Prime
Serikali yamkalia kooni Wakili Mwabukusi

Wakili, Boniface Mwabukusi.
Arusha. Kamati ya Mawakili imemtaka wakili, Boniface Mwabukusi kujieleza kwa nini asichukuliwe hatua za kisheria kwa madai ya kumkosea Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Barua ambayo Mwananchi imeiona iliyosainiwa na katibu wa Kamati hiyo, Faraji R. Ngukaha, ilitumwa Julai 14 na kupokelewa na Mwabukusi Julai 31, 2023.
Akizungumza jijini Arusha ambapo jana alijiunga na jopo la mawakili wanaomtetea wakili mwenzake Peter Madeleka, Mwabukusi alikiri kupata mashitaka hayo akisema anachojua hajafanya kosa lolote la kimaadili lakini tayari alijiandaa kwa lolote.
Jana Wakili Mwabukusi alikiri kuipokea barua hiyo yenye malalamiko dhidi yake, akisema imepokelewa ofisini kwake jijini Mbeya na ataijibu kwani hajafanya kosa lolote
"Wanafikiri kufanya hivi kutatuzuia kuzungumzia tatizo la mkataba wa bandari, lakini tutaendelea kuzungumza kwa sababu wanaounga mkono bandari hawana tatizo ila sisi ambao tunaopinga mkataba tunaonekana tunakiuka maadili," alisema.
Wakili Mwabukusi alisema yanayotokea sasa walijiandaa nayo, kwani tangu sakata la bandari kuanza wamekuwa wakikamatwa na kupokea vitisho vingi.
"Tulijua haya yatatokea lakini tulijiandaa na tunajua gharama yake, binafsi nitakabiliana nao bila hofu," alisema.
Tuhuma zenyewe
Chanzo cha mashitaka hayo ni kesi ya kikatiba namba 5 ya mwaka 2023 inayopinga makubaliano ya ushirikiano wa kijamii na kiuchumi baina ya Serikali ya Tanzania na ya Dubai (IGA) yanayohusisha uwekezaji katika bandari, iliyofunguliwa na wanasheria wanne kutoka mikoa tofauti, Alphonce Lusako, Emmanuel Kalikenya Changula, Raphael Japhet Ngonde na Frank John Nyalusi.
Mashitaka hayo yaliyosainiwa na Wakili Mkuu wa Serikali, Dk Boniface Luhende, yanamtuhumu wakili huyo kuwa mnamo Julai 3, 2023 baada ya kufungua kesi hiyo, aliitisha mkutano wa waandishi wa habari na kutoa tuhuma kwa viongozi wa mihimili ya Serikali akiwamo Spika wa Bunge.
Mashitaka hayo yamenukuu maneno yake yanayodaiwa kukashifu viongozi wa Serikali, Spika wa Bunge na kushusha imani ya umma kwa mfumo wa utoaji haki.
Sehemu ya maneno hayo yanasomeka: “Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hawajui walichopitisha bungeni kwamba hata Chifu Mangungo anasingiziwa maana yeye alijua kuwa mkataba… Serikali imekuwa ikiwadanganya wananchi, imesaini makubaliano na siyo mkataba.”
Maneno mengine anayodaiwa kuyasema ni|: ‘‘Fuatilieni hansard za Bunge, ndipo mtajua kwamba hakuna Spika, mtagundua kwamba, hamna Waziri na mtagundua kwamba, kwa sababu kama spika mwenyewe alikuwa hajui anapitisha kitu gani, waziri alikuwa anasaini kitu gani, ujue kwamba Chifu Mangungo was a genius.”
“Mbarawa na Katibu mkuu wake waondoke katika ile nafasi, wanahatarisha mali za Tanganyika, narudia kupigia mstari, wanahatarisha mali za Tanganyika sio mali za Zanzibar, yaani kwenye Muungano kuna mali za Zanzibar na mali za Tanganyika.
“Mali za Zanzibar wamebaki nazo kule, za Tanganyika zikawekwa chini ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano. Kwa hiyo walichokifanya ni kuchukua mali za Tanganyika na kuikabidhi infinite kwa mtu, ndiyo maana hukuti mtu yeyote anayetujibu anakuonyesha anakujibu kwa kifungu gani.”
Kutokana na maneno hayo, Kamati ya Mawakili imesema wakili huyo mwenye namba 1571 anatuhumiwa kufanya vitendo vya kijinai, kwa kutoa kauli za kashfa na zisizo za kitaaluma na kufanya makossa ya kimaadili.
“Maoni hayo yaliyotolewa na mtuhumiwa yakiwa na nia ya kukashifu kinyume cha kifungu cha 53(1) (b) cha Sheria ya Huduma za Habari, Na.12 ya mwaka 2016 na kifungu cha 55 cha Kanuni ya Adhabu [Sura 16, R.E 2002].
“Inaelezwa zaidi kuwa maoni hayo yalitolewa kuleta hofu na kuingilia mamlaka ya haki Tanzania yakilenga kukashifu umma au kiasi kikubwa kusababisha uvunjifu wa amani kwa mamlaka za nchi,” inasema sehemu ya maelezo ya mashitaka hayo.
Pia wakili huyo anatuhumiwa kukiuka kanuni za maadili ya uwakili katika Sheria ya Mawakili (Sura 341 RE 2002) na kanuni za Mawakili za mwaka 2018.
“Kwamba mtuhumiwa alikuwa na lengo la kukandamiza imani ya umma kwa mfumo wa haki,” imesema.
Endapo Mwabukusi atakutwa na hatia, huenda akajikuta kwenye hatari ya kuvuliwa uwakili kama ilivyotokea kwa rais wa zamani wa Chama cha Mawakili wa Tanganyika (TLS), Fatma Karume Septemba 23, 2020 akidaiwa kumdhalilisha aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dk Adeladius Kilangi, alipokuwa akisimamia kesi iliofunguliwa na Katibu mkuu wa chama cha ACT- Wazalendo, Ado Shaibu.