Serikali yaingilia kati kuadimika kwa sukari nchini

Dar es Salaam. Serikali imetoa vibali kwa wafanyabiashara kuagiza tani 50,000 za sukari kutoka nje ya nchi, ikiwa ni hatua ya kunusuru kupanda kwa bei ya bidhaa hiyo nchini.
Hatua hiyo ya Serikali imetokana na ongezeko la bei na uhaba wa bidhaa hiyo katika mikoa mbalimbali, ikiwamo Manyara ambako kilo moja inauzwa Sh4,000 kutoka Sh3,000.
Hali ni mbaya zaidi katika Mkoa wa Arusha, bei ya kilo moja ya sukari imeongezeka kutoka Sh3,000 hadi Sh4,500 na Sh5,000.
Kwa upande wa Mkoa wa Kilimanjaro, kilo moja ya bidhaa hiyo kwa sasa inauzwa kwa Sh3,800 kutoka Sh3,000 ya awali.
Hata hivyo, wazalishaji wa sukari wamesema kupungua kwa uzalishaji wa bidhaa hiyo viwandani, kumesababishwa na mvua za El-Nino.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumanne Januari 2, 2023, Mkurugenzi wa Bodi ya Sukari (SBT), Profesa Kenneth Bengesi amesema kilichotokea si uhaba, ni dharura ya kupungua kwa uzalishaji viwandani.
Amesema uzalishaji huo umeathiriwa na mvua za El-Nino zilizosababisha viwanda vingi kusimama kuzalisha.
“Mvua ina athari kubwa kwenye uzalishaji wa sukari kwa sababu mashamba ya miwa mengi yapo mabondeni, ikinyesha mvua kubwa miwa inanyonya na inapunguza sukari,” amesema Profesa Bengesi.
“Lakini uvunaji unakuwa mgumu, huwezi kuingiza trekta kwa sababu yatakwama na miundombinu ya kuifikia miwa ni changamoto nyingine, iwapo mvua zinanyesha inaharibika zaidi,” amesema Profesa Bengesi.
Kwa kuzingatia mvua zinaweza kuendelea, Profesa Bengesi alisema Serikali imeshatoa vibali kuagiza tani 50,000 za sukari nje ya nchi kwa ajili ya tahadhari.
Alisema lingine lililofanyika ni kuhakikisha viwanda vyote vinarudi kuzalisha na tayari hilo limeanza kutekelezwa, hivyo siku chache baadaye kinachotokea sasa kitakwisha.
Hatua nyingine kwa mujibu wa Profesa Bengesi, ni kuwaonya wafanyabiashara wanaotumia mwanya wa kupungua kwa uzalishaji, kupandisha bei, ilhali viwandani bei haijaongezeka.
“Waache tabia hiyo, wanawaumiza wananchi, Serikali haitakaa kimya kuona wananchi wake wanaendelea kuuziwa sukari kwa gharama kubwa ilhali bei ya viwandani haijaongezeka,” amesema Profesa Bengesi.
Kuhusu changamoto ya uzalishaji, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Mkulazi Holding Limited, Selestine Some alitaja mvua za El-Nino kuwa sababu ya kupunguza uzalishaji wa sukari viwandani.
“Oktoba hadi Desemba ndiyo vipindi vya uzalishaji mkubwa wa sukari. Katika vipindi hivyo mvua zinaendelea kunyesha, zinaponyesha inabidi msubiri ikate ndiyo muendelee,” amesema Some.
“Kwa mfano sisi (Mkulazi) tulikuwa tunafanya matengenezo na tukapanga leo (jana) tuanze uzalishaji, usiku imenyesha mvua kubwa tumeshindwa kuzalisha.”
Some alisema hakuna sababu nyingine ya kuadimika na kupanda kwa bei ya sukari, zaidi ya kupungua kwa uzalishaji kulikosababishwa na mvua hizo.
Hata hivyo, alieleza uhaba uliopo si mkubwa na unaweza kumalizwa kwa viwanda vya ndani pekee.
“Deficit (uhaba) sio kubwa, ni vile tu viwanda vimepunguza uzalishaji sababu ya mvua, lakini tukizalisha kawaida ni jambo linalokwisha mara moja,” amesema Some.
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Gerald Mweli alisema hivi karibuni kuwa, Serikali inatarajia kutoa taarifa za kina kuhusu changamoto hiyo inayoendelea.
“Tumesikia kuhusu jambo hilo na tunalifanyia kazi, hivi karibuni tutatoa taarifa ya kina kupitia Bodi ya Sukari (SBT),” amesema Mweli.
Alipoulizwa kuhusu sababu za hali hiyo, alisema hayo yote yatabainishwa kupitia taarifa hiyo.