Shirima kortini madai ya kujitambulisha kama Spika wa Bunge

Muktasari:
- Shirima anakabiliwa na mashitaka 42 yakiwemo ya kujipatia fedha na kujitambulisha kwa watu kuwa yeye ni spika wa bunge, wakati akijua kuwa ni uongo.
Dar es Salaam. Mkazi wa Kipunguni, Charles Shirima, amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kusomewa mashitaka 42 yakiwemo kujitambulisha kuwa yeye ni Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Tulia Ackson, kutumia laini ya simu iliyosajiliwa kwa jina la mtu mwingine na kitapeli watu na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu pamoja na kutakatisha Sh2.8 milioni.
Pia, Shirima anadaiwa kuchapisha taarifa za uongo katika mtandao wa kijamii wa Facebook kuwa Tulia Trust Foundation inatoa mkopo kuanzia Sh2 milioni hadi Sh50 milioni, wakati akijua kuwa ni uongo.
Mshtakiwa huyo amefikishwa mahakamani hapo leo Mei 7, 2025 na kusomewa kesi ya uhujumu uchumi na wakili wa Serikali, Michael Shindai, mbele ya hakimu Mkazi Mkuu, Romuli Mbuya.
Hata hivyo, kabla ya kusomewa mashitaka hayo, hakimu Mbuya amesema mshtakiwa hatakiwi kujibu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza kesi za uhujumu uchumi isipokuwa kwa kibali maalumu.
Pia shitaka la kutakaisha fedha linalomkabili Shirima, halina dhamana kwa mujibu wa sheria, hivyo mshtakiwa atapelekwa rumande.
Akimsomea mashitaka yake, wakili Shindai amedai kuwa shitaka la kwanza hadi la tisa, mshtakiwa anatuhumiwa kuchapisha taarifa za uongo kwenye mitandao wa kijamii wa Facebook, kinyume cha sheria.
Ilidaiwa kuwa kati Desemba 30,2024 maeneo yasiyojulikana, ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Shirima alichapisha taarifa za uongo katika mtandao wa kijamii wa Facebook kuwa Tulia Trust Foundation inatoa mkopo kuanzia Sh2 milioni hadi Sh50 milioni, wakati akijua ni uongo.
Katika shitaka la 10 hadi 19, wakili Sondai amedai mshtakiwa anatuhumiwa kujitambulisha kwa watu mbalimbali kuwa yeye ni Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Tulia Ackson Mwansasu, wakati akijua ni uongo
Inadaiwa kuwa katika tarehe tofauti kati ya Desemba 31,2024 hadi Aprili 2025 ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mshtakiwa huyo kupitia mtandao wa Whatsapp alijitambulisha kwa David Silvester Musagasa, Upendo Lawrence Kiwelu na wengine sita kuwa yeye ni Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Tulia Ackson Mwansasu na angeweza kuwapatia mikopo wakati akijua ni uongo.
Kuanzia shitaka la 20 hadi la 37 mshtakiwa alijipatia pesa kwa watu mbalimbali kwa njia ya udanganyifu.
Ilidaiwa kuwa kati ya Januari 31, 2025 na Aprili 29, 2025 mshtakiwa huyo alijipatia Sh2.8 milioni, kupitia laini za simu zilizosajiliwa kwa majina ya Abdurmalik Said, David Musagasa, Upendo Kiwelu, Jane Mzelela, Suzana Bahaye na wengine 15 kwa madai ya kuwa atawapatia mkopo huku akijua si kweli.
Vilevile, shitaka la 38 hadi la 41, Shirima anatuhumiwa kutumia laini ya simu iliyosajiliwa kwa majina ya mtu mwingine bila kutoa taarifa kwa mtoa huduma ambaye ni Mamlaka ya Mawasiliano nchini (TCRA).
Miongoni mwa mashitaka hayo anadaiwa kuwa kati Aprili 29, 2025 maeneo ya Kipunguni B Wilaya ya Ilala, Shirima alitumia namba ya simu iliyosajiliwa kwa jina la Abdurmalik Said, Merina Shirima na Anna Tadei, huku akijua kufanya hivyo ni kosa kisheria.
Shindai amedai shitaka la 42 ni kutakatisha fedha, jambo analodaiwa kulitenda kati ya Desemba 24, 2024 hadi Aprili 2025, alijipatia Sh2.8 milioni, wakati akijua fedha hizo ni zao tangulizi la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.
Baada ya kumsomea mashitaka hayo, upande wa mashitaka ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika, hivyo wanaomba tarehe nyingine kwa akili ya kutajwa.
Hakimu Mbuya aliahirisha kesi hiyo hadi Mei 22, 2025 kwa kutajwa na mshtakiwa amepelekwa rumande katika Gereza la Keko.