Sanamu la Mwalimu Nyerere lazinduliwa Ethiopia, Rais Samia ashiriki

Muktasari:
- Sanamu limewekwa mbele ya Jengo la Siasa, Amani na Usalama la Mwalimu Julius Nyerere ikiwa ni ishara ya kutambua mchango wake katika harakati za ukombozi wa barani Afrika na kuhimiza umoja
Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan pamoja na viongozi wengine wa mataifa ya Afrika wameshiriki hafla ya uzinduzi wa sanamu la Hayati Mwalimu Julius Nyerere makao makuu ya Umoja wa Afrika (AU) huko Addis Ababa, Ethiopia.
Hafla hiyo imefanyika leo Februari 18, 2024 karibu na Jengo la Siasa, Amani na Usalama la Mwalimu Julius Nyerere, ikiwa ni kutambua mchango wa kiongozi huyo katika kupigania ukombozi wa Bara la Afrika na kuhamasisha amani na umoja.
Marais waliohudhuria shughuli hiyo ni Rais Samia, William Ruto (Kenya), Hakainde Hichilema (Zambia), Cyril Ramaphosa (Afrika Kusini), Salva Kiir (Sudan Kusini) na Joao Lourenco (Angola).
Wengini ni Rais wa Mauritania, Mohamed Ghazouani ambaye pia ni mwenyekiti wa AU, Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed na Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Moussa Faki Mahamat.
Akizungumza kwenye hafla hiyo, Rais Samia amesema sanamu la Mwalimu Nyerere ni kutambua mchango wake katika ukombozi wa Bara la Afrika na kuhimiza amani na umoja kama urithi wa kujivunia.
Rais Samia ameishukuru Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Sadc) kwa kutekeleza mradi huo na AU kwa kutoa eneo kwa ajili ya sanamu la Mwalimu Nyerere karibu na sanamu za viongozi wengine mashuhuri wa Afrika; Haile Selassie na Kwame Nkrumah.
Amesema Mwalimu Nyerere alianzisha taasisi na kutafuta rasilimali kwa ajili ya kuunga mkono harakati za ukombozi wa bara la Afrika, hata baada ya kuondoka madarakani, mchango wake katika kuhamasisha amani bado unatambuliwa.
“Kama unaishi Afrika, basi tunatakiwa kujua umoja wetu na mafanikio yetu yanategemea idadi yetu. Hakuna hata mmoja wetu anayeweza kupata mafanikio bila mafanikio ya Afrika. Ni sahihi kusema upekee wetu unaendana na kutegemeana kwetu, hivyo tunakamilisha ukombozi wa kisiasa na mabadiliko ya kiuchumi, ni muhimu kwa mustakabali wetu wa badaye,” amesema Rais Samia.
Kiongozi huyo amebainisha kwamba Eneo la Soko Huru Afrika (AfCFTA) inatakiwa kutumia nafasi ya kipekee kuhakikisha mafanikio na utu wa watu wa Afrika.
“Ni matumini yangu kwamba kumbukumbu ya mwalimu Julius nyerere itahamasisha vizazi vya sasa na vijavyo kuwasha tochi zao kwa ajili ya utu, matumaini na utu mahali ambapo hakuna,” amesema Rais Samia.
Kwa upande wake, Rais wa Zambia, Hakainde Hichilema ambaye pia ni Mwenyekiti wa Troika ya Siasa, Amani na Usalama ya Sadc, amesema wanashukuru kizazi cha wapigania uhuru waliofanya kazi na Mwalimu Nyerere katika kupigania uhuru wa bara la Afrika.
“Sanamu hili litakuwa ni ukumbusho kwetu, nchi moja moja, jumuiya za kikanda na Afrika na dunia kwa jumla kwa kazi kubwa ya kutukuka mtoto huyu wa Tanzania, mtoto wa Afrika alifanya kwa ajili yetu sote.
“Ninayo heshima sasa ya kufungua sanamu hili la mmoja wa waasisi wa Sadc pamoja na Umoja wa Afrika. Kumbukumbu za Mwalimu Julius Nyerere ziendelee kuishi. Viva Sadc, viva Umoja wa Afrika,” amesema Hichilema.
Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika, Mahamat amesema mwaka 1963 wakati wa uzinduzi wa Umoja wa Afrika, Mwalimu Nyerere alisema: “Afrika ni moja na sisi wote ni Waafrika. Umoja huu ni ishara ya Imani yetu ya kwenda pamoja.”
Amesema kujidhatiti kwake kwa ajili ya umoja wa Afrika ulikwenda mbali zaidi ya mipaka na masilahi ya Taifa lake, kama ilivyojidhihirisha kwenye maneno yake aliyoyatoa kwenye Bunge la Tanzania mwaka 1970: “Tunatakiwa kusimama na ndugu zetu kupigania uhuru Kusini mwa Afrika. Kaulimbiu zao ni kaulimbiu zetu na ushindi wao ni ushindi wetu.”
Amesema wakati wa utawala wake, Tanzania ilikuwa ni kitovu cha mapambano ya ukombozi katika Bara la Afrika. Kamati ya ukombozi kusini mwa Afrika ilikuwa na makao yake makuu Tanzania na Dar es Salaam haikuwa tu kitovu cha harakati za ukombozi Afrika bali pia Kitovu cha Harakati za Palestina (PLO) na Amerika ya Kusini.
Mahamat amesema Mwalimu Nyerere alikuwa na mchango mkubwa katika usuluhishi hasa huko Burundi.