Samia na utelekezaji miradi ya kimkakati iliyoachwa na Magufuli

Miongoni mwa vichwa vya treni ya umeme ambavyo vimepokelewa na Shirika la Reli Tanzania (TRC) kikiwa kinashushwa leo Desemba 30, 2023 katika bandari ya Dar es Salaam.
Ilikuwa siku, wiki, mwezi, mwaka na sasa imetimia miaka mitatu ya uongozi wa Samia Suluhu Hassan kama Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ndivyo unavyoweza kuichambua safari ya kiongozi huyo kama mkuu wa nchi.
Rais Samia aliapishwa Machi 19, 2021 baada ya kifo cha mtangulizi wake, hayati John Magufuli aliyefariki Machi 17, mwaka huohuo.
Matakwa ya Ibara ya 37(5) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ndiyo yalihalalisha mabadiliko hayo ya uongozi, hivyo aliyekuwa Makamu wa Rais alistahili kupokea kijiti cha urais.
“Endapo kiti cha Rais kitakuwa wazi kutokana na Rais kufariki dunia, kujiuzulu, kupoteza sifa za uchaguzi au kutomudu kazi zake kutokana na maradhi ya mwili au kushindwa kutekeleza kazi na shughuli za Rais, basi Makamu wa Rais ataapishwa na atakuwa Rais kwa muda uliobaki katika kipindi cha miaka mitano...” inaeleza ibara hiyo ya Katiba.
Ukilinganisha muda Rais Samia aliokaa madarakani na umri wa binadamu, basi ni sawa na mtoto aliyeanza kutembea. Kifo cha Dk Magufuli kilitazamwa na wengi kama ndiyo mwisho wa kila kitu alichokiasisi wakati wa utawala wake hasa miradi ya kimkakati.
Katika kipindi cha miaka mitano ya urais wa hayati Magufuli, alijikita zaidi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo hasa ujenzi wa miundombinu.
Alianzisha mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa (SGR), bwawa la kufua umeme la Julius Nyerere (JNHPP), ujenzi wa daraja la Tanzanite, daraja la Magufuli (Kigongo-Busisi), daraja la juu la Mfugale na daraja la juu la Kijazi (makutano ya barabara Ubungo).
Magufuli alifariki ikiwa tayari ameshakamilisha miradi ya daraja la Mfugale na daraja la Kijazi pale Ubungo. Hata hivyo, miradi mingine ya kimkakati kama JNHPP na SGR ilikuwa katika hatua za utekelezaji.
Hata hivyo, Rais Samia alipoingia madarakani aliweka wazi msimamo wake juu ya yote yaliyoachwa na mtangulizi wake. Alisisitiza hakuna mradi hata mmoja utasimama, yote itaendelea kujengwa kama ilivyopangwa.
Katika hotuba yake ya kwanza bungeni jijini Dodoma Aprili 22, 2021, Rais Samia alionyesha msimamo wa kuendeleza yale yaliyoanzishwa na mtangulizi wake.
“Mimi na Hayati Magufuli ni kitu kimoja, kwa maana hiyo mambo mengi ambayo Serikali ninayoiongoza imepanga kuyatekeleza ni yale ambayo yalielezwa na Hayati Magufuli wakati akilizindua Bunge hili,” alisema Rais Samia.
Hilo linathibitika na kinachoshuhudiwa sasa ambapo miradi yote iliyoanzishwa na mtangulizi wake anaendelea kuitekeleza katika uongozi wake.
Katika kurejea adhima hiyo ya kuendeleza miradi, Rais Samia juzi alizungumzia kifo cha Hayati Magufuli kupitia mitandao yake ya kijamii ikiwa ni miaka mitatu tangu kilipotokea akisema, “…miaka mitatu iliyopita tuliondokewa na aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano, Hayati Magufuli.
Tuendelee kumuombea kwa Mwenyezi Mungu ampe pumziko jema. Kama ambavyo awamu zote zimeendelea kufanya, Serikali ya Awamu ya Sita itaendelea kumuenzi Hayati Magufuli kwa kusimamia na kuyaendeleza mazuri yote aliyoyaanzisha.”
Naye Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko juzi akishiriki katika ibada ya kumbukumbu ya kumuombea hayati Magufuli iliyofanyika katika Kanisa la Parokia ya Mtakatifu Yohana Maria wa Muzeyi alisema Serikali itaendelea kuyaenzi yale yote yaliyofanywa na hayati Magufuli.
Alisema watasimamia uwajibikaji kwa kuondoa uzembe, kusikiliza kero za wananchi na kuzitatua pamoja kuondoa ubadhirifu ili kile Watanzania walichokitazamia waweze kukipata.
Alisema Serikali inaendelea kumkumbuka Dk Magufuli sio tu kama Rais wa Tanzania bali kama kiongozi aliyeweka misingi ambayo awamu ya sita inaendelea kutekeleza.
“Miradi mbalimbali ambayo Magufuli aliibuni kama ujenzi wa bwawa la Julius Nyerere na ndoto ya kuwaunganisha Watanzania kwa reli ya kisasa, Rais Samia ameendeleza ndoto hiyo na ujenzi wa kipande cha reli kutoka Dar es Salaam majaribio yamefanyika.
“Kwa watu wa kanda ya Ziwa mikoa ya Geita na Mwanza, ilikua inamkera sana kuona wakichukua muda mrefu kwenye kivuko cha Busisi, akaamua uanzishwe ujenzi wa daraja ambalo sasa limefika zaidi ya asilimia 80. Rais aliposema kazi iendelee alikusudia kuendeleza maono aliyokuwa nayo Rais Magufuli,” alisema Biteko.
Hayati Magufuli alifariki dunia katika kipindi ambacho utekelezaji wa mradi wa JNHPP ukiwa umefikia asilimia 33.
Katika kipindi hicho, hakukuwa na aliyeamini kama kutakuwa na mwendelezo wa utekelezaji na ndipo matumaini ya kupatikana kwa nishati ya umeme wa uhakika yaliyeyuka vichwani mwa Watanzania.
Hata hivyo, Rais Samia ndani ya miaka mitatu ya uongozi wake, mradi huo uliendelea kujengwa hadi sasa umefikia asilimia 97.
Hadi hivi tunavyoadhimisha miaka mitatu ya Rais Samia, tayari Watanzania wameanza kunufaika na mradi huo, baada ya mmoja kati ya mitambo tisa imewashwa na kuanza kuingiza umeme katiia gridi ya taifa.
Pamoja na mtambo huo unaoingiza megawati 235 katika gridi ya taifa, mtambo mwingine namba nane unatarajiwa kuwashwa hivi karibuni, nao utaingiza megawati 235 za umeme katika gridi hiyo.
Ukiachana na mradi wa JNHPP, ndani ya kipindi cha miaka mitatu ya Rais Samia, daraja la Magufuli (Kigongo–Busisi) linaendelea kutekelezwa.
Wakati Magufuli anafariki, utekelezaji wa daraja hilo ulikuwa ni asilimia 16, lakini ndani ya miaka mitatu ya Rais Samia, daraja hilo limefikia asilimia 80.1 na ujenzi wake utakamilika Desemba.
Mradi mwingine ni reli ya kisasa (SGR) iliyoachwa na hayati Magufuli ikiwa katika awamu ya kwanza ya ujenzi wa kipande cha Dar es Salaam – Morogoro, ambacho katika uongozi wa Rais Samia kimekamilika na sasa vipande vingine vinaendelea kujengwa.
Vilevile, Serikali ya awamu ya sita imeendelea kuliimarisha Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) kwa kununua ndege mpya. Hayati Magufuli aliacha ndege 11, lakini kwa sasa Rais Samia amenunua ndege zingine tano ikiwemo ndege ya mizigo aina ya Boeing 767-300F.
Tayari ndege aina ya Boeing 737-9 Max ilipokelewa; na imelipa sehemu ya malipo ya ndege aina ya Boeing 737 Max 9, Boeing 787-8 na Boeing 737-7.
Wachambua uamuzi huo
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam (UDSM), Profesa Humphrey Moshi anasema Rais Samia amejitahidi kuibeba miradi ya kimkakati kwa sababu inaendelea lakini kasi ya utekelezaji wa miradi hiyo haiendi kama angekuwepo mwenyewe.
“Tulizindua reli ya Morogoro hivi karibuni, lakini hiyo kitu ingefanyika mwaka mmoja na nusu uliopita. Kwa hiyo, ni kweli tunaona hiyo miradi inaendelea lakini siyo kwa kasi ileile, hata ujenzi wa bwawa la Nyerere, kama mwenyewe angekuwepo, kasi ingekuwa tofauti.
“Tumepata shida ya umeme hapa katikati, watu wanauliza tumekuwa na tatizo la umeme kwa muda mrefu namna hii, mbona wakati ule haikuwa hivi? Moja kwa moja hapa tunajua hili ni tatizo la Serikali,” anasema Profesa Moshi.
Anashauri kwamba Rais Samia awe mkali kwenye miradi hiyo ili ikamilike kwa wake na kutoruhusu ucheleweshaji wake unalisababishia taifa upotevu wa fedha nyingi za walipakodi ambazo zingeweza kutumika kwenye maeneo mengine.