Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Serikali: Miradi ya kimkakati itaendelea kutekelezwa

Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa akitoa maelekezo baada ya kukagua moja ya miradi uliyo chini ya wizara hiyo wakati wa ziara yake mkoani Mara.

Muktasari:

Serikali imesisitiza kuwa utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati utaendelea kama ilivyopangwa licha ya hofu ya kiuchumi inayoikumba dunia kutokana na kupanda kwa thamani na kuadimika kwa Dola za Kimarekani kulinganisha na fedha za ndani.

Musoma. Serikali imesisitiza kuwa utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati utaendelea kama ilivyopangwa licha ya hofu ya kiuchumi inayoikumba dunia kutokana na kupanda kwa thamani na kuadimika kwa Dola za Kimarekani kulinganisha na fedha za ndani.

Msimamo huo umetolewa mjini Musoma na Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa akijibu swali kuhusu hofu ya kuongezeka kwa gharama za utekelezaji wa miradi ya kimkakati kutokana na dola siyo tu kuongezeka thamani, bali pia kupungua kwenye mzunguko.

"Kuna mambo mengine hayahitaji hata kutumia misuli….tayari hii miradi ipo kwenye utekelezaji na itaendelea kutekelezwa kadri fedha inavyopatikana," amejibu Waziri Bashungwa

Baadhi ya miradi mikubwa ya kimkakati inayotekelezwa inayohofiwa kuathirika kwa ama gharama kuongezeka au kusuasua ni ujenzi wa Bwawa la kufua umeme la Mwalimu Nyerere, Daraja la JPM maarufu kama Kigongo-Busisi, Reli ya kisasa (SGR) na miundombinu ya barabara katika mikoa mbalimbali nchini.

Waziri Bashungwa amesisitiza kuwa Serikali ina uhakika utekelezaji wa miradi yote kuendelea kama ilivyopangwa kadri fedha zinazvyopatikana.

Mchumi atoa ushauri

Akizungumzia hofu ya ongezeko la gharama na kusuasua kwa miradi ya kimkakati, Mkurugenzi wa taasisi ya Uongozi na Ujasiriamali, Dk Donat Olomi ameshauri mambo matatu yafanyike kuhakikisha miradi hiyo siyo tu haikwami, bali pia gharama zake haziongezeki.

‘’Kwanza Serikali inaweza kupunguza kasi ya utekelezaji kwa kukubaliana na mkandarasi kuondoa wafanyakazi na mitambo yake kutoka eneo la miradi hadi fedha zitakazopatikana….wakiendelea kukaa site bila kazi wataendelea kulipwa gharama ya wao kukaa bila kufanya kazi,’’ amesema Dk Olomi

Msomi huyo ambaye ni mchumi kitaaluma ametaja njia nyingine kuwa ni kuchukua mikopo nafuu ya muda mrefu kutoka kwa wadau wa maendeleo ikiwemo Benki ya Dunia (WB) na Benki ya Maendeleo Africa (AfDB).

‘’Serikali pia inaweza kuchukua mikopo ya kibiashara yenye riba kubwa na ya muda mfupi, Hii njia siyo nzuri wala salama kwa sababu inaongeza mzigo mkubwa wa madeni kwa Taifa,’’ anasema Dk Olomi

Njia nyingine ambayo hata hivyo anasema ni ya muda mrefu ni kugeukia matumizi ya gesi kupunguza gharama ya kutumia fedha za kigeni kuagiza bidhaa ya mafuta kutoka nje.

Kuongeza uzalishaji wa ndani wa mafuta ya kula ni eneo lingine ambalo msomi huyo anasema inaweza kutumika kupata fedha za kigeni kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati kwa sababu Serikali itapunguza zaidi ya Sh400 bilioni zinazotumika kuagiza mafuta ya kula kutoka nje.

Kwa mwaka, Tanzania inahitaji tani 650, 000 ya mafuta ya kula lakini uwezo wa uzalishaji nchini ni tani 290, 000 pekee, sawa na asilimia 44.6 ya mahitaji.

Kutokana na upungufu huo wa karibia asilimia 55.4, Tanzania hutumia zaidi ya Sh470 bilioni kuagiza tani 360, 000 za mafuta kutoka nje kila mwaka.