Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sh10 bilioni kukusanywa kupitia leseni 71 za uvuvi

Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi, Shaaban Ali Othman

Muktasari:

  • Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi yataja vipaumbele 12 kwa mwaka wa fedha wa 2024/25.

Unguja. Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi, kupitia Mamlaka ya Kusimamia Uvuvi wa Bahari Kuu, inatarajia kutoa leseni 71 za uvuvi kwa meli za uvuvi wa bahari kuu za ndani na nje ya nchi.

Hilo ni miongoni mwa vipaumbele 12 vya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha wa 2024/25.

Kutokana na leseni hizo na vibali vya uvuvi, wizara inatarajia kukusanya Sh10.8 bilioni kwa mwaka 2024/25.

Hayo yamebanishwa na Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi, Shaaban Ali Othman alipowasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo Juni 7, 2024 katika mkutano wa 15 wa Baraza la Wawakilishi, Chukwani, Zanzibar.

Ili kutekeleza mipango ya bajeti hiyo, waziri ameliomba Baraza kuidhinisha matumizi ya Sh66.012 bilioni kwa ajili ya kazi za kawaida na miradi ya maendeleo ya wizara. Kati ya fedha hizo Sh10.985 bilioni ni kwa shughuli za kawaida na Sh55, 027 bilioni ni kwa shughuli za maendeleo.

Pia amesema mamlaka kwa kushirikiana na kampuni ya Albacora, itatekeleza mpango wa ujenzi wa kiwanda cha kuchakata samaki katika Manispaa ya Tanga.

Kipaumebele kingine amesema ni kuendelea kutoa elimu kwa wadau kuhusu vivutio na fursa zinazopatikana kwenye uvuvi wa bahari kuu na kuimarisha utekelezaji wa sheria na kanuni za usimamizi na uendelezaji wa uvuvi huo.

“Kufanya mazungumzo na wawekezaji zaidi wa ndani na nje ya nchi ili kuchukua leseni za uvuvi wa bahari kuu na kuwekeza katika miundombinu muhimu,” amesema akitaja kipaumbele kingine.

Wizara pia itaimarisha ulinzi na usalama wa rasilimali za uvuvi katika ukanda wa uchumi wa bahari kwa kuweka waangalizi wa uvuvi na kufanya ukaguzi wa meli zitakazoomba leseni na zitakazokuwa zikivua kwa kufanya doria za anga na kwenye maji kwa kushirikiana na jumuiya za kikanda.

Kipaumbele kingine ni kuendelea kuratibu na kuwezesha utekelezaji wa utafiti na kuwezesha upatikanaji wa taarifa kuhusu maeneo yenye samaki wengi (PFZ) baharini kwa kutumia simu janja.


Uhifadhi rasilimali za bahari

Waziri Shaaban amesema wizara inatarajia kuanzisha mfumo wa ufuatiliaji kwa viumbe walio hatarini kutoweka ili kuimarisha uhifadhi wa viumbe hao.

Pia kuanzisha kanuni na miongozo ya usimamizi wa wanyama wa bahari, wakiwamo pomboo na viumbe wengine katika maeneo ya hifadhi.

Wizara itaimarisha doria 340 na ulinzi shirikishi katika maeneo ya maji ya ndani kwa kununua boti tatu za doria ili kudhibiti uvuvi haramu.

Wizara kupitia Kampuni ya Uvuzi Zanzibar (Zafico) imesema imejipanga kuendelea na utaratibu wa ununuzi wa meli ya uvuvi kupitia programu ya kuendeleza kilimo na uvuvi (IFAD).

Kupitia programu hiyo, amesema Zafico inaendelea na mchakato wa ujenzi wa kiwanda jumuishi cha kuchakata samaki na mitambo ya baridi kitakachojengwa Fungurefu Mkokotoni, Mkoa wa Kaskazini, Unguja.


Maendeleo ya uvuvi

Wizara imepanga kuimarisha kilimo cha mwani na kuongeza uzalishaji wa mwani kutoka tani 16,564 za sasa hadi tani 20,000 kwa kuwapatia wakulima elimu na vifaa vya kisasa vya kilimo.

Pia itatoa elimu ya uvuvi bora na endelevu kwa wavuvi wadogowadogo na ufugaji wa mazao ya baharini kwa wafugaji, ujenzi wa masoko na majokofu mawili ya kisasa Unguja na Pemba ili kuimarisha sekta ya uvuvi.

Wizara imesema itaimarisha uchakataji wa mazao ya baharini kwa kujenga vituo vya usarifu na uongezaji wa thamani wa mazao ya baharini ikiwemo mwani, Unguja na Pemba.


Mafuta na gesi

Wizara kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Utafutaji na Uchimbaji wa Mafuta na Gesi Asilia imepanga kuendelea na shughuli ya kuvitangaza vitalu vinane vipya vilivyopo Mashariki mwa bahari ya Zanzibar kupitia majukwaa ya kitaifa, kikanda na kimataifa.

Amesema watakaribisha wawekezaji kwa ajili ya shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi asilia na kusimamia utekelezaji wake.

Mamlaka itaendelea na programu ya ugawaji upya wa vitalu kwa eneo la kitalu cha Pemba – Zanzibar pamoja na kuvitafutia wawekezaji kwa ajili ya shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi asilia na kusimamia utekelezaji wake.

“Kukamilisha majukumu ya kisheria na kimkataba ikiwemo ulipaji wa fidia kwa wananchi waliobakia kutokana na kazi ya utafutaji wa mafuta na gesi asilia kwa njia ya mtetemo lililofanywa na Kampuni ya RAKGas,” alisema.

Waziri Shaaban katika bajeti hiyo, amesema watakamilisha miundombinu ya matumizi ya kituo cha muda cha uhifadhi wa taarifa (TDC) kupitia mradi wa NDR na kutoa taarifa na machapisho kuhusu shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi asilia nchini.

Amesema lengo kuu la wizara ni kukuza uchumi wa Zanzibar kwa kuimarisha matumizi endelevu ya bahari na kuwawezesha wajasiriamali ili kukuza ubunifu, uwezo wa kupata zana za kisasa, mitaji na masoko.

Lengo lingine amesema ni kuchangia katika sekta ya uwekezaji na uimarishaji wa minyororo ya thamani ambayo itasaidia upatikanaji wa ajira na masoko kwa vijana kupitia uchumi wa buluu.


Michango ya wawakilishi

Akichangia mjadala wa hotuba hiyo, mwakilishi wa Mfenesini, Machano Othman Said aliitaka wizara kutenga maeneo maalumu yanayouzwa samaki aina ya peduu badala ya kuwachanganya kwenye masoko mengine kwani watu wanakula kitoweo hicho bila kupenda.

Amesema licha ya kugawa boti 527 za uvuvi, bado wavuvi wengi hawana vifaa vya kuvulia, hivyo kuitaka Serikali kuongeza mkakati wa kuwapatia vifaa wavuvi hao.

Kuhusu mradi wa kuchimba mafuta na gesi, alitoa angalizo akisema ulianza tangu utawala wa awamu ya saba lakini ulimaliza muda wake bila mradi huo kukamilika.

Amesema wanapata wasiwasi isije hata awamu ya nane ikamaliza bila kukamilika na kutaka wajipange katika udhibiti wa uharibifu wa mazingira.

Mwakilishi wa Mkwajuni, Sulubu Kidongo Amour aliitaka Serikali kuangalia utaratibu mpya kwa wavuvi waliokopeshwa boti kwani kiwango walichopangiwa kurejesha cha Sh24, 000 kwa siku ni kikubwa.

Amesema wavuvi bado ni wachanga na fedha hizo hazitalipwa.

“Hakuna mvuvi atakulipa Sh24, 000 kwa siku, inawezekana mvuvi akamaliza siku nne hajapata kitu sasa umwambie akulipe kiasi hicho cha fedha, hiki kima ni kirefu sana fanyeni maarifa ili watu wapate kurejesha fedha vizuri,” alisema.

Amesema katika ugawaji wa boti, kuna dosari ndogo zilijitokeza hivyo wajitahidi kuziondoa, akisema vipo vikundi ambavyo vilikamilisha taratibu zote lakini hawakupatiwa lakini waliopeleka maombi mwisho walipewa na ushahidi wa jambo hilo anao, wakitaka atautoa.

Kuhusu kampuni ya mwani kuanza kununua zao hilo na kujenga kiwanda cha kulichakata alisema:

“Kujenga kiwanda ni jambo moja na soko jambo lingine ila wanaponunua waende sambamba na kuongeza bei ya mwani badala ya hii Sh700 kwa kilo ambayo inawakatisha tamaa wakulima.”

Akizungumzia bei ya mwani, mwakilishi wa Kojani, Hassan Hamad Omar amesema:

“Bei ya mwani inakwaza sana wakulima lazima jambo hili liangaliwe kwa jicho la kipekee kwa wakulima hawa.”