.
Amesema baada ya uchunguzi kukamilika, mwanafunzi huyo atafikishwa mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake.
Katika hatua nyingine, Masija amewataka wazazi na walezi kuwa karibu na watoto wao ili waweze kubaini mapema iwapo wanapitia changamoto zozote.
"Haiwezekani mwanafunzi awe mjamzito na mzazi asiwe na taarifa yoyote, ilhali wanaishi pamoja. Hii inaashiria ukosefu wa uangalizi wa karibu kutoka kwa wazazi," amesema Kamanda huyo.
Hata hivyo, Mwananchi imefanya mahojiano na Dk Deus Julius kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Sumbawanga, ambaye amesema kitaalamu inawezekana mwanafunzi huyo alipata tatizo la afya ya akili.
"Kwa kuzingatia mazingira ya tukio, inawezekana alikusudia kuficha ushahidi, hivyo alijipanga kuhakikisha hakuna anayegundua alichokuwa anakifanya," amesema Dk Julius.
Aidha, ametoa wito kwa wanafunzi kuacha tabia ya kujihusisha na ngono zembe ambazo husababisha mimba za utotoni na badala yake wajikite katika masomo yao.
Shuhuda wa tukio hilo, Emiliana Josephati, amesema alisikia sauti ya mtoto ikitokea chooni, lakini hakuwahi kumtilia shaka binti huyo kuwa alikuwa na ujauzito.
"Hili jambo linashangaza sana. Ujasiri alioonyesha kwa kuficha siri hii mpaka anajifungua bila mzazi wala walimu kujua chochote ni wa kipekee," amesema Emiliana.