Serikali yanunua hisa zote za General Tyre

Mwakilishi wa Kampuni ya General Tyre (Continental AG)Michael Strain (Kushoto) na Msajili wa Hazina, Lawrence Mafuru wakitia saini katika hati za mauzo ya hisa asilimia 26 za kampuni hiyo kwenda Serikalini Dar es Salaam jana. Katikati ni Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue. Picha na Venance Nestory
Muktasari:
Tangu mwaka 2012, mazingira ya kurejesha uzalishaji katika kiwanda hicho yalikuwa yakiandaliwa pamoja na kuzungumza na mwekezaji
Dar es Salaam. Serikali imesema sasa inamiliki kiwanda cha kutengeneza magurudumu ya magari cha General Tyre kwa asilimia 100 baada ya kununua hisa zote 26 zenye thamani ya Dola 1 milioni zilizokuwa zikimilikiwa na kampuni ya Continental AG.
Akizungumza wakati wa makabidhiano ya nyaraka mbalimbali kati ya Serikali na kampuni hiyo jana, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue alisema kumekuwa na maneno kuwa Serikali imekitekeleza kiwanda hicho na vingine, jambo ambalo alisema si la kweli.
Alisema tangu mwaka 2012 Serikali imekuwa ikiandaa mazingira ya kufufua uzalishaji katika kiwanda cha General Tyre wakati mazungumzo na mwekezaji yakiendelea na sasa wamefikia makubaliano.
“Tumejiridhisha kwamba kila kitu kimekwenda vizuri kwa misingi ya sheria kama tulivyoshuhudia hapa, kwa hiyo sasa tupo tayari kuendelea na hatua inayofuata ya kumtafuta mwekezaji mahiri ambaye atashirikiana na NDC (Shirika la Maendeleo la Taifa) katika uzalishaji kwa kutumia teknolojia ya kisasa zaidi,” alisema Sefue na kuongeza kuwa mchakato wa kuimiliki Kampuni ya Simu ya TTCL kwa asilimia 100 nao unaendelea.
Kwa upande wake, Msajili wa Hazina, Lawrence Mafuru alisema jitihada za Serikali kukifufua kiwanda hicho kilichoanzishwa mwaka 1969 zilikuwa zikikwamishwa na mwekezaji aliyekuwapo baada ya kuonyesha dalili za kutotaka kuendelea kuwekeza.
“Ilikuwa vigumu kwa Serikali kufanya jitihada hizi bila kufahamu mwekezaji ana mawazo gani, ilikuwa dhahiri kwamba wakati fulani hawakuwa tayari kuwekeza,” alisema Mafuru.
Katibu mkuu wa Wizara ya Viwanda, Uledi Musa alisema wakati kiwanda hicho kinafungwa kilikuwa kinaweza kuajiri wafanyakazi 360, lakini kitakapoanza uzalishaji kitatoa ajira zaidi.
Hata hivyo, Musa alisema General Tyre wamezuia Serikali kuendelea kutumia nembo ya kampuni hiyo mara uzalishaji utakapoanza. Pia, alisema mchakato wa kuendelea kufufua viwanda vingi zaidi unaendea kimya kimya.
“Hapa tunazungumzia vile ambavyo Serikali inahisa kubwa, Serikali ilikuwa na hisa 74 lakini mwekezaji mdogo alikuwa ameshika mpini, hilo haliwezekani,” alisema Musa.