Serikali kuikagua mifumo ya mitihani vyuo vikuu

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda (kulia) akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, kuhusu malalamiko ya usimamizi mbaya wa mitihani katika vyuo vikuu nchini. Kushoto ni Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), Profesa Charles Kihampa. Picha na Sunday George
Muktasari:
- Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imeanza kutafuta ufumbuzi wa mtandao wa watu wanaocheza na mifumo ya mitihani na matokeo ya vyuo vikuu kwa kubadilisha ufaulu wa wanafunzi.
Dar es Salaam. Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imeanza kutafuta ufumbuzi wa mtandao wa watu wanaocheza na mifumo ya mitihani na matokeo ya vyuo vikuu kwa kubadilisha ufaulu wa wanafunzi.
Wizara hiyo kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) inakusudia kufanya uhakiki wa mifumo ya utoaji matokeo ya vyuo vikuu kuona kama ina uwezekano wa alama kubadilishwa kuruhusu wanafunzi kuhitimu au kufaulu.
Hatua hiyo imekuja ikiwa ni siku chache baada ya gazeti The Citizen kuchapisha taarifa ya uchunguzi iliyoeleza namna rushwa inavyotumika kuwezesha watu kuingilia mifumo wa matokeo na kuyabadilisha kwa lengo la kuwapatia waliofeli alama zinazowawezesha kutunukiwa shahada.
Kwa mujibu wa habari hiyo, mtandao huo unahusisha baadhi ya wahadhiri na watalaamu wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), wanaoshughulika na mifumo hiyo, ambao ndiyo watu wa mwisho wa vyuo wenye jukumu la kuingiza matokeo ya mwisho kabla ya kuchapwa.
Leo Ijumaa, Julai 12, 2024, akizungumza hilo jijini Dar es Salaam, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amesema licha ya kuwa na uhakika wa mifumo ya mitihani ya vyuo vikuu haitoi mwanya wa kufanyika kwa udanganyifu wa aina hiyo, lazima uhakiki huo ufanyike kubaini kama kuna sehemu inayoruhusu uovu huo kufanyika.
“Tumezisoma tuhuma hizi kwenye gazeti kwamba kuna wanafunzi wanahonga ili matokeo yakishaingizwa kwenye mfumo wa Tehama yabadilishwe. Kuliwahi kutokea tuhuma kama hii katika chuo kimoja, lilitajwa jina la mwanafunzi na mtu aliyehusika kubadilisha hayo matokeo.
“Nilimwagiza Katibu Mkuu auende tume huru ya uchunguzi ikiwa ni pamoja na Idara ya Usalama wa Taifa na wataalamu wa Tehama, waliingia kuangalia mfumo wote, uzuri ni kwamba ukiingia kwenye mfumo ni lazima itaonekana uliingia saa ngapi na mabadiliko yapi yamefanyika. Uchunguzi ulipokamilika iligundulika si kweli, bali kulikuwa na vita ya kimamlaka inaendelea ndani ya chuo kile, hivyo waliamua kuchafuana,” amesema.
Waziri Mkenda amesema licha ya uchunguzi huo kubaini hakuna namna mifumo inaweza kuingiliwa bila kuacha ushahidi, wizara yake imeona ipo haja ya kujiridhisha dhidi ya taarifa hizo zilizochapishwa na gazeti la The Citizen.
“Sasa tumekubaliana na katibu mkuu aiandikie TCRA wachukue chuo kile kama sampuli kwa sababu ya tuhuma tulizosoma kwenye gazeti, kwenda kufanya uhakiki wa kimfumo kwa matokeo yote, ambayo yameingizwa kwenye Tehama na kuangalia matokeo yanapoingizwa na kubadilishwa nani anabadilisha.”
“Kwa utaratibu, mhadhiri anapomaliza kusahihisha mtihani anaingiza mwenyewe kwenye mfumo, zile karatasi zinapelekwa kwa mtahini wa nje. Huyu anaweza kuwa wa chuo kingine au anayetoka nje ya nchi, ikitokea yeye ameona kuna haja ya kufanyika mabadiliko, ni lazima yaende kwenye kamati ya mitihani kabla ya kuingizwa kwenye mfumo na mkuu wa idara,” amesema.
Waziri huyo amesema: “Baada ya hapo yanaingia kwenye ngazi ya kitivo yanajadiliwa kisha yanaenda kwenye seneti ndipo yanatoka. Hatua zote hizi za kugusa matokeo zinaacha alama, huwezi kufuta alama, lakini tutafanya uhakiki ili kuuhakikishia umma kuwa hatutaki mtu acheze na mitihani yetu, hivyo lazima tujiridhishe.
“Niwahakikishie kuwa bado vyuo vyetu vikuu vinazingatia maadili na weledi, hasa katika eneo la mitihani.”
Akizungumzia hatua hiyo, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Dk Paul Loisulie amesema licha ya udhibiti mkubwa uliopo kwenye mifumo, hiyo haiondoi ukweli kuwa wapo wanaoiingilia.
“Kuna udhibiti mkubwa kwenye hii mifumo lakini kwa kuwa imetengenezwa na watu na inasimamiwa na watu, wapo watu wasio na uadilifu wanaweza kuiingilia, hivyo muhimu ni kuzidi kuilinda,” amesema Dk Loisulie
Hilo lilielezwa pia na mtaalamu wa Tehama ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini akisema: “Hakuna kitu kinachoshindikana kwa sababu mifumo imetengenezwa na binadamu, haohao wanaweza kuingia kinachofanyika katika hali kama hiyo ni kuilinda, ndiyo maana kuna programu za kulinda mifumo nafikiri vyuo viwekeze zaidi eneo hilo.”
Matukio ya udanganyifu vyuo vikuu yameanza kuonekana wazi na hivi karibuni na walikamatwa watu 17 walioghushi vitambulisho na tiketi ya kuingia kwenye ukumbi wa mtihani wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT).
Kwa mujibu wa Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa Elifas Bisanda, watu hao waliokamatwa hawakuwa wanafunzi wa chuo hicho ila kitendo cha kughushi vitambulisho na tiketi ya kuingia ukumbi wa mtihani ni wazi kulikuwa na udanganyifu.
Hata hivyo, baada ya watuhumiwa hao kuhojiwa na Jeshi la Polisi ilibainika walighushi vitambulisho hivyo ili kuingia kwenye chumba cha mtihani kuwafanyia wanafunzi wanaowalipa kati ya Sh30,000 hadi Sh50, 000 kwa somo.
Akizungumzia sakata hilo la OUT, Profesa Mkenda amesema: “Kilichofanyika OUT kuwagundua watu wanaojaribu kuwafanyia wengine mitihani ni kati ya jitihada ambazo tunaendelea nazo kudhibiti mianya ya udanganyifu kwenye elimu. Majaribio ya udanganyifu yapo dunia nzima ila sisi tutaendelea kupambana kuyazuia.”