Prime
Safari ya Katiba mpya kuchochewa na hawa

Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Damas Ndumbaro. Picha na Mtandao
Dodoma. Wakati Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Damas Ndumbaro akieleza mchakato wa kuichambua Katiba iliyopo utaanza Septemba mwaka huu kwa kushirikisha asasi za kiraia, viongozi wa dini na wasomi wa vyuo vikuu, wadau wameeleza hofu ya mchakato huo.
Kwa mujibu wa Dk Ndumbaro, mchakato wa uchambuzi hautashirikisha wanasiasa kwa lengo la kuepuka mawazo yenye kuegemea vyama vya siasa.
Dk Ndumbaro alisema; “Tunaamini asasi za kiraia ndizo zinawakilisha mawazo ya wananchi bila kuegemea katika chama chochote cha siasa, tunaamini wasomi wetu wa vyuo vikuu wanajua mambo mengi kuhusiana na Katiba, hivyo watatusaidia kuelimisha wananchi nao watajua.”
Miongoni mwa wadau waliotilia shaka mchakato huo ni mjumbe wa Jukwaa la Katiba (Jukata), Hebron Mwakagenda aliyetaka wadau wote washirikishwe.
Dk Ndumbaro alisema hayo juzi jioni, baada ya kumalizika mkutano wa kampeni ya msaada wa kisheria wa Rais Samia Suluhu Hassan, maarufu ‘Kampeni ya Mama Samia’ iliyofanyika uwanja wa Majimaji mjini Songea, mkoani Ruvuma.
Mchakato wa Katiba mpya ulianza mwaka 2011 na kukwama mwaka 2014, ukiwa katika hatua ya Katiba iliyopendekezwa, huku Serikali ikieleza sababu ni kupisha uchaguzi wa mwaka 2015.
Hata hivyo, madai ya Katiba mpya yaliendelea hata baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kushika madaraka na Machi 21, 2022 aliitikia wito wa madai ya Katiba mpya kwa kuunda kikosi kazi kilichokuwa chini ya uenyekiti wa Profesa Rweikiza Mukandara.
Kikosi kazi hicho kilikabidhi ripoti yake Oktoba 21, 2022 na kupendekeza mchakato wa Katiba mpya kuanza baada ya Uchaguzi Mkuu 2025.
Januari mwaka huu, Rais Samia alipokutakana na viongozi wa vyama vya siasa nchini Ikulu, jijini Dar es Salaam, alieleza wanakwenda kuukwamua mchakato wa Katiba mpya, kauli aliyoirudia akiwa katika mkutano wa Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha).
Katika Bunge la Bajeti la mwaka 2023/24, Serikali imetenga bajeti ya Sh9 bilioni kwa ajili ya mchakato huo na masuala mengine, yakiwemo marekebisho ya sheria za uchaguzi.
Lakini juzi jioni Dk Ndumbaro alisema kuna athari ya kubadilisha kitu usichokijua.
“Sisi hatusemi kwamba Katiba hii haina upungufu, ndiyo maana tunasema yale mazuri tuyabainishe, kama ni zuri kwa nini tunataka tuliondoe? Kama ni zuri liendelee kuwepo kwenye Katiba mpya, lakini kama ni baya kwa nini liendelee kuwa katika Katiba,” alisema.
Alisema Serikali iko katika mchakato wa kuchambua Katiba, lakini shughuli hiyo hawataifanya wao, bali ni asasi za kiraia, wasomi wa vyuo vikuu na taasisi za dini.
“Tunaamini asasi za kiraia ndizo zinawakilisha mawazo ya wananchi pasipo kuegemea katika chama chochote cha siasa, tunaamini kuwa wasomi wetu wa vyuo vikuu wanajua mambo mengi kuhusiana na Katiba, hivyo watatusaidia kuelimisha wananchi nao watajua,” alisema.
Alisema wanaamini taasisi za dini zina waumini wengi ambao zinawasikiliza kila Ijumaa, Jumamosi na Jumapili na kwamba wakishamaliza hilo watawaeleza kuwa elimu wameitoa, lakini maoni yao na wananchi yanahitajika.
“Hapo ndipo tutaanza Septemba mwaka huu, kwa nini? Kwa sababu sasa tunajipanga, bajeti ndio imepita, hivyo Julai na Agosti tunajipanga ndani ya wizara, ili Septemba tuanze kwenda,” alisema Dk Ndumbaro.
Maoni ya wadau
Akizungumza na Mwananchi, Mjumbe wa Jukwaa la Katiba (Jukata), Hebron Mwakagenda alishauri wanasiasa kuwemo katika mchakato huo wa kuchambua na kuelimisha kwa sababu nao wanawatu wao wa kuwaelimisha.
Alisema walichosema mwaka 2011 wakati mchakato wa Katiba mpya uliokwama ulipoanza ni wanasiasa wawepo lakini wasiteke mchakato wa Katiba.
“Mbona Serikali kama inasuasua. Ni kama inataka kutupiga chenga tena mara ya pili. Mara ya kwanza Kikwete (Rais wa Awamu ya Nne Jakaya Kikwete) mwaka 2014 alitupiga chenga kwamba muda umeisha tunaelekea katika uchaguzi,” alisema.
Maoni hayo yaliungwa mkono na Mkurugenzi wa Jukata, Bob Wangwe aliyesema matarajio ya wadau wengi kuhusu kuanza kwa mchakato wa Katiba ni Serikali kupeleka mapendekezo ya marekebisho ya sheria mbili bungeni.
Alizitaja sheria hizo ni ile ya mabadiliko ya katiba na sheria ya kura ya maoni ili ziendane na mazingira ya sasa.
“Huo ndio utaratibu wa kisheria wa kuanza kwa mchakato wa Katiba, lakini taratibu zote zinazokwenda kinyume na utaratibu wa sheria zinatupa mashaka,” alisema.
Alisema hivi sasa ni kama Rais Samia anaelekea kule kule, baadaye atawaambia muda umeisha, hivyo hilo jambo watalifanya baada ya uchaguzi.
“Kwa nini isiwe sasa hadi Septemba, wanajiandaa nini wakati bajeti imepita?” alihoji.
Kwa upande wake, Askofu wa Dayosisi ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Jimbo la Dodoma, Amon Kinyunyu alisema haiwezekani kuanza mchakato wa Katiba mpya bila kupata maoni kutoka kwa wananchi.
“Viongozi, asasi za kiraia ni kweli wana watu wengi, lakini waongeze watu wengine baadaye kama wafanyakazi, wakulima na wafanyabiashara. Hii itasaidia katika kulitatua jambo hili,” alisema.
Alisema lazima washirikishwe pia wanasiasa kwa sababu pia wana haki ya kutoa mawazo yao kama Watanzania.