Serikali yafafanua umiliki ardhi inakojengwa minara ya simu

Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mathew Kundo wakati akijibu swali la msingi la mbunge wa Momba, Condesta Sichalwe bungeni leo Ijumaa Aprili 8, 2022. Picha na Said Khamais
Muktasari:
Serikali imeagiza watoa huduma wote hasa wa minara kuhakikisha kuwa wanashirikisha Serikali ya Wilaya na Kijiji wanapotaka kujenga minara ya mawasiliano katika kijiji husika ili kuepuka migogoro inayoweza kujitokeza.
Dodoma. Serikali imeagiza watoa huduma wote hasa wa minara kuhakikisha kuwa wanashirikisha Serikali ya Wilaya na Kijiji wanapotaka kujenga minara ya mawasiliano katika kijiji husika ili kuepuka migogoro inayoweza kujitokeza.
Agizo lingine ni kwa watoa huduma kuhakikisha wanaingia mikataba ya ulinzi wa minara na Serikali za Vijiji ili kuwa na ulinzi wa uhakika katika minara ya mawasiliano inayojengwa huko.
Agizo hilo limetolewa bungeni leo Ijumaa Aprili 8, 2022 na Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mathew Kundo wakati akijibu swali la msingi la mbunge wa Momba, Condesta Sichalwe.
Sichalwe ameuliza ni lini Serikali itatatua migogoro ya mikataba ya minara ya simu kati ya kampuni za simu na Kijiji cha Namchinka, Kata ya Kapele ambako kumekua na sintofahamu ya kuhusu malipo.
Naibu Waziri amesema katika Kijiji cha Namchinka kina minara miwili iliyojengwa na Kampuni za Tigo na Halotel lakini minara hiyo imesimikwa katika ardhi inayomilikiwa na watu binafsi na sio kijiji.
Amsema watoa huduma hulipa malipo ya pango la ardhi kwa wamiliki hao kulingana na makubaliano kati ya watoa huduma na wamiliki wa ardhi hiyo.
Naibu Waziri amesema ni vema wananchi kuwa wazalendo na kutoa ushirikiano kwa watoa huduma wakati wa ujenzi na ulinzi wa miundombinu ya mawasiliano ili kuhakikisha huduma za mawasiliano zinakuwa endelevu kwenye maeneo yao.