Samia atoa maagizo kwa Dk Biteko, ataka umeme wa uhakika Katavi

Rais Samia Suluhu Hassan wakati akizungumza na wananchi wa Inyonga Wilayani Mlele wakati wa ziara yake mkoani Katavi. Picha na Wizara ya Ujenzi
Muktasari:
- Mkoa wa Katavi unatumia Sh2 bilioni kila mwezi kwa ajili ya kuendesha majenereta kupata umeme, hivyo mkoa huo utaachana na matumizi ya majenereta na kutumia umeme wa Gridi ya Taifa.
Dar es Salaam. Rais, Samia Suluhu Hassan amemuagiza Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko kuhakikisha mkoa wa Katavi unapata umeme wa uhakika kufikia Septemba 2024.
Pia ameliagiza Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) mbali na kuwasha umeme mkoani Katavi, liharakishe usambazaji na uunganishaji wa umeme kwenye taasisi mbalimbali na nyumba za watu.
Rais Samia ameyatoa maagizo hayo leo Jumamosi, Julai 13, 2024 kwenye ziara yake ya kikazi mkoani Katavi akiwa wilayani Mlele kwenye mkutano wa hadhara na wananchi.
Amesema mradi alioukagua wa kupooza umeme wa Inyoga, kazi yake inaendelea vizuri.
“Septemba mwaka huu mkoa huo unakwenda kutumia umeme wa Gridi ya Taifa. Tunakwenda kuachana na majenereta, majenereta ambayo yanatumia Sh2 bilioni kila mwezi kuyaendesha. Sasa tunakwenda kuachana nayo,’’ amesema.
Katika kusisitiza hilo, Rais Samia amesema:”Niiagize Wizara ya Nishati na Tanesco kuhakikisha mradi unakamilika kama tulivyojipanga mwezi wa tisa na Katavi kuanza kupata umeme wa uhakikisha.”
Pia Rais Samia amesema wakati akikagua miradi ya umeme, ameonyeshwa namna Tanesco wanavyojenga laini ya kupokea umeme kutoka Ubungo jijini Dar es Salaam na kusambaza umeme katika maeneo mengine.
Kupitia mradi huo, Rais Samia amesema vituo vitatu vinajengwa, akitolea mfano kituo cha Inyonga ambacho kitapokea umeme kutoka Sikonge.
“Kituo cha Inyonga kitapeleka umeme Mpanda vituo vitatu vinajengwa na mradi huo thamani yake ni Sh48 bilioni tumetumia fedha hizo kuhakikisha mkoa huu unapata umeme wa kutosha,”amesema.
Mbali na hayo, amesema Serikali inakuza usikivu wa Redio ya Taifa na sasa ujenzi wa minara ya kunasa mawasiliano inaendelea kujengwa, ili kuwe na usikivu mzuri ili wananchi wapate taarifa zenye kuwawezesha kufanya uamuzi.
Kuhusu miundombinu ya barabara, amesema Serikali inajenga barabara ya Kibaoni- Mlele km 50, vikonge- Luhafwe km25, Luhafwe-Mishamo km 37 na Kagwera- Karema km110 kwa kiwango cha lami.
Miradi yote ya barabara pamoja na umeme Rais Samia amesema inalenga kuchochea maendeleo ya mkoa huo, hivyo wananchi wautumie umeme hata kwenye shughuli za kilimo cha umwagiliaji.
Akizungumzia suala la uhifadhi wa mazingira, Rais Samia amesema ni muhimu wananchi kutunza mazingira.
“Tunajua kuna uhaba wa ardhi, kuna maeneo ya hifadhi mnatolea macho. Panapotokea haja tukae tuwasiliane tuone namna Serikali itakavyokata kama tulivyokata nyuma ekari 10,000 zilikuwa za wafugaji zikaenda kwa wakulima kama kuna haja nyingine tukae tuzungumze,” amesema.