Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Serikali kununua ndege kuwamaliza wadudu waharibifu

Naibu Waziri wa Kilimo, Anthony Mavunde (watatu kushoto) akikata utepe kuzindua mradi wa zana za kilimo za chama cha ushirika cha msingi cha wakulima wanawake wa Dodoma mjini (Chawauwawado) kwenye shamba lao lililopo Kijiji cha Narakauo Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara.Picha na Joseph Lyimo

Muktasari:

Serikali imesema ina mpango wa kununua ndege mpya na kuifanyia matengenezo nyingine moja kwa lengo la kukabiliana na wadudu waharibifu wa mazao ya wakulima.

Simanjiro. Serikali imesema ina mpango wa kununua ndege mpya na kuifanyia matengenezo nyingine moja kwa lengo la kukabiliana na wadudu waharibifu wa mazao ya wakulima.

Naibu Waziri wa Kilimo, Anthony Mavunde ameyasema hayo alipotembelea shamba la soya na kukabidhi zana za kilimo za chama cha ushirika cha msingi cha wakulima wanawake wa Dodoma Mjini (Chauwawado) katika kijiji cha Narakauo, kata ya Loiborsiret, wilayani Simanjiro, mkoani Manyara.

Amesema ameisikia changamoto kubwa ya uharibifu wa mazao kutokana na wadudu wasumbufu, wamejipanga kuimarisha kilimo kwa kununua ndege mpya ya kunyunyiza na kuifanyia matengenezo moja iliyopo ili iwasaidie wakulima wa nchi kutopata hasara ya uharibifu wa mazao unaofanywa na wadudu waharibifu.

"Tunamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa utashi wake wa kuikuza sekta ya kilimo, hivi sasa bajeti ya kilimo imeongezeka kutoka sh294 bilioni hadi Sh751 bilioni, haya ni mapinduzi makubwa sana kwenye sekta ya kilimo," amesema.

Amesema amefurahishwa na namna wanawake, wametoka Dodoma na kwenda kufanya kilimo kijiji cha Narakauo, wilayani Simanjiro kwani wameonesha udhubutu mkubwa.

"Nawapongeza sana kwani mmeonesha kwa vitendo namna mnavyounga mkono juhudi za Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan," amesema Mavunde.

Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro, Dk Suleiman Serera amemuhakikishia Mavunde kuwa atahakikisha Chauwawado wanapata ardhi na kuahidi kuendelea kuwasaidia ili waendelee kuzalisha kwa tija na hatimaye kukuza uchumi wa wananchi.

"Mafanikio ya kikundi hiki itakuwa mafanikio makubwa kwa wananchi wa kijiji cha Narakauo na wilaya ya Simanjiro kwa ujumla," amesema Dk Serera.

Mwenyekiti wa Chauwawado, Winifrida Kario amesema wamelima ekari 160 za soya, ambazo wameingia mkataba wa masoko na kampuni ya Dar Lyon.

"Tuna malengo ya kuendelea kuongeza eneo la kulima mwaka hadi mwaka ila moja ya changamoto kubwa ni chama chetu kukosa ardhi, hali inayotufanya kukodi eneo la kuendesha shughuli za kilimo," amesema.

Zana za kilimo ambazo Chauwawado wamezizindua zimetokana na mkopo kutoka benki ya maendeleo ya Kilimo (TADB) zana hizo ni trekta, jembe la kusawazishia, mashine ya kupanga na jembe la kulimia.