Serikali yapiga marufuku uuzaji asali isiyochakatwa nje ya nchi

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja

Muktasari:

Serikali imezuia uuzaji wa asali isiyochakatwa nje ya nchi ikisema uuzaji huo unaondoa thamani ya zao hilo.

Dodoma. Serikali imezuia uuzaji wa asali isiyochakatwa nje ya nchi ikisema uuzaji huo unaondoa thamani ya zao hilo.

 Agizo hilo limetolewa leo Jumatatu Februari 21, 2022 jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja wakati akizindua Programu ya Uwezeshaji na Mwongozo wa Ufuatiliaji Nyuki.

Amesema kwa sasa Tanzania ina viwanda vinavyotosha kuchakata asali yote inayozalishwa nchini.

Masanja amesema hata asali inayouzwa ndani ya nchi inapaswa kuchakatwa kwa ajili ya kuwekwa ubora unaotakiwa kwa watumiaji kuliko kuwauzia ilivyo.

Kuhusu programu hiyo, amewashuru Umoja wa Ulaya waliofadhili mradi huo kwa kutoka Euro 10 milioni ambayo ni sawa na Sh27 bilioni katika mikoa saba ikiwemo Tanzania Bara 5 na mikoa miwili ya Zanzibar.

"Wananchi washiriki kwa pamoja na programu hii, lakini wasimamizi kuweni karibu na wananchi katika kuwahamasisha na kuwapa miongozo mbalimbali ili tufanikiwe," amesema Masanja.

Amesema kuwa Serikali inalenga kuzalisha asali hadi tani 138,000 kwa mwaka ikiwa watu watahamasika na kuchangamkia mpango huo.

Amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kushirikiana na makatibu wakuu wengine kutenga maeneo ya ufugaji nyuki ili watu waweze kufuga kibiashara.

Balozi wa Umoja wa Ulaya, Manfredo Fanti amesema soko la asali kwa nchi za Ulaya ni kubwa na bado wanahitaji kiasi kikubwa kutoka Tanzania ndio maana wamewekeza fedha nyingi ambazo ni msaada na siyo mkopo.

Balozi Manfredo amesema hakuna kiwango kamili kinachotakiwa kupelekwa huko isipokuwa ubora wa asali ndiyo utakuwa kigezo cha kutazamwa na watu wa Ulaya.