Ruto: Nina miezi sijazungumza na Rais Kenyatta
Muktasari:
- Rais mteule wa Kenya, William Ruto ameweka wazi kuwa hajazungumza na Rais Uhuru Kenyatta kwa miezi sasa huku akiahidi kuwa atampigia simu kuzungumza naye.
Dar es Salaam. Rais mteule wa Kenya, William Ruto ameweka wazi kuwa hajazungumza na Rais Uhuru Kenyatta kwa miezi sasa huku akiahidi kuwa atampigia simu kuzungumza naye.
Ruto amesema hayo muda mfupi baada ya Mahakama ya Juu nchini Kenya kutupilia mbali maombi ya kikatiba yalifunguliwa wiki iliyopita na mgombea aliyeshindwa, Raila Odinga kupinga ushindi wa Ruto.
Akitoa uamuzi wa hukumu hiyo huo leo Jumatatu Septemba 5, 2022, Jaji Mkuu Martha Koome amesema Raila na waleta maombi wenzake wameshindwa kuthibitisha kuwa kulikuwa na udanganyifu na uchakachuaji wakati wa mchakato wa kuelekea uchaguzi, siku na baada ya kupiga kura.
Akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya uamuzi huo wa mahakama, Ruto ameweka wazi kuwa hajazungumza na Rais Kenyatta kwa miezi sasa.
“Nina miezi sasa sijazungumza naye lakini nitampigia rafiki yangu Rais Uhuru Kenyatta tuzungumze” amesema Ruto huku akicheka.
Rais Kenyatta alikuwa anamuunga mkono Odinga katika kampeni za uchaguzi huo uliofanyika Agosti 9 mwaka huu.