Udanganyifu wa mitihani shuleni, vyuoni uko hivi

Zungumza na mdau yeyote wa elimu, soma andiko lolote kuhusu mifumo ya mitihani Tanzania kwa ngazi zote za elimu, mojawapo ya changamoto utakayokumbana nayo ni udanganyifu au wizi wa mitihani.

Ni changamoto kongwe, yenye sura nyingi ndani yake,ambayo hata hivyo mamlaka husika hazijabweteka katika kutafutia mwarobaini wake.

Katikati ya harakati hizo za kuzua udanganyifu huo, bado uzoefu unaonyesha kuwapo kwa matukio na vitendo vinavyoashiria kuwa hali si shwari sana katika udhibiti wa udanganyifu na wizi wa mitihani.

Ni ukweli unaochagizwa na tukio la hivi karibuni la Waziri wa Elimu, Profesa Adolf Mkenda kuifungia kwa muda shule ya msingi Chalinze Islamic kuwa kituo cha mitihani.

Ni uamuzi uliotokana na tuhuma alizozitoa mwanafunzi wa shule hiyo iliyopo mkoani Pwani, Iptisum Slim aliyedai kubadilishiwa namba yake ya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi uliofanyika mwanzoni mwa Oktoba.

Tukio hilo likazua mjadala mkubwa katika vyombo vya habari na hata mitandao ya kijamii. Sehemu ya mjadala hiyo ilikuwa hoja kuwa kilichotokea shuleni hapo pengine ni aina mojawapo ya mbinu za udanganyifu zinazotumika katika shule nyingi nchini.

Si tukio la kufungiwa kwa shule hiyo pekee, lakini hivi karibuni jamii imeshuhudia watu 10 wakiwamo walimu saba wakipandishwa kizimbani kwa tuhuma ya kusambaza mitihani ya Taifa ya darasa la saba kwa kutumia mitandao ya kijamii.

Ilidaiwa mahakamani kuwa kati ya Oktoba 2 na 12, 2022, sehemu isiyojulikana jijini Dar es Salaam kupitia mitandao ya kijamii ukiwamo wa telegram, watuhumiwa walisambaza mitihani na kusababisha kuvuja kwa mitihani ya Taifa ya darasa la saba.


Sababu ya udanganyifu

Kuna mambo kadhaa yanayochangia udanganyifu au wizi wa mitihani kuanzia ngazi ya shule za msingi, sekondari na hata vyuoni.

Moja ya sababu ambazo Mwananchi limebaini ni msisitizo wa kuufanya mtihani kuwa ndio kigezo pekee cha kuamua hatima ya mwanafunzi kuendelea na masomo ya juu na hata kupata kazi. Hii ni moja ya sababu kubwa zinazofanya wizi au ulaghai kwenye mitihani uendelee.

‘’ Bado Taifa letu linatumia mitihani kama kipimo pekee cha mtu kupanda madaraja, hali hiyo ni sawa na vita ndiyo maana utaona kuanzia mwanafunzi mwenyewe, wazazi au walezi, shule na wengineo wanafanya kila wanaloweza ili kuishinda vita hiyo. Ni katika mtazamo huu, lazima kuwe na mbinu hata zile chafu za kurahisisha ushindi huo, anasema mwalimu mstaafu, Bakari Kheri.

Ni kwa sababu hiyo wadau wa wanasema elimu ya Tanzania haina mkazo kwenye kufundisha maarifa na ujuzi, bali watoto wanafundishwa kukariri masomo kwa minajili ya kufaulu mtihani pekee.

Hali hii imefanya wazazi na walimu kuhakikisha wanafunzi wanafaulu mtihani kwa njia yoyote ile ikiwamo njia zisizo halali.

Wadau wanasema kungekuwa na vigezo vingine vya kuwapima wanafunzi wetu uwezo wao, pengine kusingekuwa na vitendo hivi vya udanganyifu au vingepungua kwa kiwango kikubwa.

Sababu nyingine ni maagizo na amri kutoka kwa viongozi wa kisiasa wanaosisitiza walimu wakuu kuhakikisha watoto wanafaulu kwa njia yoyote. Aidha, baadhi ya maofisa elimu pia wamekuwa na tabia ya kuwaamuru walimu wakuu wajieleze kwa nini watoto hawajafaulu mitihani.

Kutokana na shinikizo hilo la maofisa elimu, walimu wakuu wamekuwa na woga wa kushushwa vyeo endapo hawatofaulisha katika shule zao. Hili huwafanya watumie njia zozote ikiwamo udanganyifu ili kulinda nafasi zao.

Na hili ndilo linaloweza kuwa kielelezo kwa walimu na maofisa elimu katika Halmashauri ya Wilaya ya Chemba waliobainika kufanya udanganyifu mwaka 2018, kitendo kilichosababisha shule zote za msingi kufutiwa matokeo ya mtihani wa darasa la saba.

Ushindani baina ya walimu shuleni, unatajwa kuwa kichocheo kingine, hasa katika mazingira ambayo wamiliki wa shule wanatoa zawadi kwa walimu ambao wanafunzi wao wamefanya vizuri.

Mwalimu Kheri anasema: ‘’Kwa kuwa katika baadhi ya shule kinachotolewa na wamiliki hao huwa kinajaza mifuko, baadhi ya walimu wanalazimika kuacha maadili kwa minajili ya kujipatia vitita hivyo vya fedha kutoka kwa wenye shule. Ndio utaona mwalimu yuko tayari hata kujitolea kufundisha twisheni bila malipo ili somo lake lije kufaulisha sana. Haya yapo katika shule.’’

Sababu nyingine ni elimu kugeuzwa kuwa bidhaa. Tangu kuanza kwa mfumo wa soko huria miaka ya 1990, shule nyingi zilianzishwa, sio kwa lengo la kusaidia Serikali kutoa huduma lakini kwa minajili ya kufanya biashara. Ndio maana haishangazi kuona wamiliki wa shule wakifanya kila wanaloweza kukuza ufaulu ili kutengeneza jina la shule kwa lengo la kuvutia wazazi.

Kwa mujibu wa mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Christian Bwaya, licha ya mfumo huo wa uchumi wa soko kutoa fursa ya huduma ya elimu kutolewa na watoa huduma binafsi mbali ya Serikali, kuna baadhi ya watoa huduma wanaogeuza huduma hiyo kuwa biashara.

‘’ Watoa huduma hao wanapoigeuza elimu kuwa biashara, ndipo hata mbinu chafu huanza kutumika. Ili shule hizo za kibiashara siyo za kihuduma ziweze kupata wateja wengi, itazilazimu zijikite kule wanakohitaji wateja wao.

Wateja wanahitaji ufaulu. Wanahitaji elimu ya ufaulu. Wateja wanataka kusikia alama za juu na nafasi za juu kitaifa,’’ anasema


Hatua za mitihani

Nchini Tanzania, mitihani ya Taifa kwa ngazi za elimu ya msingi na sekondari inapitia hatua kadhaa ikiwamo kuandaliwa kwa maswali, usambazaji wa mitihani shuleni, uhifadhi wa mitihani, ufanyaji wa mitihani, usafirishaji mitihani iliyosahihishwa, hatua ya usahihishaji, upangaji matokeo na kisha kutangazwa.

Wadau wanasema upo uwezekano wa kila hatua kila mchakato huo, ikawa na ina yake ya udanganyifu, japo Baraza la Mitihani Tanzania (Necta), linasema kuwa limejipanga kudhibiti udanganyifu katika mitihani.

Akizungumza hivi karibuni, Kaimu Katibu Mtendaji wa baraza hilo, Athumani Amasi alisema: “Tuko vizuri, hii ni vita, hatuwezi kusema hadharani tunafanya nini lakini tunapambana na wahusika….’’

Kwa kuwa kila hatua inaweza kukumbwa na adha hiyo, makala haya yanaangazia baadhi ya hatua na namna mitihani inavyoweza kufanyiwa udanganyifu.

Katika hatua ya uhifadhi shuleni, upo uwezekano wa baadhi ya karatasi za mitihani kuchomolewa na kusambazwa kwa wanafunzi. Mtindo huu hujulikana kwa jina la kuvuja kwa mtihani na ndio maana miaka ya nyuma, haikuwa jambo geni kuwapo kwa kile kilichojulikana kama ‘ feki’ yaani mitihani iliyokuwa ikisimbaa siku chache au saa kadhaa kabla ya mitihani.

Wakati wa ufanyaji wa mitihani, mbinu zinazotumika kama anavyosema mhadhiri wa chuo Kikuu cha Dar es Salaam Dk Faraja Kristomus ni pamoja na wanafunzi kuingia na majibu katika chumba cha mtihani maarufu kama ‘vibomu’, anavyosema huandikwa katika sehemu za mwili au vikataratasi vilivyofichwa. Majibu pia huandikwa katika makasha ya calculator.

‘’Udanganyifu mwingine ni taasisi au shule kuiba mitihani na kuwapa majibu wanafunzi wanaofanya mtihani huo, hivyo wanafunzi wanaingia katika chumba cha mtihani wakiwa na majibu tayari,’’ anasema.

Mdau wa elimu na mwalimu mstaafu, Zaida Mgala anasema udanganyifu mwingine ambao umekuwa ukiripotiwa ni walimu kuwachukua wanafunzi wengine ili wafanye mtihani kwa niaba ya walengwa.

“Udanganyifu huu ulikuwa unaripotiwa sana miaka ya nyuma,” anasema. anaeeleza.

Katika baadhi ya shule wasimamizi wa nje wamekuwa wakikirimiwa kama wageni maalumu. Huduma wanazopewa sambamba na takrima, huwajengea hisia kuwa wanapaswa kulipa fadhila.

Hivyo sia ajabu kuona wasimamizi hawa wakitumia muda mwingi nje ya vyumba vya mitihani ili kutoa mwanya kwa wanafunzi kusaidiana. Zipo taarifa kuwa baadhi ya shule huwapa milungula wasimamizi iliwatoe nafasi ya kufanyika kwa udangayifu.

Aidha, udhaifu wa mbinu za usimamizi nazo zinatajwa kuchangia udanganyifu ndani ya chumba cha mitihani.

Leopald Mwalongo katika utafiti wake uitwao: ‘Language and cheating in higher learning education examinations- a case study of The Open University of Tanzania, anashauri wasimamizi kupewa mafunzo ya namna kubaini vitendo vya wizi kwenye mitihani anavyosema hufanyika kwa mbinu za mitikisiko ya mwili.

Anasema kwa mfano mwanafunzi ambaye katika chumba cha mtihani anapepesa sana macho, hiyo ni dalili kuwa anauliza nani ana shida amsaidiea au huenda yeye mwenyewe anatafuta wa kumsadia.

Pia anasema kuna mitikisiko mingi tu inayofanywa na watahiniwa ikiashiria ama mhusika anayeombwa msaada hana jibu au anasema subiri.

Anasema mitikisiko ya kimwili inayofanywa, hutegema na mahitaji ya mwanafunzi anayetaka kufanya udanganyifu.

‘Kujua haya lazima wasimamizi wafunzwe njia za mawasiliano zinazoweza kutumika kwenye mitihani na mbinu za wizi zinazofanyika,’’ anaeleza Mwalongo.


Wizi vyuo vikuu

Vitendo vya wizi udanganyifu na wizi wa mitihani , ni suala mtambuka; ni janga kubwa katika ngazi zote za elimu nchini ikiwamo ngazi ya elimu ya juu.

Katika ripoti ya utafiti wake wa shahada ya uzamili aliouita kwa jina la; The prevalence of academic cheating in Tanzania Universities, Peter Muga, anasema katika utafiti wa vyuo sita alivyovifanyia uchunguzi, amebaini tatizo hilo kusababishwa na wahadhiri na wanafunzi, huku akivitaja vyuo navyo kuwa moja ya sababu zinazochangia hali hiyo.

Kwa wahadhiri alisema vitendo wanavyovifanya ni pamoja na kuuza mitihani, kuiba mitihani pamoja na kuvujisha kwa wanafunzi.

‘’Examination cheating committed by students include copying from other students, seeking help from fellow students during the exams, sitting closer to academically able students and hiding materials in toilets, anaandika Muga katika dokezo la utafiti huo lililowekwa katika wavuti wa maktaba ya chuo Kikuu cha Dar es Salaam (http://[email protected])

Hata hivyo, kwa vyuo vya elimu, udanganyifu mkubwa wa kitaaluma ni ule wa ubwakuzi (plagiarism), ambapo mwanafunzi anatumia au kughushi kazi za mwingine hasa katika uandishi wa tasnifu (dissertation) na tazmili (thesis)

Hata hivhyo, baahi ya vyuo kikiwamo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, vinatumia njia za kisasa kukabliana na udanganyifu huo.

“Tuna software ya ‘Turnitin’ ambayo ina uwezo wa kubaini originality (uhalisia) wa kazi za kitaaluma... na tangu tuanze kuitumia, ni lazima kazi ya mwanafunzi ipitie software hiyo, ili ijulikane kiwango cha uhalisia wa kazi kiasilimia,’’ alisema Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa William Anangisye katika mahojiano aliyofanya na gazeti dada la The Citizen mwaka 2020.


Athari za wizi wa mitihani

Athari za wanafunzi kufaulu kwa njia za ujanja ujanja ni mbaya kwa Taifa, kwa kuwa hali hiyo inatengeneza wasomi wasiojiamini na wasiokuwa na maarifa wala ujuzi ambao ungeweza kuwasaidia katika maisha yao na taifa kwa jumla.

Mbali ya kukosa ujuzi na maarifa, wanafunzi waliofaulu kwa njia haramu ndio wanaokuja kuwa wafanyakazi katika serikalini na nje ya serikali sambamba na kuwa viongozi wa kisiasa au kijamii. Si ajabu kwa mtu wa aina hii akakosa maadiili na kushindwa kufuata miiko, kwa kuwa amejengwa katika misingi mibovu tangu masomoni.

Kwa mujibu wa Bwaya, wizi wa mitihani katika mfumo wa elimu wa ngazi yoyote ile, huathiri maslahi mapana ya maendeleo ya taifa, hivyo kinapaswa kuchukuliwa kama kitendo cha kuhujumu taifa.

‘’Fikiria itakapofika wakati ambapo mataifa mengine yatakapokuwa na mashaka na wasomi wetu. Sisi wenyewe ndani ya nchi tunahudumiwa na daktari, lakini unamtazama mara mbili mbili na kujiuliza moyoni kama ana sifa,’’ anaeleza.

Aidha, anasema athari kubwa ni kupata watumishi wa kada mbalimbali ambao siyo waadilifu. Hawana maadili kwa sababu wamekulia hivyo katika mfumo huo tangu shule ya msingi.


Imeandikwa na Abeid Poyo, Mariam Mbwana na Aurea Simtowe