Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Saa 16 zatumika kutenganisha pacha wa Tanzania walioungana

Madaktari bingwa wakiendelea na upasuaji wa pacha hao. Picha na Mtandao

Muktasari:

  • Madaktari wabobezi wa upasuaji wa watoto wamefanikiwa kuwatengenisha watoto pacha waliozaliwa wameungana kutoka Tanzania, upasuaji uliofanyika kwa saa 16 kutokana na pacha hao kuungana ogani muhimu ikiwemo ini, njia moja ya mkojo huku wakiwa na kiungo kimoja cha uzazi cha kiume.

Saudi Arabia/Dar. Saa 16 zimetumika kuwatenganisha watoto pacha Hassan na Hussein Saidi (2) waliozaliwa mwaka 2021 wakiwa wameungana baadhi ya viungo vyao vya mwili katika kijiji cha Kifurumo kilichopo Wilaya ya Igunga, mkoani Tabora katika upasuaji uliofanyika kwa mafanikio makubwa mjini Riyadh, Saudi Arabia.

Mpaka wanafanyiwa upasuaji wa kutenganishwa, pacha hao walikuwa na uzito wa kilogramu 13.5 kwa pamoja ambapo walikuwa wameungana kwenye kifua cha chini, tumbo, nyonga, ini, utumbo, njia ya mkojo na walikuwa kiungo kimoja cha uzazi wa kiume.

Taarifa zilizotolewa na vyombo vya habari nchini Saudia zimeeleza kuwa upasuaji huo ulifanyika Oktoba 5 kwa hatua tisa na timu ya madaktari wabobezi, wataalamu na wauguzi 35 katika hospitali ya watoto ya King Abdullah iliyopo mji wa King Abdulasis chini ya Wizara ya Ulinzi wa Taifa hilo wakiongozwa na Dk Abdullah Rabeen.

Balozi wa Saudi Arabia nchini Tanzania, Yahya Okiesh akitoa taarifa hiyo, alieleza kuwa timu ya madaktari wa upasuaji nchini Saudi Arabia ilitangaza mafanikio ya upasuaji wa pili wa mapacha wa Tanzania walioungana.

Operesheni hiyo iliyofanikiwa inafuatia ile ya pacha wengine walioungana kutoka Misenyi, Kagera waliotambulika kwa majina ya Anishia na Melanese, ambao walisafirishwa hadi Ufalme wa Saudi Arabia na kurejea Tanzania baada ya upasuaji uliofanikiwa Agosti 2019.

Kwa mujibu wa Balozi Okiesh, Msimamizi Mkuu wa Kituo cha Msaada wa Kibinadamu cha Mfalme Salman (KSrelief) na mkuu wa timu hiyo, Dk Abdullah bin Abdulaziz Al-Rabeeah wameufahamisha ubalozi kuhusu mafanikio hayo.

"Pamoja na ukweli kwamba operesheni ilikuwa ngumu, tumefarijika sana kusikia kuwa upasuaji huo umefanyika kwa mafanikio," amesema Balozi Okeish.

Amesema kabla ya upasuaji huo, Hassan na Hussein walikuwa wakishiriki sehemu ya chini ya kifua, tumbo na nyonga, kila mmoja akiwa na kiungo kimoja cha chini kwa maana ya njia zote za kujisaidia.

Mapacha hao waliokuwa wameungana pia walikuwa wakigawana kiungo cha tatu cha chini ambacho kilikuwa na ulemavu.

Waliungana kwenye ini, matumbo, mfumo wa mkojo, na kiungo kimoja cha uzazi wa kiume, wakiwa na ulemavu katika ukuta wa chini wa tumbo na kibofu cha mkojo.


Balozi Okeish amesema kabla ya upasuaji wa kuwatenganisha pacha hao, Saudi Arabia imefanikiwa kushughulikia kutenganisha mara 133 kutoka nchi 24 kwa kipindi cha miaka 33 tangu mwaka 1990 na kwamba huo ni upasuaji wa 59.

Mwanadiplomasia huyo ametoa shukrani kwa mlezi wa Misikiti miwili Takatifu na Mwana Mfalme kwa msaada wao usio na kikomo kwa mpango wa Saudi wa kutenganisha mapacha walioungana, ambao umeokoa maisha ya watu wengi kote ulimwenguni.

"Msaada wa matibabu ni matokeo ya ushirikiano kati ya uongozi na watu wa nchi hizi mbili. Hospitali ya Taifa Muhimbili ilikuwa imeomba Kituo cha Msaada wa Kibinadamu cha King Salman (KSrelief) kusaidia katika upasuaji huo na bila kusita walikubali,” aliongeza.

Hassan na Hussein waliondoka Tanzania kwenda Riyadh Agosti 23, mwaka huu kwa ndege binafsi baada ya kulazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa takribani miaka miwili.

Hii si mara ya kwanza kwa upasuaji kama huo kufanyika kwa watoto wa Kitanzania ambapo Agosti 31 mwaka jana, jopo la madaktari waliwatenganisha pacha waliokuwa wameungana kifuani, Rehema na Neema ambao ogani zao zilishikana yaani ini, moyo na baadhi ya tishu za ndani.

Upasuaji huo uliodumu kwa saa 7, ulianza saa 3 asubuhi na kumalizika saa 9 alasiri, ulifanyika  kwa ushirikiano kati ya wataalamu wa afya 31 kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na Ireland waliotokea Shirika la Operation Child Life lakini kwa bahati mbaya watoto hao walifariki wakiendelea na matibabu.