Serikali ya Tanzania yapunguza gharama upimaji corona

Muktasari:
Serikali ya Tanzania imeshusha gharama za upimaji wa ugonjwa wa Covid-19 kwa wasafiri nchini kutoka Dola za Marekani 100 hadi 50 kwa kipimo cha RT PCR.
Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imeshusha gharama za upimaji wa ugonjwa wa Covid-19 kwa wasafiri nchini kutoka Dola za Marekani 100 hadi 50 kwa kipimo cha RT PCR.
Pia imeshusha gharama kwa kipimo cha Antigen Rapid Test kutoka Dola 25 hadi 10 kwa wasafiri wote wanaoingia nchini na kuondoa kipimo hicho mipakani isipokuwa katika viwanja vya ndege.
Taarifa iliyotolewa leo Jumatano Agosti 11, 2021 na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Doroth Gwajima imeeleza huduma hiyo itaanza rasmi Agosti 16, mwaka huu.
“Sababu ya kushusha gharama ya vipimo hivi inatokana na gharama za uendeshaji kutengwa na Serikali kupitia bajeti yake ya mwaka 2021/2022,” amesema Dk Gwajima.
Amesema hatua hiyo imetokana na agizo lililotolewa Mei 4 na Rais Samia Suluhu Hassan alipofanya ziara ya kikazi Kenya na kutoa maelekezo ya kutatua vibali na upimaji Covid-19 kwa wasafiri wanaovuka mipaka ya Tanzania na Kenya na kuagiza mawaziri wa nchi hizo kutatua kero hiyo.
“Kupitia agizo hilo, wizara tumepitia upya gharama za upimaji Covid19 na kuangalia namna ya kupunguza, ili wasafiri wote waweze kupata huduma hii muhimu,” amesema Waziri Gwajima.