Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Serikali yaandaa mkakati wa pensheni za wanajeshi wastaafu, wanafunzi wa JKT

Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Stergomena Tax  akijibu maswali ya wabunge katika kikao cha 47 cha mkutano wa bunge la bajeti jijini Dodoma leo, Juni 13, 2024. Picha na Hamis Mniha

Muktasari:

  • Miongoni mwa changamoto hizo ni madai ya kuingizwa katika daftari la pensheni kwa maveterani wote licha ya baadhi yao kutokidhi vigezo kwa mujibu wa Sheria na madai kuwa pensheni ni ndogo.

Dodoma. Serikali ya Tanzania inaandaa mapendekezo ya maboresho ya Sheria ya Pensheni na Viinua Mgongo ya Mwaka 1966 ili kukabiliana na changamoto mbalimbali za wanajeshi wastaafu waliopigana vita ikiwemo madai ya pensheni ni ndogo.

Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Stergomena Tax ameyasema hayo leo Alhamisi Juni 13, 2024 wakati akijibu swali la msingi la Mbunge wa Ndanda, Cecil Mwambe aliyehoji ni lini wanajeshi wastaafu waliopigana vita vya Kagera watalipwa mafao yao.

Akijibu swali hilo, Dk Tax amesema wanajeshi wote wastaafu waliopigana vita vya Kagera na waliostahili malipo ya viinua mgongo na pensheni walikwishalipwa.

Amesema pia wanajeshi hao, wengine wanaendelea kulipwa kwa mujibu wa Sheria ya Pensheni na Viinua Mgongo ya Mwaka 1966 ikiwemo malipo ya ulemavu na kustaafu.

Dk Tax amesema wizara imekuwa ikikabiliana na changamoto mbalimbali kuhusiana na maveterani wa vita ya Kagera.

Amesema miongoni mwa changamoto hizo ni madai ya kuingizwa katika daftari la Pensheni kwa maveterani wote licha ya baadhi yao kutokidhi vigezo kwa mujibu wa Sheria na madai kuwa pensheni ni ndogo.

“Ili kukabiliana na changamoto hizo, wizara inaandaa mapendekezo ya maboresho ya Sheria ya Pensheni na Viinua Mgongo ya mwaka 1966,” amesema.

Katika swali la nyongeza, Mbunge wa Hai, (CCM), Saasisha Mafue ametaka kujua ni lini Serikali itaileta sheria hiyo bungeni ili ifanyiwe maboresho maana wanajeshi wastaafu wanapata shida mitaani.

Pia, amehoji Serikali haioni ni wakati muafaka wa kuandaa orodha ya waliopigana vita waliolipwa na amabo hawajalipwa ili watu hao waache kuhangaika huko mitaani kudai stahiki zao.

Akijibu swali hilo, Dk Tax amesema maveterani wote waliokuwa wanastahili kulipwa walilipwa na hakuna anayedai na kuwa orodha yao ipo kwasababu inatumiwa katika shughuli mbalimbali.

Amesema katika siku za hivi karibuni waliwaomba wanajeshi hao wastaafu kuhakiki kama wamo katika orodha hiyo.

Amesema maboresho hayo yatapelekwa bungeni katika mwaka ujao wa fedha baada ya kukamilika michakato ya ndani.

Mbunge wa Viti Maalum, Esther Matiko ametaka kujua ni lini wanalipa mafao ya watumishi.

Akijibu swali hilo, Dk Tax amesema kwa sasa hakuna malimbikizo hayo kwa sababu wameendelea kulipwa na wanafanya uhakiki endapo kama yapo malimbikizo basi yatalipwa kulingana na utaratibu.

Mbunge wa Kinondoni, (CCM), Abbas Tarimba amesema Serikali haioni haja ya kushusha orodha ya wanajeshi wastaafu waliopigana vita na wengine waliopo katika daftari la pensheni kwenye ngazi ya wakuu wa wilaya ili wanajeshi hao waweze kujitambua maana wanapata tabu majina yao yaliko.

Akijibu swali hilo, Dk Tax amesema katika uhakiki unaoendelea mavetarani wote waliombwa kufika wilayani na kwamba wataendelea na zoezi hilo.

Amesema iwapo kuna veterani ambaye anaona anashindwa kupata haki yake anaweza kuwasiliana nao wakati wowote wizarani ama kambi yoyote iliyoko karibu naye neo lake na atahudumiwa ipasavyo.

Mbunge wa Kawe (CCM), Askofu Josephat Gwajima amesema Jimbo la Kawe lina wanajeshi wengi wastaafu ambao ni wapiga kura wake.

“Mheshimiwa waziri ulishakuja kuwaona, wakakwambia shida zao, wanakuomba tena kama itakupendeza unaweza kufanya nao tena kikao wakwambie shida zao,” amesema.

Akijibu swali hilo, Dk Tax amesema wameweka utaratibu ambao wataona ni jinsi gani na siyo kwenda tu kwenye jimbo la Kawe lakini kuweza kupata mahitaji, ushauri na changamoto wastaafu wao.

“Utaratibu huo ukikamilika, tutaanza kuutekeleza,” amesema.

Mbunge wa Iringa Mjini, (CCM), Jesca Msambatavangu ametaka kujua kauli ya Serikali kwa wale wote wanafunzi waliomaliza kidato cha sita kuripoti katika kambi za JKT.

Akijibu swali hilo, Dk Tax amesema ni nia na dhamira ya Serikali kuhakikisha vijana wote wanaweza kuchukuliwa kwa sababu madhumuni ni kuwajengea uzalendo, umahiri, uhodari na kuwa walinzi wa Taifa.

“Kwa sasa tunafanya tathmini ya mahitaji ya kuchukua na imefikia mbali. Hatutaweza kuchukua wote kwa wakati mmoja na mpango tunaokuja nao ni kuiona jinsi gani tukaboresha miundombinu na bajeti ili kuwachukua kwa awamu na kwa sasa utakuwa mpango wa miaka mitano mpaka 10 lakini hatujaukamilisha,” amesema.