Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Samia atia neno maadili, uwazi sekta ya ununuzi

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati,Doto Biteko,akizungumza kwa niaba ya Rais Samia Suluhu Hassan, katika jukwaa la 16 la ununuzi wa umma la Afrika Mashariki, lililoanza leo jijini Arusha.

Muktasari:

  • Wizara ya Fedha na Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), zimeboresha udhibiti wa ununuzi wa umma kupitia marekebisho ya sheria, kanuni na taratibu za ununuzi wa umma.

Arusha. Rais Samia Suluhu Hassan amewataka wataalamu wa ugavi na manunuzi kutoka nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kuzingatia maadili, uwazi na uwajibikaji ili kutoa huduma bora kwa wananchi.

Pia amewaasa kuongeza tija kwenye miradi ya maendeleo.

Amesisitiza kuwa fedha nyingi zinazotumiwa katika nchi za EAC zinatokana na kodi za wananchi, hivyo ni muhimu kusimamiwa kwa uangalifu ili kuepusha athari ikiwamo rushwa.

Akizungumza kwa niaba ya Rais Samia, katika ufunguzi wa jukwaa la 16 la ununuzi wa umma la Afrika Mashariki, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko, amehimiza umuhimu wa wataalamu wa ugavi na manunuzi kuzingatia misingi hiyo ili kutoa huduma bora na kutekeleza miradi yenye tija.

Hata hivyo, Dk Biteko amesema viongozi wa EAC wamekuwa wakifanya kazi kwa bidii ili kuleta maendeleo endelevu, ikiwa ni pamoja na kuimarisha hali za kisiasa, kisheria, kiuchumi na kijamii ili kupunguza umasikini, kuunda mazingira bora ya ajira na maendeleo ya wanawake na vijana.

"Tunapotumia fedha za umma kununua bidhaa, huduma au miradi katika nchi zetu, tunapaswa kufahamu hitaji la maendeleo endelevu na ustawi wa ushirikiano baina ya nchi zetu. Fedha hizi zinatokana na kodi za wananchi, hivyo ni lazima tuzingatie maadili, uwazi na uwajibikaji," amesema Dk Biteko kwa niaba ya Rais Samia.

Ameongeza kuwa tofauti na nchi zilizoendelea kiviwanda, nchi za Afrika Mashariki zinategemea sana bidhaa na huduma kutoka nje.

Hivyo, amewasisitiza wataalamu wa ununuzi kujenga uwezo wa kuzalisha bidhaa zinazohitajika ndani ya EAC kabla ya kufikiria kuagiza kutoka nje, ili kukuza viwanda vya ndani na kuinua uchumi wa kanda.

Kwa upande wa Tanzania, Dk Biteko amesema Wizara ya Fedha na Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), zimeboresha udhibiti wa ununuzi wa umma kupitia marekebisho ya sheria, kanuni na taratibu za ununuzi wa umma. Amesema Serikali imeipa Wizara ya Fedha jukumu la kuandaa Sera ya Taifa na Mkakati wa Usimamizi wa Mnyororo wa Ugavi ili kuhakikisha ununuzi na shughuli zote zinazofungamana na ugavi kwenye taasisi za umma, zinafuata sera na mikakati iliyojiwekea.

Tukio hili pia lilienda sambamba na uzinduzi wa Mfumo wa Kielektroniki wa Ununuzi wa Umma (NeST).

Kuhusu mfumo huo,  Dk Biteko amesema ulianzishwa kutokana na changamoto za mfumo wa zamani.

Amesema huu mpya  utasaidia kupunguza gharama za ununuzi na kuongeza kasi, kuondoa matumizi ya karatasi na kupunguza makosa katika mchakato wa ununuzi.

Akizungumza awali, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa PPRA, Dk Leonada Mwagike amesema utengenezaji wa mfumo wa NeST ulianza Julai 18, 2022 na ulianza kutumika Oktoba Mosi, 2023, kwa ushirikiano na wadau mbalimbali.

Dk Mwagike amesema mfumo huo bado haujakamilika, lakini moduli mbili za usajili na utoaji wa zabuni kwa njia ya mtandao zinafanya kazi kwa ufanisi mkubwa hivi sasa.

Naye Mkurugenzi wa PPRA, Dennis Simba amesema kongamano hilo litahusisha mada mbalimbali, zikiwemo utekelezaji wa mfumo wa kielektroniki katika manunuzi na kubadilishana uzoefu kuhusu namna teknolojia inavyoweza kuboresha sekta ya ununuzi.

Nchi nyingine zilizoshiriki kongamano hilo ni Afrika Kusini, Senegal, Zambia na Malawi.