Serikali yawakatia rufaa wanaotuhumiwa kulawiti, kumrekodi aliyelawitiwa

Muktasari:

  • Watuhumiwa hao wanne akiwemo mwanajeshi walifikishwa Mahakama ya Wilaya ya Mtwara wakituhumiwa kumteka mtu kwa lengo la kumlawiti na kushawishi watu wafanye makosa pamoja na kuchukua video ya mwathiriwa akiwa analawitiwa.

Mtwara. Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Mkoa wa Mtwara imekata rufaa katika Mahakama Kuu mkoani hapa juu ya hukumu iliyotolewa katika Mahakama ya Wilaya ya Mtwara dhidi ya washtakiwa wanne akiwemo mwanajeshi mmoja walioshtakiwa kwa makosa mbalimbali likiwemo la ulawiti.

Washitakiwa hao ni mwanajeshi mwenye cheo cha Koplo namba MT 95850 Shaibu Yusuf Said, Bahati Joseph Aduma (20) Mkulima, Selemani Hamis Baise (29) ambaye ni mkulima na kijana mwenye miaka 17, (jina linahifadhiwa) wote wakazi wa eneo la Naliendele Wilayani Mtwara.

Washtakiwa hao wote kwa pamoja walifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Januari 14, 2021 kwa mashtaka mbalimbali likiwemo la kumteka mtu kwa lengo la kumlawiti, kushawishi watu wafanye makosa pamoja na kuchukua video ya mwathirika akiwa analawitiwa.

Mkuu wa Mashtaka Mkoa wa Mtwara, Joseph Maugo ameiambia Mwananchi Digital leo Machi 22, 2023 kuwa tayari wameshakata rufaa siku chache baada ya hukumu ya kesi hiyo namba 2 ya mwaka 2021 kutolewa Desemba 20, 2022.

Hukumu ya kesi hiyo ilitolewa Desemba 20, 2022 na Hakimu wa Mahakama hiyo, Lucas Jang'andu ambaye alitoa uamuzi kuwa makosa ya kulawiti na kuchukua video hayajathibitika kwa washitakiwa watatu ila la kumteka mtu lilithibitika kwa washtakiwa wote.

Mshtakiwa namba moja wa kesi hiyo ambaye ni mwanajeshi amepewa adhabu ya kulipa kiasi cha Sh1 milioni au kwenda jela miezi kumi na mbili.

Mshtakiwa namba tatu, Selemani Baise alitiwa hatiani kwa kosa la kulawiti lakini hata hivyo alikimbia hajulikani alipo.

"Upande wa Jamhuri hatujaridhika na hayo maamuzi tunaamini kwamba ushahidi uliowasilishwa Mahakamani ulikuwa unatosha kuthibitisha makosa yote pasipo kuacha shaka yoyote" amesema Mkuu wa Mashtaka.

Awali, Mahakama hiyo ilielezwa kuwa mnamo Januari 4, 2021 washtakiwa hao walimteka Mhanga maeneo ya Mbae kisha wakampeleka Pori la Ludipe na kumfanyia vitendo vya ulawiti, wakiwa wamemfunga pingu, huku wakichukua picha ya video.

Ushahidi wa video hizo uliwasilishwa mahakamani hapo ukionyesha tukio zima huku ambalo sauti za washtakiwa zikisikika.

Hata hivyo wakati mwenendo wa kesi ukiendelea washitakiwa namba mbili na tatu walikimbia (waliruka dhamana).

Chanzo cha kitendo hicho kilielezwa mahakamani hapo kuwa ni wivu wa kimapenzi ambapo ilidaiwa kuwa mshitakwa namba moja alikuwa na mke wake ambaye walishatengana na baadaye kugundua kuwa alikuwa na mahusiano ya kimapenzi na mwathirika wa tukio la ulawiti.

Baada ya kusikiliza zaidi ya mashahidi 19 wakiwemo wataalamu wa picha za video na washitakiwa wawili waliobaki, mwanajeshi na kijana wa miaka 17 kujitetea wenyewe ndipo mahakama ilipotoa maamuzi hayo.

Shitaka hilo liliendeshwa kwa ushirikiano wa Mmawakili waandamizi wa Serikali Wilbroad Ndunguru na Paul Kimweri.