Sakata la Lissu kupigwa risasi laendelea kutokota

Mwonekano wa gari la Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu ambaye alishambuliwa kwa risasi zaidi ya 30 na watu wasiojulikana mkoani Dodoma Septemba 7, 2017. Picha na maktaba
Muktasari:
- Makamu Mwenyekiti wa Chadema (Bara), Tundu Lissu amesema Jeshi la Polisi na Serikali hawajawahi kuwa na nia ya kuchunguza tukio la jaribio la mauaji dhidi yangu
Dar es Salaam. Wakati Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni akisema kinachotoa faraja kwenye suala la upelelezi wa Makamu Mwenyekiti wa Chadema (Bara), Tundu Lissu upelelezi ni pamoja na muhusika mwenyewe (Lissu) kuwepo nchini, mwenyewe ameseama Jeshi la Polisi na Serikali hawajawahi kuwa na nia ya kuchunguza tukio la jaribio la mauaji dhidi yake.
Masauni alieleza hayo jana Jumapili Juni 4,2023 wakati wa mazungumzo kwenye kipindi kinchoongozwa, Msemaji wa Serikali Gerson Msigwa kupitia Clubhouse baada ya kuulizwa na wachangiaji, ni watu gani waliomshambulia Lissu kwa risasi.
Ameeleza ikiwa imepita miaka mitano tangua kiongozi huyo aliposhambuliwa kwa risasi zaidi ya 30 Septemba 7, 2017 na watu wasiojulikana akitoka kuhudhuria vikao vya Bunge ambapo aliwahishwa katika Hospitali ya Rufaa ya Dodoma na kisha kukimbizwa jijini Nairobi nchini Kenya.
“Nitoe wito kwa muhusika mwenyewe (Lissu) pamoja na wengine, watakaoweza kusaidia suala hilo ili liweze kukamilika kwa haraka, hatimaye wahusika waweze kupatikana na kufikishwa kwenye mkondo wa sheria kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi,”amesema Masauni.
Alibainisha kuwa kwenye suala la uchunguzi wa Lissu bado upelelezi unaendelea, kwa kuwa kwenye suala la uchunguzi hakuna ukomo wa muda (time limit).
“Upelelezi bado unaendelea, uchunguzi hauna ukomo wa muda useme ni mwaka mmoja au miwili ndio usitishe, kinachotoa faraja kwenye suala mhusika mwenyewe (Lissu) yupo nchini,”amesema.
Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu Lissu amesema, kauli hiyo, ni kama kauli zao za mwanzo, ni visingizio tu. Kwa nini, kwa mfano, hawajawahi kusema nani aliyeondoa walinzi wote kwenye nyumba za Serikali siku ya shambulio.
“Kwa nini hawajawahi kusema CCTV camera waliyoichukua kutoka jengo nilikoshambuliwa imeonyesha nini na iko wapi? alihoji.
“Kwa nini hawajawahi kunihoji au kuhoji watu wengine ambao wanaweza kuwa mashahidi wa tukio hilo. Kisingizio kilikuwa nimekimbia kesi; lakini tangu nimerudi wamekaa kimya,” amesema.
Aidha Lissu amesema alinyimwa na nimeendelea kunyimwa haki zake za matibabu, ili hali alifukuzwa ubunge kwa kisingizio cha utoro, wakati walikuwa wanajua yuko kwenye matibabu.
Lissu ambaye wakati anashambuli alikuwa Mbunge wa Singida Mashariki, kwa nyakati tofauti amekuwa akivitaka vyombo vya dola, kukamilisha upelelezi ili haki iweze kutendeka ikiwemo kuwabaini waliomshambulia.
Mei 9, mwaka huu baada ya kuliona gari lake lililoshambuliwa kwa risasi ikiwa ni kwa mara ya kwanza likiwa Polisi Dodoma tangu aliposhambuliwa, Lissu alilitaka Jeshi hilo kuwatafuta waliofanya tukio hilo washughulikiwe kwa mujibu wa sheria.
“Mimi ningependa huyo aliyepiga hizo risasi zote hizo atafutwe na ashughulikiwe kwa mujibu wa sheria,” alisema