Shigongo afichua NHIF ‘inavyopigwa’

Muktasari:
- Wabunge wameendelea kuchangia Muswada wa Bima ya Afya kwa Wote kwa ajili ya kuuboresha ambapo Mbunge wa Buchosa (CCM) Eric Shigongo ametoa angalizo.
Dodoma. Mbunge wa Buchosa (CCM), Eric Shigongo amesema wapo baadhi ya watu wanatumia kadi za bima za afya za Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kupata fedha za kununulia chakula.
Shigongo amesema hayo leo Jumatano Novemba Mosi, 2023 wakati akichangia Muswada wa bima ya afya kwa wote wa mwaka 2022.
Amesema hana kumbukumbu kama kuna mfuko mwingine ambao unaibiwa kama NHIF, lakini ukweli ni kwamba kuna watu wamekuwa mabilionea kwasababu ya mfuko huo.
“Nikupe mfano mmoja kadi ya bima ya afya siku hizi ni pesa mtu anaweza kwenda nayo akamwambia mwenye hospitali nipatie Sh30,000 nikanunue chakula, akampa, akasaini nyaraka akaondoka. Huku nyuma daktari anajaza anachotaka,”amesema Shigongo.
Amesema hilo wanalifahamu na kwamba wiki iliyopita walimkamata mtu Songea akifanya jambo hilo hilo.
Aidha, amesema kuna changamoto ya mifumo kutosomana na hivyo kufanya wagonjwa kurudia vipimo kwa kila hospitali wanayokwenda.
Amesema hali hiyo inafanya NHIF kuingia hasara kubwa kwa wagonjwa kuwa na matibabu mara mbili na kwamba ikiendelea hivyo hata wakibadilisha sheria mfuko huo utakuja kufa.
Ametaka mfumo huo kuboreshwa na kuwa na mfumo unaosomana ili kuokoa fedha nyingi zinazopotea kutokana na changamoto hiyo, hivyo kuepusha hasara.
Amesema tofauti na hapo mfuko huo utarudi tena katika wodi mahututi na hivyo mfuko huo utakufa.
Aidha, Shigongo ametaka Serikali kuwekeza katika kuwakinga watu kuugua badala ya kuwatibu.
Amehoji kwa nini mfuko huo usichukue sehemu ya fedha wanazopewa kwa kuwekeza katika vyumba vya mazoezi na elimu juu ya afya.