Sababu pekee kuahirisha sherehe za Uhuru
Raisi John Magufuli akitoa salamu za miaka 57 ya Uhuru wa Tanzania Bara, Ikulu jijini Dar es Salaam. Picha na Ikulu.
Muktasari:
Rais John Magufuli ametoa msamaha kwa wafungwa 4,477 na kati yao 1,176 wataachiwa katika maadhimisho ya sherehe za uhuru zinazofanyika Desemba 9, 2018
Dar es Salaam. Rais John Magufuli ametangaza rasmi kuahirishwa kwa sherehe za maadhimisho ya miaka 57 ya Uhuru zilizokuwa zifanyike kesho na badala yake fedha zilizopangwa kwa ajili ya shamrashamra hizo zitatumika kujenga hospitali mpya jijini Dodoma.
Novemba 20, 2018 Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alipokuwa akizungumza na viongozi waandamizi wa Mkoa wa Lindi aliokutana nao mjini humo, alisema fedha zilizotengwa kufanikisha sherehe hizo ni zaidi ya Sh995 milioni.
Hii ni mara ya pili kwa Rais Magufuli kuahirisha sherehe za Uhuru ambapo awali alifanya hivyo Desemba 9, 2015 ikiwa ni mwezi mmoja tangu aingie madarakani na fedha zilizotengwa aliagiza zitumike kupanua kipande cha barabara kutoka Morocco hadi Mwenge jijini Dar es Salaam.
Pia siku hiyo alishiriki kufanya usafi katika maeneo ya kuzunguka Ikulu hadi katika soko la samaki la Feri na kueleza kuwa ni aibu kwa Taifa kukumbwa na kipindupindu kwa sababu ya uchafu.
Akizungumza jana alipokuwa akitoa salamu za sikukuu ya Uhuru kupitia Televisheni ya Taifa (TBC), Rais Magufulialitoa msamaha kwa wafungwa 4,477 kati yao 1,176 alisema wataachiwa huru siku ya kilele cha Uhuru.
Rais Magufuli alisema ili kutekeleza mawazo ya waasisi wa Taifa, Serikali imeamua kuhamishia rasmi makao makuu ya nchi jijini Dodoma.
“Na karibu wahusika wengi wameshahamia kule, nimebaki mimi, nipo kwenye mpango wa kuhamia hivi karibuni,” alisema.
Alisema hali hiyo imechangia kuongezeka kwa mahitaji ya huduma za jamii ikiwamo afya katika Jiji la Dodoma, hivyo Serikali imeamua kujenga hospitali nyingine kubwa itakayosaidiana na ile ya Benjamin Mkapa na Hospitali ya Mkoa wa Dodoma katika kutoa huduma.
Alisema hospitali hiyo mpya itakayoitwa Uhuru itasaidia kuongeza kasi ya utoaji wa huduma za afya jijini humo.
Msamaha kwa wafungwa
Rais alisema msamaha alioutoa kwa wafungwa utawahusu wale ambao ni wagonjwa, wazee, wa kike walioingia gerezani wakiwa wajawazito, walioingia wakiwa na watoto wanaonyonya na wasionyonya pamoja na wafungwa wenye ulemavu wa mwili na akili.
“Hali kadhalika nimeamua kwa wafungwa waliotumikia robo ya adhabu zao wapunguziwe robo ya adhabu zao baada ya punguzo la kawaida la theluthi moja linalotolewa kwenye kifungu cha 49 (1) cha Sheria ya Magereza sura ya 58,” alisema Rais Magufuli.