Mama adaiwa kumnyonga mwanawe, kisa baba kumkana

Muktasari:
- Mwanamke huyo ambaye ni muhudumu wa baa katika eneo la Lerangwa, anadaiwa kufanya tukio hilo Januari 13 na kisha kuutelekeza mwili wa mtoto huyo kando mwa Mto Ngarenairobi Wilaya ya Siha.
Moshi.

Mwanamke huyo ambaye ni muhudumu wa baa katika eneo la Lerangwa, anadaiwa kufanya tukio hilo Januari 13, 2025 na kisha kuutelekeza mwili wa mtoto huyo kando mwa Mto Ngarenairobi Wilaya ya Siha.
Akizungumzia tukio hilo leo Jumatatu Januari 20, 2025 alipopigiwa simu na Mwananchi Digital, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa amethibitisha kutokea kwa tukio hilo.
Kamanda huyo amesema uchunguzi wa awali umebaini baada ya mama huyo kujifungua, alianza kutoka na mtoto huyo akiwa na siku 21 huku akiwaeleza majirani zake kuwa anampeleka kwa baba yake jambo ambalo liliwashangaza.

Mariam Samweli, mama mkubwa wa marehemu Noela Samwel ambaye ana siku 21, akilia kwa uchungu wakati wa maziko ya kichanga hicho ambacho kimezikwa katika makaburi ya Soweto, Manispaa ya Moshi. Picha na Omben Daniel
"Huyu mama alijifungua mtoto na baada ya wiki tatu watu walimwona akitoka naye akisema anampelekea baba yake, lakini siku ya tukio, hakurudi na mtoto, ndipo majirani waliposhikwa na mashaka na baadaye wakapata taarifa za kuokotwa kwa mtoto mchanga akiwa ameviringishwa nguo na kutelekezwa pembezoni ya mto akiwa ameshakufa,” amesimulia Kamanda Maigwa.
Hata hivyo, amesema tayari polisi wanamshikilia mwanamke huyo kwa mahojiano zaidi kabla ya kuchukua hatua zaidi za kisheria dhidi yake.
Akizungumzia tukio hilo dada wa mtuhumiwa, Mariam Samweli amesema limewaumiza sana kama familia na kusisitiza kuwa hata kama ni ugumu wa maisha, haikustahili kufikia hatua ya kufanya kitendo hicho.
"Nilipigiwa simu nikaarifiwa kuwa mdogo wangu amemnyonga mtoto na kumtupa Ngarenairobi mpakani mwa Kenya. Tukio hili limetuathiri sana kama familia," amesema Mariam.
Amesema walipomuuliza ndugu yao sababu ya kufanya kitendo hicho, aliwajibu kuwa ni ugumu wa maisha.
Kwa upande wake, Vicky Massawe mwanaharakati na mtetezi wa haki za binadamu kutoka Mkoa wa Kilimanjaro, amelaani vikali tukio hilo.
Amesema hata kama mwanaume alimkataa mtoto huyo, haikuwa sahihi kuchukua uamuzi wa kukiua kichanga kisicho na hatia.
"Tulipata taarifa hizi kanisani jana kwamba mwanamke huyo alitelekezwa na mume wake, jambo lililomfanya aamue kumuua mtoto wake," amesimulia Vicky.
Amesema’ "Mtoto hana kosa lolote. Kama mnakosana ni suala lenu wawili, mtoto hana hatia. Haya ni maamuzi mabaya sana na tunalaani vikali kitendo hiki cha kinyama. Ifike mahali jamii ikemee mauaji haya kwa nguvu zote ili yakome."