Sabaya amkataa mwendesha mashtaka

Aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya akifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi kufunguliwa kesi mpya.
Muktasari:
Aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai Mkoa wa Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya, amemkataa Mwendesha Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).
Moshi. Aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai Mkoa wa Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya, amemkataa Mwendesha Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Tumaniel Kweka kwa kuwa anatokea wilaya ya Hai.
Amewasilisha hoja hiyo leo Jumatano June Mosi, 2022 mbele ya Hakimu Mkazi, Salome Mshasha, Sabaya amesema hana imani na mwendesha mashitaka huyo kwa kuwa anatokea katika wilaya hiyo na kwamba ni mtu aliyedai ni wa visasi na anatumika kisiasa.
Sabaya na washtakiwa wenzake wanne wanaokabiliwa na mashitaka saba likiwamo kosa la Uhujumu Uchumi, kuogoza genge la uhalifu, pamoja na Kujihusisha na Vitendo vya rushwa.
Sabaya amemuomba Rais Samia Suluhu Hassan kuingilia kati kesi hiyo.

Mbali na hoja hiyo lakini kulijitokeza hoja nyingine kupitia kwa wakili Hellen Mahuna, aliyedai washitakiwa hao hawakupelekwa mahakamani hapo kwa kufuata taratibu za kisheria na kwamba mawakili wao hawakupewa taarifa.
Kutokana na malumbano hayo, Hakimu Mshasha ameahirisha kesi hiyo kwa muda wa dakika 10 hadi 15 ili kupitia hoja hizo ili kutoa uamuzi mdogo.