Sativa kuletwa Dar kwa matibabu

Edgar Mwakabela (27) maarufu kama 'Sativa' akiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Mpimbwe mkoani katavi.

Muktasari:

  • Awali ilikuwa asafirishwe kwa ndege sasa kusafiri kwa gari la kubeba wagonjwa

Dar es Salaam. Wakati wowote kuanzia sasa Edgar Mwakabela maarufu Sativa anayedaiwa kutoweka Juni 23 na kupatikana porini mkoani Katavi, atawasili Dar es Salaam kwa ajili ya matibabu.

Mwakabela alitarajiwa kuwasili Dar es Salaam saa tisa alasiri kwa ndege maalumu ya kukodi, lakini kutokana dharura iliyojitokeza, amesafirishwa kwa gari la wagonjwa akitokea mkoani Dodoma kuletwa jijini hapa.

Sativa mkazi wa Mbezi wilayani Ubungo alipatikana Alhamisi Juni 27, 2024 katika Hifadhi ya Taifa ya Katavi akiwa na majeraha mwilini, akiomba msaada wa kupelekwa hospitalini.

Baada ya kupatikana katika hifadhi, alipekelewa Kituo cha Afya Mpimbwe kisha Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Katavi.

Jana Ijumaa Juni 28, 2024 Patrick Israel, ambaye ni kaka wa Mwakabela alisema wanasubiri ripoti ya madaktari ili kujua lini watamsafirisha kumleta Dar es Salaam.

Akizungumza na wanahabari leo Jumamosi, Juni 29, 2024 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Terminal 1, Martin Masese maarufu ‘MMM’ anayeratibu matibabu na safari ya Mwakabela amesema anaendelea vyema na hali yake inazidi kuimarika ndiyo maana madaktari wametoa ruhusa asafirishwe.

Masese amesema alikuwa asafiri kwa Shirika la Ndege la Tanzania, tangu Juni 28 kutoka Katavi kupitia Tabora hadi Dar es Salaam, lakini kwa bahati mbaya usafiri huo ulishajaa.

“Tukatafuta njia nyingine ya kupata ndege kati ya Mbeya, Dodoma au Mwanza, hatukufanikiwa, lakini tukapata wasamaria wema waliotuwezesha ndege ya kusafirisha wagonjwa. Hii ilitakiwa ifike Katavi jana, lakini ikapata dharura ya kumsafirisha mgonjwa mwingine kwenda Afrika Kusini.

“Hospitali ya Katavi ikatoa rufaa ya Sativa apelekwe Dodoma ili ndege ikitoka Afrika Kusini imchukue jijini humo kuanzia saa saba mchana. Hata hivyo, tukaelezwa ndege itachelewa kwa saa tano na itafika Dodoma saa mbili usiku au saa tatu,” amesema Masese.

Kutokana na hali hiyo, Masese amesema walishauriana na ndugu wa Sativa na madaktari na kuazimia asafirishwe kwa gari la wagonjwa badala ya kusubiria ndege iliyopangwa kufika Dodoma usiku.

“Tunavyoongea hivi sasa saa tisa, Sativa yupo njiani kuja Dar es Salaam, kuanzia saa mbili au saa tatu atakanyaga mkoa huu na kupelekwa moja kwa moja katika hospitali iliyotengwa kwa matibabu yake,” amesema Masese.