Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Samia aeleza sababu kuendeleza Daraja JP Magufuli

Muktasari:

  • Rais Samia amesema hayo leo, Alhamisi Juni 19, 2025 alipohutubia wananchi wa Mkoa wa Mwanza na maeneo jirani katika hafla ya uzinduzi wa daraja hilo

Mwanza. Rais Samia Suluhu Hassan amesema uamuzi wake wa kusimamia na kuhakikisha anaendeleza utekelezaji wa Daraja la John Pombe Magufuli hadi kukamilika kwake, umetokana na nia ya dhati ya kutimiza maono ya mtangulizi wake, hayati John Magufuli.

Pia, amesema daraja hilo litakuwa alama ya nchi na uthibitisho kwamba, Taifa limepiga hatua ya kiuchumi, uwezo wa kupanga, kutekeleza na kufanikisha mambo yake makubwa.

Ameeleza hayo huku akirejea simulizi ya kusikitisha ya  Rais wa Awamu ya Tano, hayati Magufuli na eneo la Kigongo-Busisi hadi kufikiria kujenga daraja hilo, akisema kwa sababu hiyo ameona hana budi kuendeleza mradi huo na kuukamilisha.

Rais Samia amesema hayo leo, Alhamisi Juni 19, 2025 alipohutubia wananchi wa Mkoa wa Mwanza na maeneo jirani katika hafla ya uzinduzi wa daraja hilo.

Amerejea kilichowahi kusimuliwa na mtangulizi wake, hayati Magufuli aliyenusurika na ajali ya mtumbwi aliotakiwa kupanda na pikipiki yake, lakini aligoma na baadaye kuambiwa ulizama na kusababisha vifo vya watu kadhaa.

“Alipokuwa Rais wetu, ndiyo akasema ile shida na tabu waliyokuwa wanapata wananchi, sasa basi ndiyo akaja na wazo la kujenga daraja hili,” amesema.

Pia, amesema shida hiyo ilimgusa hayati Magufuli kwa namna ya pekee ndiyo sababu akaamua kutekeleza mradi huo.

“Baada ya kuondoka kwake, nikasema nitasimama imara kuhakikisha maono yake yanatekelezwa. Nilifanya hivyo kwa kuwa ahadi yangu kwa Watanzania ilikuwa ni kuyaendeleza mema yote ya awamu zilizopita na kuleta mema mengine mapya,” amesema Rais Samia.

Amesema kuzinduliwa kwa daraja hilo, kunaondoa hadithi za kusikitisha zilizowahi kusimuliwa na hayati Magufuli.

Pia, amesema daraja hilo litakuwa alama ya nchi na uthibitisho kwamba, Taifa limepiga hatua nyingine kiuchumi na ishara Tanzania ina uwezo wa kupanga, kutekeleza na kufanikisha mipango mikubwa.

“Mradi huu, asilimia 92 ya wafanyakazi walikuwa Watanzania, hii inathibitisha daraja hili lilitokana na wazo la Watanzania wenyewe lililogharimiwa na Watanzania na kujengwa kwa nguvu yao. Hii ni fahari nyingine kubwa kwa nchi yetu,” amesema.

Amesema imekuwa fursa ya kukuza maarifa na juhudi wa kutekeleza miradi mikubwa miongoni mwa Watanzania, akisema ni matumaini ujuzi uliopatikana ni kwa faida ya nchi.

“Na hii ndiyo faraja na furaha yangu kubwa na tunayo kila sababu ya kumtukuza Mwenyezi Mungu kwa kutufikisha katika hatua hii, daraja hili limejengwa kwa lengo la kuunganisha barabara kuu ya Usagara na Sengerema ambayo ni muhimu katika ushoroba wa kiuchumi Kanda ya Ziwa,” amesema. 

Katika hotuba hiyo, amesimulia historia ya vivuko katika eneo la Kigongo Busisi, akisema cha kwanza kilinunuliwa mwaka 1968 kilichokuwa na uwezo wa kubeba abiria 15 na hakikuweza kupakia magari.

Ulipofika mwaka 1971, amesema Serikali ilinunua Kivuko cha Mv Mwanza kilichokuwa na uwezo wa kubeba tani 20 sawa na magari madogo matatu hadi manne kulingana na ukubwa wake.

“Jitihada za Serikali hazikuishia hapo, mwaka mmoja baadaye 1972 Serikali iliongeza kivuko kingine kilichojulikana kwa jina la Geita Feri kikiwa na uwezo wa tani 65 kilichobeba magari matatu na abiria 100.

“Geita Feri kwa sasa inafahamika kwa jina la Mv Temesa na kinahudumia katika Kituo cha Ilunda na Luchelele mkoani Mwanza,” amesema Rais Samia.


Kwa mwaka 1977, amesema Serikali ilinunua kivuko kingine cha Mv Sabasaba chenye uwezo wa tani 85, kilibeba magari madogo 10 na abiria 330 na vingine vilinunuliwa mwaka 1985, 2008 na 2018.

Alichokisema Majaliwa

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amekumbushia hali ilivyokuwa mwaka 2017 wakati mikakati ya kujenga daraja hilo na miradi mingine ya kimkakati inasukwa kati ya hayati Magufuli na Samia akiwa makamu wake wa Rais.

Amesema licha ya mwasisi wa mipango na miradi ya kimkakati ikiwamo Daraja la Kigongo-Busisi, Reli ya Kisasa (SGR), Bwawa la Umeme la Mwalimu Nyerere, Barabara ya Juu ya Ubungo (Flyover) na meli kubwa ya Mv Mwanza na Magufuli kufariki dunia Machi 17, 2021 lakini Rais Samia hakukatishwa tamaa kwa kuwa, aliwaita wasadizi wake na kuwaeleza nia ya kukamilisha miradi hiyo.

"Kwa bahati mbaya sana mwaka 2021 Rais Magufuli alifariki ukaingia madarakani, ulianza juhudi za kuiendeleza, nakumbuka uliniita ofisini ukaniambia miradi hii ni yetu lazima tuikamilishe,"amesema Majaliwa.

Amesema katika kuonesha dhamira yake ya kukamilisha miradi hiyo, Rais Samia alifanya jitihada za kutafuta fedha ndani na nje ya nchi ili kuikamilisha.

Amesisitiza kukamilika kwa ujenzi wa daraja la J.P Magufuli na miradi mingine, Rais Samia ametekeleza alichokiahidi, hivyo Watanzania wanapaswa kumuunga mkono na kutomuacha kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.

Picha za harusi, video ruksa

Awali, Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega aliwaambia wakazi wa Mwanza na Kanda ya Ziwa kuwa, shughuli za kijamii katika daraja hilo hazitozuiwa kama kupiga picha mjongeo (video) kwa ajili ya kwaya na qaswida lakini kabla ya kufanya hivyo wahusika waombe kibali kwa wizara hiyo.

“Harusi, matukio ya sherehe ruksa daraja la J.P Magufuli. Hatutakataza kufanya kazi zozote za kijamii kama vile kupiga picha, kurekodi kwaya, wanaotaka kuimba, lakini nataka niwaombe kwamba kabla hujaenda kufaya hivyo, uombe kibali Wizara ya Ujenzi, tunaye Meneja wa Tanroads Mkoa wa Mwanza atakupa kibali cha kufanya hivyo,” amesema Ulega.











Pia, amemshukuru Rais Samia akisema wizara yake ilimuomba aridhie daraja hilo liitwe jina la John Pombe Magufuli naye akaridhia.

“Wakati unapokea kijiti kutoka kwa mtangulizi wako, daraja hili lilikuwa asilimia 25 tu na  Sh152 bilioni zilikuwa zimelipwa, lakini umesimamia mpaka limekamilika kwa asilimia 100 likiwa na thamani ya Sh718 bilioni pamoja na thamani ya kodi, wewe umeweza kulipa zaidi ya Sh450 bilioni,” amesema Ulega.

Amesema daraja hilo ni kielelezo cha uwezo wa Tanzania, kama Taifa kufanya uamuzi na kufanya maendeleo yake yenyewe.

“Kanda ya Ziwa umeiwekea msisitizo mkubwa wa kiuchumi, sasa inakwenda kuchechemka na vijana watapata ajira…umetuelekeza tuondoe msongamano.

“Mwanza sasa ina msongamano, tutajenga barabara ya njia nne, mbili zinazoingia na mbili zinazotoka. Tupo hatua ya mwisho ya utekelezaji,” ameongeza Ulega.

CCM yajivunia

Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Bara, Stephen Wasira amesema chama hicho kiliahidi na kimetekeleza, akieleza kwamba miaka minne iliyopita Rais Samia alitoa matumaini ya kazi inaendelea, akihoji wengine wanaonaje tofauti? Akitaka wasilaumiwe kwa kuwa ni wanafunzi.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda amemuomba Rais Samia kuruhusu vivuko vilivyokuwa vikitumika kabla ya ujenzi wa daraja hilo, kupelekwa kwenye visiwa vya mkoa huo.

Ametoa pendekezo kwamba Kivuko cha Mv Misungwi kipelekwe Kisorya, Wilaya ya Ukerewe, Mv Mwanza iende Nyakalilo-Nkome, Wilaya ya Sengerema na Mv Sengerema ipelekwe Kanyara Wilaya ya Sengerema.

Mtanda amesema mkoa huo wenye idadi ya watu milioni 3.6 ukiwa unachangia asilimia 7.2 ya pato la Taifa, umepokea Sh5.6 trilioni kwa ajili ya miradi ya maendeleo ikiwamo miradi mikubwa ya kimkakati kuanzia mwaka 2021-2025.

Ameitaja baadhi ya miradi hiyo ni ujenzi wa hospitali ya kibingwa wilayani Ukerewe kwa zaidi ya Sh5 bilioni, ujenzi wa soko la kisasa mjini kati kwa zaidi ya Sh20 bilioni na mradi wa chanzo cha maji Butimba utakaozalisha lita 48 milioni kwa siku na kuhudumia watu 400,000.

Hili ndilo Daraja la J.P Magufuli

Daraja hilo la sita kwa urefu barani Afrika limejengwa kwa  gharama ya Sh718 bilioni pamoja na kodi ya ongezeko la thamani huku utekelezaji wa mradi huo ukifanywa na mkandarasi China Civil Engineering Construction Corporation na China Railway 15 Bureau Group Corporation.


Daraja hilo lenye urefu wa kilomita tatu, upana wa mita 28.45 na barabara unganishi zenye urefu wa kilomita 1.66 lilianzwa kujengwa Februari 25, 2020 na kukamilika 2025.