Bashe ataja mafanikio sekta ya kilimo mwaka 2023

Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe.
Muktasari:
- Waziri wa Kilimo Hussein Bashe amesema hatua ya Serikali kuipa kipaumbele wizara hiyo kumeipa mafanikio makubwa sekta hiyo inayoajiri Watanzania wengi zaidi.
Dar es Salaam. Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe amejivunia mafanikio 10 yaliyopatikana mwaka 2023, huku akipongeza uamuzi wa Serikali kutaka nchi ijitegemee katika uzalishaji na usambazaji wa pembejeo za kilimo, zikiwemo mbegu bora.
Bashe ameyabainisha hayo leo Januari Mosi katika salamu zake za mwaka mpya 2024 alizoitoa kwa vyombo vya habari, huku pia akichambua mafanikio katika sekta hiyo.
Amebainisha kuwa Serikali inaendelea na ujenzi miundombinu ya umwagiliaji katika hekta 19,387 za mashamba ya Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA) na vituo ya Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI).
Kwa mujibu wa Bashe, lengo ni kufikia mahitaji ya tani 652,250 za mbegu ifikapo mwaka 2030. Kati ya hizo, hekta 8,533.2 ni za mashamba 16 ya mbegu ya ASA na hekta 854.5 za vituo 17 vya TARI.
“Katika mpango huo wa kijitegemea, uzalishaji wa mbegu bora za mazao ya kilimo umeongezeka kutoka tani 50,747 mwaka 2021/2022 hadi tani 58,807.61 mwaka 2022/2023 sawa na ongezeko la asilimia 15.9.
“Kati ya hizo, tani 42,096.68 za mbegu bora sawa na asilimia 71.6 zimezalishwa hapa nchini kupitia ASA na kampuni binafsi, na tani 16,710.93 zimeagizwa kutoka nje ya nchi,” amebainisha.
Mbali na maamuzi ya kujitegemea kwenye pembejeo, pia waziri huyo amegusia kuongezeka kwa bajeti na hivyo kuiwezesha wizara kutoa mchango unaostahili katika uchumi kwa kuimarisha usalama wa chakula, kuongeza ajira, upatikanaji wa malighafi za viwanda na kukidhi mahitaji ya soko la ndani na kimataifa.
Amesema bajeti ya kilimo imeongezeka kutoka Sh751 bilioni mwaka 2022/2023 hadi Sh970 bilioni mwaka 2023/2024 sawa na ongezeko la asilimia 29.2 au asilimia 230 tangu Serikali ilipoamua kuongeza bajeti ya kilimo.
“Maeneo ya kipaumbele katika uwekezaji huo ni ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji, ghala, kuimarisha utafiti, uzalishaji wa mbegu bora na huduma za ugani,” amesema.
Wizara hiyo pia inaonekana kufurahia kuongezeka kwa matumizi ya mbolea nchini kutoka tani 363,599 mwaka 2021/2022 hadi tani 580,628 mwaka 2022/2023, huku Bashe akisema ongezeko hilo limetokana na Serikali kutoa mbolea ya ruzuku, kuimarisha uwezo wa Kampuni ya Mbolea (TFC) kwa kuipatia mtaji wa jumla ya Sh116 bilioni.
“Kuimarika kwa uzalishaji wa viwanda vya ndani na kuwezesha uanzishwaji wa kiwanda kipya cha mbolea cha ITRACOM chenye uwezo wa kuzalisha Tani 1,000,000 za mbolea kwa mwaka,” amebainisha.
Amesema Serikali itaendelea kutoa ruzuku ya mbolea hadi mwaka 2025 ikiwa ni hatua mojawapo muhimu ya kuimarisha matumizi ya pembejeo bora za kilimo.
“Pia bajeti ya huduma za ugani zimeongezeka kutoka Sh11.5 bilioni mwaka 2021/2022 hadi Sh17.7 bilioni mwaka 2022/2023. Maofisa ugani wamepewa vitendea kazi ikiwemo jumla ya pikipiki 5,889, vishikwambi 805, seti ya vifaa vya kupima udongo 142 na seti 1,579 za vifaa vya kazi katika Halmashauri 166.
“Serikali katika mwaka 2023/2024 imeanza kutekeleza mpango wa kujenga nyumba za maofisa ugani katika kata 4,000 nchini,” ameongeza.
Katika salamu hizo, Bashe amegusia suala la kilimo cha umwagiliaji huku akibainisha kuwa ofisi za umwagiliaji zimeanzishwa katika Wilaya 139, na kwamba wataalamu wa kilimo 320 wameajiriwa na kusambazwa katika hizo pamoja na vitendea kazi.
Aidha Bashe amesema, Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi imeanza kutekeleza mpango wa uanzishwaji wa vituo vya huduma za zana za kilimo (mechanization centres) katika mikoa mbalimbali nchini ili kuongeza tija katika kilimo.
“Uzalishaji wa mazao ya viwandani yanayojumuisha korosho, pamba, pareto, kahawa, tumbaku, chai, mkonge, sukari na kakao umeongezeka kutoka tani 983,177 mwaka 2021/2022 hadi tani 1,291,006.64 Desemba, 2023 sawa na ongezeko la asilimia 31.3.
Pia Bashe amesema katika mwaka 2023, mauzo ya mazao ya kilimo nje ya nchi yameongezeka kutoka Dola za Marekani 2.1 bilioni mwaka 2020/2021 hadi Dola za Marekani 2.3 bilioni sawa na ongezeko la asilimia 9.5.
Mauzo hayo yamechangiwa zaidi na mauzo ya kahawa, tumbaku, korosho, mchele, ufuta, mazao jamii ya mikunde na mazao ya bustani.
Aidha Bashe amesema Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo imeendelea kuimarisha mifumo ya masoko ya mazao kwa kutumia minada, soko la bidhaa (TMX), soko la moja kwa moja na kilimo cha mikataba katika mazao mbalimbali ikiwemo Mkonge, Kahawa, Korosho, Chai, Ufuta.
“Katika kuimarisha soko la chai nchini, Serikali imefanikiwa kuanzisha mnada wa Chai Dar es Salaam Novemba, 2023 utakaosaidia kupunguza gharama za biashara zilizokuwa zinasababishwa kwa kutumia mnada wa chai wa Mombasa,” amebainisha.
Aidha Bashe amesema huko nyuma mazao na bidhaa za kilimo zilishindwa kufikia masoko ya kimataifa kutokana na kukosekana kwa maabara za kilimo zenye ithibati zinazotambuliwa kimataifa katika upimaji wa ubora wa mazao.
“Katika kuondoa changamoto hiyo, Serikali imefanya tathmini ya uwezo wa maabara zilizopo katika taasisi 15 za Serikali na kuainisha upungufu,’’ amesema.
Hatua za kuboresha maabara nyingine zinaendelea ikiwemo maabara ya ‘tissue culture’ na udongo katika Kituo cha Utafiti wa Kilimo Mlingano mkoani Tanga.
Jingine alilosema ni ushiriki wa vijana na wanawake kwenye sekta ya kilimo kupitia Programu ya Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT)