Sheikh Doga afariki dunia, kuzikwa leo Dar

Muktasari:
- Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Bakwata, Sheikh Khamis Mataka amethibitisha kuwa Sheikh Doga amefariki dunia na taratibu zote za mazishi zitafanyika nyumbani kwa Marehemu Temeke Mwembe Yanga
Dar es Salaam. Mwanazuoni ambaye ni sheikh maarufu, Muharram Juma Doga amefariki duania usiku wa kuamkia leo Jumanne, Agosti 20, 2024 katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Temeke jijini Dar es Salaam alipokuwa akipatiwa matibabu.
Akizungumza na Mwananchi, Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Bakwata, Sheikh Khamis Mataka amesema Sheikh Doga amefariki duania na taratibu zote za mazishi zitafanyika nyumbani kwa marehemu Temeke Mwembe Yanga na anatarajiwa kuzikwa leo baada ya Swala ya Adhuhuri.
Akizungumzia enzi za uhai wake, Mataka amesema ni mwanazuoni mkubwa ambaye alitumia sehemu kubwa ya maisha yake kujitolea kuelimisha jamii.
“Sheikh Doga amekuwa mwalimu wa masheikh mbalimbali hapa nchini, vijana wengi ambao sasa ni masheikh wamepita katika mikono yake,” amesema.
Pia, amesema mbali na kufundisha vijana alikuwa akitoa mawaidha pamoja na elimu ya masuala ya dini na maisha kwa misingi ya kiislamu katika vyombo mbalimbali vya habari kwa kipindi cha muda mrefu.
“Licha ya kuwa na elimu ya kiwango kikubwa lakini alikuwa ni mtu wa watu, hakuwa na makuu wala majivuno alisaidia watu bila kuwabagua,” amesema Sheikh Mataka.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Al-Hikma, Sheikh Nurdin Kishki kupitia akaunti yake ya mtandao wa Instagram amesema dunia imeondokewa na mmoja kati ya wanazuoni wakubwa na kuomba watu kuendelea kumuombea dua.
“Waislamu wote duniani tumeondokewa na mwanawachuoni mkubwa mno, Sheikh Muharram Juma Doga, Allah amreham amsamehe na amlaze pahala pema peponi, Tusimsahau kwa dua,” ameandika Sheikh Kishki.