Sangu aipa mbinu e-GA kuongeza ajira kwa vijana

Muktasari:
- Naibu Waziri, Deus Sangu ameitaka ameipa mbinu e-GA ili kuongeza ajira kwa vijana wabunifu katika Tehama ikiwemo kushirikiana na ili kuongeza fursa za ajira.
Dar es Salaam. Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Deus Sangu, ameitaka Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) kushirikiana zaidi na sekta binafsi ili kuongeza ajira kwa vijana wabunifu katika sekta ya teknolojia ya habari na mawasiliano (Tehama).
Akizungumza wakati wa kufunga programu ya awamu ya sita ya mafunzo kwa vitendo na mafunzo kazini kwa mwaka wa fedha 2024/2025 inayoendeshwa na e-GA kupitia Kituo cha Utafiti, Ubunifu, na Uendelezaji wa Serikali Mtandao (e-GovRIDC) jijini Dodoma, Sangu aliipongeza e-GA kwa kukuza vipaji vya vijana kwenye tehama. Alisisitiza kwamba ushirikiano wa karibu na sekta binafsi utaongeza fursa za ajira kwa vijana, huku akitoa wito kwa e-GA kutafuta njia za kuwasaidia vijana wanaoshiriki mafunzo hayo kupata fursa za ajira.
"Huu ushirikiano na sekta binafsi utaongeza tija katika kukuza tasnia ya tehama, hivyo kuongeza ajira kwa vijana na kupunguza changamoto za ajira nchini," alisema Sangu.

Sangu pia alibainisha kuwa baadhi ya taasisi binafsi, kama benki na kampuni za simu, zimeonesha nia ya kushirikiana na e-GA kupitia mikataba ya ushirikiano (MoU) katika masuala ya elimu, utafiti, na ubunifu wa teknolojia, hatua ambayo inatarajiwa kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi hizi na e-GA.
"Nimetembelea miradi mbalimbali ya e-GA na kuona jinsi wanavyowaandaa vijana wetu kukabiliana na teknolojia mpya kama akili bandia na sarafu ya kidijitali. Hii itawawezesha vijana wetu kuingia katika soko la ajira la kidijitali na kuleta ubunifu serikalini," aliongeza.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa e-GA, Benedict Ndomba, aliahidi kuimarisha ushirikiano na sekta binafsi na vyuo vikuu ili kuwajengea uwezo vijana kwenye tehama na kuwaandaa kushindana katika soko la ajira kimataifa.
Akizungumza kwa niaba ya wanafunzi, Philemon Mbunda, mwanafunzi wa mwaka wa tatu kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), alishukuru e-GA kwa kuwapa nafasi ya kushiriki programu hiyo, ambayo imewasaidia kujifunza teknolojia mpya na jinsi ya kuzitumia kubuni mifumo itakayoinufaisha taifa.
Kwa mwaka wa fedha 2024/2025, e-GA imeendesha programu ya mafunzo kwa vitendo iliyowashirikisha wanafunzi 65 kutoka vyuo vikuu 12 kwa kipindi cha wiki 10, ikiwa ni jitihada za kuwajengea uwezo wa kushindana katika soko la ajira.