Serikali, TLS wakubaliana mambo saba

Wakili wa Mkuu wa Serikali, Dk Ally Possi (kulia) akimkabizi jarida la ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Boniface Mwabukusi, baada ya kumaliza kikao chao,Jijini Dar es Salaam. Picha na Michael Matemanga
Muktasari:
- Wakili Mkuu wa Serikali, Dk Ally Possi asema taaluma ya sheria itatumika kusimamia mikataba na masuala ya uwekezaji.
Dar es Salaam. Serikali imekubaliana kushirikiana na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) na Chama cha Mawakili wa Serikali (PBA) katika maeneo saba, yakiwamo ya uandaaji wa mikataba ya uwekezaji.
Maeneo mengine ni kuendeleza maadili ya mawakili, kufanya kazi kwa karibu na Mahakama, kutatua migogoro nje ya Mahakama, kutumia fursa zilizopo katika utengemano, namna bora ya kuisaidia Serikali kwa kutoa ushauri utakaosaidai nchi, na kusaidia sekta binafsi katika masuala ya kodi, bima ya afya, mikataba na kukuza taaluma ya wanasheria.
Hayo yamesemwa leo Jumatano Septemba 25, 2024 na Wakili Mkuu wa Serikali, Dk Ally Possi alipozungumza na waandishi wa habari baada ya viongozi wa TLS na PBA kutembelea ofisini kwake kwa lengo la kuimarisha ushirikiano.
Amesema wameona haja ya vyama hivyo kushirikiana kutokana na shughuli wanazofanya za kusaidia wananchi.
Dk Possi amesema maeneo hayo wameyaweka katika hati ya ushirikiano ambayo imeshaandaliwa na inapitia utaratibu wa kiserikali kabla ya kusainiwa.
Amesema suala la taaluma limepewa kipaumbele kwenye hati hiyo kwa kuwa dunia imebadilika na kuna uwekezaji wa kimataifa unaofanyika kwa wawekezaji wageni kuja Tanzania na Watanzania kwenda nje ya nchi kuwekeza.
Amesema ipo fursa kwa wanasheria kufanya kazi na wawekezaji wa kimataifa wanaoingia nchini kuwekeza, badala ya wawekezaji hao kutumia wanasheria wa kigeni.
"Tuna wanasheria Watanzania, tunavyo vyuo vinavyotoa taaluma ya sheria vizuri, hivyo tunataka kukuza taaluma ya wanasheria watumie fursa hizi kwa kufanya kazi na wawekezaji wa kimataifa na si mwekezaji anakuja na mwanasheria wake kutoka nje," amesema.
Amesema wataendeleza maadili ya wanasheria kwa kuwa ni jambo endelevu kwa kuwapatia mbinu za namna ya kujiepusha na masuala yanayohujumu uchumi wa nchi kama vile utakatishaji fedha.
Dk Possi amesema wanasheria wanapaswa kujua uandishi wa mikataba na mambo yanayosababisha kuwepo kwa masuala ya uhujumu uchumi, ili kuepukana nayo na kusimamia maadili.
"Eneo lingine tutakalofanyia kazi kwa karibu ni Mahakama, kwa kutatua migogoro nje ya Mahakama. Hii itasaidia kupunguza mlundikano wa kesi mahakamani na kupunguza gharama," amesema.
Amesema Tanzania si kijiji, kwani imejiunga na jumuiya mbalimbali za kimataifa zikiwamo za Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), hivyo wanasheria waliopo waone fursa zilizopo kwenye utengamano, badala ya kuacha mawakili kutoka nje kufanya kazi hizo nchini.
"Mawakili binafsi wana mchango mkubwa kwa maendeleo ya nchi, hivyo basi tutaweka namna bora ya kuishauri Serikali na mawakili wa Serikali wawasaidie sekta binafsi kwenye masuala ya kuandika mikataba ya kodi, gesi, mafuta na uandishi wa sheria," amesema.
Dk Possi amesema anaamini TLS itawasaidia hata katika masuala ya bima ya afya, utetezi katika kesi za mirathi na ardhi, hivyo kusaidia wananchi kupata huduma bora.
Awali, rais wa TLS, Boniface Mwabukusi amesema mazungumzo yalilenga kutumia taaluma yao ya uwakili kuisaidia Serikali kwa masilahi ya Taifa, hususan eneo la uwekezaji na kuhakikisha vyama hivyo vinakuwa na faida na tija.
Amesema watashirikiana katika kuongeza uzoefu na kutekeleza majukumu yao kwa namna ambayo italeta tija kiuchumi, kijamii na kisiasa nchini.
"Tumezungumza kuhusu kusaini hati ya makubaliano kati ya TLS na PBA, namna ya kuhusiana, kufanya shughuli zetu na kushirikishana uzoefu katika shughuli mbalimbali," amesema.
"Tumeweka mikakati ya pamoja ya kushirikiana kwa namna ya kujenga na si kukosoa na kuzipa nguvu sheria zetu katika kutatua migogoro inayotokana na uwekezaji," amesema.
Mwabukusi amesema watashirikiana kujenga na kusimamia sheria za ulinzi wa rasilimali za nchi pia katika kumiliki na kuendeleza rasilimali hizo.
"Kuna sheria zinatupa wajibu kuona tija ya kutungwa kwa sheria za ulinzi wa rasilimali, hivyo kama wanasheria tuna wajibu wa kulinda kwa masilahi ya Taifa," amesema.
Mwabukusi amesema watashauri Serikali kuhusu utatuzi wa migogoro ya uwekezaji badala ya kwenda kutatuliwa nje ya nchi, utatuzi ufanyike nchini.
"Nia yetu uwepo wa TLS na PBA iwe daraja la kuhakikisha shughuli za uwekezaji zinanufaisha Taifa, wananchi na wawekezaji na kulinda rasilimali hizo kwa masilahi ya kizazi kijacho," amesema.
Rais wa PBA, Amedeus Shayo amesema watashirikiana katika michakato yote ya mikataba, ili kuongeza uwekezaji na usimamizi wa rasilimali za Taifa.