Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Serikali yaita wadau kuchangia vifaatiba

Katibu Tawala wa Wilaya ya Kinondoni, Stella Msofe akikabidhiwa vifaa tiba na  Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Garda World, Goodluck Lukunay (mwenye miwani) kwa ajili ya wanaojifungua katika Hospitali ya Mwananyamala jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo Zavery Benela. Picha na Michael Matemanga

Muktasari:

  • Huenda changamoto ya vifaatiba kwa upande wa wodi za wazazi ikapungua kutokana na wadau kujitokeza kutoa msaada.


Dar es Salaam. Serikali imewataka wadau kuchangia huduma za afya hasa za mama na mtoto ili kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi.

Hayo yameelezwa leo Machi 13, 2024 na Katibu Tawala wa Wilaya ya Kinondoni, Stella Msofe kwa niaba ya mkuu wa wilaya hiyo, alipokuwa akipokea vifaa tiba vyenye thamani ya Sh27.7 milioni vilivyotolewa na Kampuni ya GardaWorld katika Hospitali ya Rufaa ya Mwananyamala, ikiwamo mashine ya kutambua mwenendo wa mtoto akiwa akiwa tumboni.

Vifaa vingine vilivyokabidhiwa ni pamoja na vitanda sita vya kujifungulia vinavyoweza kurekebishwa, viti sita vya magurudumu, mashine ya kuchungiza mapigo ya moyo ya watoti wachanga, mita nane za kupima mzunguko wa oksijeni na kifaa cha kufuatilia mwenendo wa magonjwa.

"Serikali katika kuhakikisha usalama wa mama na mtoto iliamua kutoa huduma hizo bure, lakini pia Serikali peke yake haiwezi bila kuwa na wadau wanaoweza kutoa msaada wa vifaa katika kusaidia kuokoa afya ya mama na mtoto," amesema Stella.

Akizungumzia vifaa hivyo, mganga mfawidhi wa hospitali hiyo, Dk Zavery Benela amesema wamekuwa na upungufu wa vifaa ikiwamo mashine ya Kardiotorografia (CTG) ambayo ipo moja katika wodi ya wazazi.

Amesema katika wodi ya wazazi wana CTG moja na iliyoletwa ni ya pili ambapo wanahitaji mashine nane na endapo zitapatikana zote zilizobaki zitasaidia kila mjamzito anapokuwa na uchungu anakuwa kuwa na mashine yake.

"Vifaa vinavyoletwa huwa tunajadiliana kwa ajili ya kupunguza mahitaji yanayohitajika hivyo tunatoa orodha ya vitu muhimu kwa wakati huo ili kuona ni namna gani tunawasaidia wagonjwa kwa wakati," amesema Dk Benela.

Amesema kutokana na uhaba huo wamekuwa wakihamisha mashine hiyo moja kutoka kwa mgonjwa mmoja kwenda kwa mwengine kwa ajili ya uchunguzi wa kidaktari.

Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya Wanawake na Afya ya Uzazi, Dk Maembe Luzango amesema vifaa walivyopokea vitasidia kuhakikisha mjamzito anaingia na kutoka salama.

Amesema changamoto waliyonayo kwa sasa ni kwa upande wa watoto kwa hiyo kifaa cha CTG kitasaidia kutambua kama kuna hatari na kuchukuliwa hatua ya haraka.

"Nia yetu ni kupunguza vifo vya watoto, hivyo tunahitaji kifaa cha CTG kwa sababu hicho ni kifaa kinachopima mapigo ya moyo ya mtoto na kinahakikisha mtoto anatoka salama na kulia kwa wakati na kina uwezo wa  kumuepusha na utindio wa ubongo," amesema Dk Maembe.

Mkurugenzi Mtendaji wa Gardaworld, Goodluck Lukunay amesema wamekabidhi vifaa katika hospitali hiyo na kulenga katika huduma ya uzazi kwa kuwa ni sehemu ambayo maisha ya binadamu huanzia lakini ukosefu wa vifaa imekuwa ni kizuizi cha usalama na ustawi wa mama na mtoto.

"Tunalenga katika usalama na ubora wa huduma ya uzazi, kupunguza hatari za matatizo wakati wa ujauzito, kabla na baada ya kujifungua, mchango huu una uwezo wa kuongeza idadi ya wajawazito kuazalia katika hospitali hii," amesema Lukunay.