Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Serikali yaahidi kuendelea kuwekeza katika maendeleo ya miji

Mwonekano wa Jiji la Dodoma. Picha na Mtandao

Muktasari:

  • Serikali itaendelea kutumia takwimu hizo kupanga na kutekeleza miradi ya maendeleo ya miji kwa lengo la kuboresha maisha ya wananchi na kuhakikisha ukuaji wa miji unakuwa endelevu.

Dar es Salaam. Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imesema itaendelea kusimamia ukuaji wa miji nchini kwa kutenga fedha za kuboresha miundombinu na huduma za jamii, sambamba na kushirikiana na wadau mbalimbali katika kujenga miji ya kisasa na endelevu.

Kauli hiyo imetolewa jana Julai 21, 2026,  na Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Sospeter Mtwale wakati wa kikao cha 80 cha Umoja wa Mataifa kuhusu mapitio ya ajenda mpya ya miji kilichofanyika katika Makao makuu ya Umoja wa Mataifa, New York, Marekani.

Akizungumza katika kikao hicho, Mtwale amesema Serikali itaendelea kuongeza uwekezaji katika maendeleo ya miji ili kukidhi ongezeko la watu na kuboresha utoaji wa huduma muhimu kwa wananchi.

Amesema pamoja na fedha za Serikali, juhudi zinaendelea kufanyika kushirikiana na wadau wa maendeleo ili kupata rasilimali za kugharamia miradi ya ujenzi wa miji ya kisasa na kuimarisha huduma za kijamii.

Katika kikao hicho, Mtwale pia amewasilisha hatua zinazochukuliwa na Tanzania kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, majanga na uchafuzi wa mazingira katika maeneo ya mijini.

“Serikali inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya kuboresha miundombinu ya miji ili kupunguza athari za mafuriko na majanga mengine yanayotokana na mabadiliko ya tabianchi,” amesema.

Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Sospeter Mtwale

Akitolea mfano, Ntwale amesema uboreshaji wa Bonde la Msimbazi kupitia Mradi wa Uendelezaji wa Jiji la Dar es Salaam (Dar es Salaam Metropolitan Development Project-DMDP) ni miongoni mwa hatua zinazolenga kuongeza ustahimilivu wa miji dhidi ya mafuriko na kuboresha mazingira ya makazi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Miundombinu kutoka Tamisemi, Gilbert Mwoga, amesema kikao hicho kimejadili namna ya kuongeza kasi ya utekelezaji wa ajenda mpya ya miji kwa kuhimiza ujenzi wa miji endelevu, kuboresha makazi ya mijini na kupanga maendeleo ya miji mipya.

Amesema Tamisemi inaendelea kuboresha miundombinu ya mijini kupitia ujenzi na ukarabati wa barabara, masoko, vituo vya mabasi na majengo mengine ya huduma za jamii.

"Utekelezaji wa miradi hii unafanyika kupitia Mradi wa Uendelezaji wa Jiji la Dar es Salaam (DMDP), Mradi wa Tactic pamoja na bajeti ya Serikali Kuu. Miradi hiyo inatekelezwa katika manispaa nne za Mkoa wa Dar es Salaam, Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, pamoja na majiji matano, manispaa 18 na miji 12 inayonufaika na Mradi wa TACTIC," amesema Mwoga.

Ameongeza kuwa upangaji na uendelezaji wa miji unazingatia takwimu za Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), hususan kasi ya ongezeko la watu na mahitaji ya huduma za msingi, ili kuhakikisha uwekezaji unaendana na ukuaji wa maeneo ya mijini.

Amesema Serikali itaendelea kutumia takwimu hizo kupanga na kutekeleza miradi ya maendeleo ya miji kwa lengo la kuboresha maisha ya wananchi na kuhakikisha ukuaji wa miji unakuwa endelevu.